Tafuta

Papa Francisko: Wito na utume wa binadamu katika shughuli za kilimo, mkazo ni ukarimu na uwajibikaji. Papa Francisko: Wito na utume wa binadamu katika shughuli za kilimo, mkazo ni ukarimu na uwajibikaji.  (ANSA)

Papa Francisko: Wito na Utume wa Binadamu Katika Sekta ya Kilimo: Ukarimu na Uwajibikaji

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kijiji cha Coldiretti, tarehe 15 Oktoba 2023 mjini Roma, anakazia kuhusu wito na utume wa binadamu katika shughuli za kilimo, kwa ukarimu na uwajibikaji; matumizi ya teknolojia rafiki katika kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote pamoja na kuepukana utamaduni wa kutupa unaoshuhudia mamilioni ya watu wakiteseka na kufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Uwajibikaji Kilimo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kijiji cha Coldiretti ni mkutano kati ya ulimwengu wa kilimo na mashirika ya kiraia. Ni Mahali panapoonesha ukaribu wa chakula, mkutano, mazungumzo na jamii. Kijiji cha Coldiretti kiliundwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wakulima na wananchi, ulimwengu wa kilimo cha chakula na taasisi, wadau na viongozi washawishi. Kijiji cha Coldiretti kuanzia tarehe 13-15 Oktoba 2023 kimeyakusanya Makampuni 13 pamoja na washirika elfu mbili kutoka sehemu mbalimbali za Italia, mkutano ambao umefunguliwa na Rais Sergio Mattarella wa Italia. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Mater et Magistra” yaani “Kanisa ni Mama na Mwalimu” uliochapishwa tarehe 15 Mei 1961, kuhusu Wito na utume katika shughuli za kilimo anasema “Katika kazi ya kilimo mwanadamu hupata motisha kwa uthibitisho, maendeleo yake, kwa utajiri wake, kwa upanuzi wake pia juu ya kiwango cha maadili ya kiroho. Kwa hiyo ni kazi ambayo lazima itungwe na kuibuliwa kama wito na utume; yaani, kama jibu la mwaliko kutoka kwa Mungu wa kuchangia katika utekelezaji wa mpango wake wa majaliwa katika historia; na kama kujitolea kwa wema kwa kujiinua mwenyewe na wengine na mchango kwa ustaarabu wa binadamu.” Huu ni wito kwa binadamu kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mater et Magista, 135. Mwenyezi Mungu ameumba ulimwengu wenye mpangilio mzuri, anaumba kwa hekima. Uumbaji ni kielelezo cha wema wa Mungu. Mwenyezi Mungu alitaka uumbaji uwe kama zawadi kwa binadamu, urithi uliokusudiwa na kuaminishwa kwake. Rej. KKK 299.

Wito wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu
Wito wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ufalme wa Mungu

Ulimwengu una uzuri wake na ukamilifu wake wa pekee, lakini haukutoka katika mikono ya Mungu ukiwa umekamilika, lakini uko njiani “in statu viae” kuelekea ukamilifu wa mwisho uliokusudiwa na Mungu ambao bado haujapatikana. Mipango ya Mungu anbayo kwayo anaongoza ulimwengu kufikia utimilifu huo huitwa “Maongozi ya Mungu.” Kumbe wito na utume wa mwanadamu katika shughuli za kilimo ni mchakato wa kuendeleza kazi ya uumbaji; kuleta mageuzi kwa kuzingatia utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, maana yake ni kushiriki kikamilifu katika mpango wa awali wa Mungu. Rej. KKK 302. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa Kijiji cha Coldiretti, tarehe 15 Oktoba 2023 mjini Roma. Baba Mtakatifu anakazia kuhusu wito na utume wa binadamu katika shughuli za kilimo, kwa ukarimu na uwajibikaji; matumizi ya teknolojia rafiki katika kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote pamoja na kuepukana utamaduni wa kutupa unaoshuhudia mamilioni ya watu wakiteseka na kufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Tangu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo cha Agano la Kale, kunaonesha jinsi ambavyo kazi ya kilimo ilivyotoa fursa kwa mwanadamu kujielimisha na kutambua kazi ya uumbaji kama kielelezo cha Agano kati ya Mungu na binadamu, baada ya kuwa ameumba mbingu na nchi.

Papa Francisko Sekta ya Kilimo: Wito na Utume wa Kanisa
Papa Francisko Sekta ya Kilimo: Wito na Utume wa Kanisa

“Siku ile BWANA Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana BWANA Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa 2:4-9.  “Bwana Mungu  akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kutunza.” Mwa 2:15. Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili atekeleze kwa akili kazi ya kutunza mazingira kimaumbile na kimaadili, atumie sheria, kanuni na taratibu za kilimo bora, ili ardhi iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa na hivyo kumwezesha mwanadamu kuwa na utu zaidi, mkarimu pamoja na kuenzi zawadi ya uhai. Kwa kufanya kazi hii, mwanadamu anawajibika na kuwa ni mkarimu zaidi, tayari kutawala kama sehemu ya ushiriki wake katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma na ukombozi wa ulimwengu kutokana na uharibifu pamoja na madhara ya dhambi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, siku hizi walimwengu wanaendelea kushuhudia ukuaji wa teknolojia, ufanisi na utendaji wa kazi kiasi kwamba mtu anaweza kuongeza nguvu zake juu ya asili na hivyo kuzaa matunda mengi zaidi. Lakini utumiaji wa teknolojia usiojali na wa kulazimishwa, unaotumia viwango vya juu vya uzalishaji usioendelevu una bei za juu sana.

Maonesho ya Kijiji cha Coldretti
Maonesho ya Kijiji cha Coldretti

Hali hii inashuhudiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yana madhara makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumekuwepo na uchafuzi mkubwa wa vyanzo vya maji na hewa; pamoja na ukataji ovyo wa misitu ni mambo yanayochangia athari za mabadiliko ya tabianchi. Ongezeko la kiwango cha joto duniani, mafuriko na hali mbaya ya hewa ni mambo yanayochangia kugumisha shughuli za kilimo sehemu mbalimbali za dunia. Waathirika wakuu si tu mazingira nyumba ya wote, lakini pia maskini. Bado ni kitendawili cha “kashfa” cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ulimwengu unaweza kuzalisha chakula cha kutosha kulisha idadi ya watu wote duniani, lakini kuna mamilioni wanaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Kumbe, kila mtu anawajibika kusimama kidete ili kutokomeza vitendo hivi vinavyodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kupitia sera na mikakati yenye kuleta tija na ufanisi. Wakati huu Coldiretti inapotafakari jinsi ya kuongeza tofauti na ubora wa chakula na mazao ya kilimo nchini Italia, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wajumbe kuwakumbuka watu ambao wanateseka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Huu ni mwaliko wa kuwakumbuka na kuwaenzi maskini wanaotafuta njia za kujipatia chakula cha kutosha. Ndoto ya walimwengu wengi anasema Baba Mtakatifu ni kuona ulimwengu ambao watu wanapata maji safi na salama, chakula bora na lishe yenye afya; watu wasiokuwa na fursa za ajira, wanaoteseka kutoka na afya mbaya; watu wasiokuwa na ardhi ya kufanyia shughuli zao; makazi bora pamoja na upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa mahitaji ya watu. Baba Mtakatifu abawaombea wajumbe wa mkutano Coldiretti ili Mwenyezi Mungu awakirimie ujasiri na ari ya kupanda mbegu ya amani ambayo itachangia ujenzi wa Ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu.

Papa Kilimo
15 October 2023, 15:04