Tafuta

Papa Francisko: Waamini Itikieni Wito wa Kukaa na Kristo Yesu

Kristo Yesu leo anatoa mwaliko kwa waamini kutafuta muda utakaowaweka huru, ili kujisadaka kwa ajili ya Mungu, anayewapunguzia mizigo, anayewatakasa na kuponya nyoyo zao; na kuwasaidia kukuza amani, imani na furaha; huyu ni Mungu anayewaokoa kutoka katika upweke hasi na kukosa mwelekeo sahihi wa maisha. Inapendeza na inalipa kweli, ikiwa kama waamini wataweza kutenga muda kwa ajili ya kukaa pamoja na Kristo Yesu katika adhimisho la Ibada ya Misa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karamu ya harusi: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua.” Rej. Mt 22: 1-14. Hii ni karamu ya arusi iliyoandaliwa na mtu mwenye mamlaka, Baba mkarimu anayetoa mwaliko kwa watu kuja kushiriki katika furaha yake kwa uhuru kamili, lakini waalikwa wanatumia vibaya uhuru wao. Lakini, ikumbukwe kwamba, hii ilikuwa ni fursa ya kukutana na kusherehekea arusi ya mwanaye. Mwenyezi Mungu anawaandalia waja wake karamu, kielelezo cha mchakato wa ujenzi wa ushirika na kwamba, watu wote wanaalikwa na ili kushiriki kikamilifu kunahitajika jibu la “Ndiyo.” Kwa hakika Mwenyezi Mungu anatoa mwaliko kwa waja wake, ili kukaa pamoja naye, huku akitoa mwanya wa kukubali au kuukataa mwaliko. Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu bila ya ridhaa yake, lakini hawezi kumkomboa mwanadamu bila ya ridhaa yake. Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote, lakini ni kutokana na upendo wake anaheshimu uhuru wa watoto wake, Mwenyezi Mungu anapendekeza na halazimishi kamwe.

Kristo Yesu anawaalika waamini kuitikia wito wa kuishi pamoja naye.
Kristo Yesu anawaalika waamini kuitikia wito wa kuishi pamoja naye.

Mfalme alitoa mwaliko, lakini waalikwa wakaukataa mwaliko, Mwenyezi Mungu anatoa mwaliko, lakini binadamu anaukataa mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kutokujali, wakaenda zao, mmoja shambani mwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake wakawatenda jeuri, na kuwauwa. Pamoja na vituko vyote hivi, Mfalme, bado alithubutu kutoa mwaliko na kati yao walikuwemo pia maskini, kiasi kwamba, arusi ikajaa wageni. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Dominika ya 28 ya Mwaka A wa Kanisa, tarehe 15 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, mara nyingi waamini hawatilii maanani mwaliko, kwa kisingizio cha kukosa muda, Kristo Yesu leo anatoa mwaliko kwa waamini kutafuta muda utakaowaweka huru, ili kujitoa sadaka kwa ajili ya Mungu, anayewapunguzia mizigo ya maisha yao, kwa kutakasa na kuponya nyoyo zao, anawasaidia kukuza amani, imani na furaha; huyu ni Mungu anayewaokoa kutoka katika mabaya, upweke hasi pamoja na kukosa mwelekeo sahihi wa maisha. Inapendeza na inalipa kweli, ikiwa kama waamini wataweza kutenga muda kwa ajili ya kukaa pamoja na Kristo Yesu katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu.

Papa Francisko anawaalika waamini kutenga musa kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu
Papa Francisko anawaalika waamini kutenga musa kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu

Hapa ni mahali muafaka pa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu; ni mahali pa sala na huduma ya upendo, kwa sababu ni faraja kubwa kuwasaidia maskini na wanyonge mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu ni kupoteza muda na hivyo wanajikuta wakijifungia katika ulimwengu na ubinafsi wao, jambo linalosikitisha sana. Baba Mtakatifu anapenda kuwahoji waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Je, wanaitikiaje mwaliko wa Mungu katika maisha yao? Katika maisha yao ya kila siku, Je, Mwenyezi Mungu ana nafasi gani? Je, ubora wa maisha yao unategemea kitu gani: Pengine ni shughuli zao za kila siku, muda wa utawala binafsi au ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na jirani na hasa wahitaji zaidi? Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa kwa “Ndiyo” yake alitengeneza nafasi kwa Mwenyezi Mungu, awasaidie waamini kuwa ni wasikivu wa mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Karamu ya Bwana
15 October 2023, 14:39

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >