Papa Francisko: Ukweli Mbele ya Mungu na Ukweli Nafsini: Dhambi na Ufisadi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya neno la Mungu, Dominika ya 26 ya Mwaka A wa Kanisa, Mwinjili Mathayo anaweka mbele ya waamini mfano wa wana wawili katika kutimiza mapenzi ya Baba yao. Wa kwanza alipoambiwa na Baba yake kwenda kufanya kazi katika shamba la mzabibu akajibu kwa haraka kwamba, anaenda, lakini asiende. Wa pili naye akamwambia vilevile, lakini akasema, “sitaki”; baadaye akatubu, akaenda! Rej. Mt 21:28-32. Kwa hakika kwenda kufanya kazi katika shamba la mzabibu kunahitaji moyo wa majitoleo na kujisadaka bila ya kujibakiza, licha ya kutambua kwamba, kama watoto wa mwenye shamba wanayo haki ya kurithi mali na utajiri wa Baba yao! Jambo la msingi linalowekwa mbele ya waamini hapa ni ukweli mbele ya Baba yao na ukweli katika nafsi zao! Mtoto wa kwanza alikataa, wa pili alikosea, lakini akabaki kuwa mkweli mbele ya Baba yake, na mkweli nafsini mwake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe Mosi Oktoba 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mtoto wa kwanza alijibu kwamba, anaenda, lakini hakwenda, kwani hakukusudia kutoka moyoni mwake kutekeleza mapenzi ya Baba yake, wala hakutaka kujadiliana wala kuzungumza na Baba yake.
Ni mtoto aliyeficha ukweli na kutawaliwa na uvivu, ili kuficha uso wake. Kwa hakika mtoto wa kwanza hakuonesha utii wala heshima kwa Baba yake ingawa alikuwa huru kabisa kumwambia kwamba, hataki. Hizi ni dalili za mtenda dhambi na fisadi, kwa sababu ili kuficha hali yake ya kutotii, anakataa kuzama katika majadiliano na mazungumzano katika ukweli na uwazi. Mtoto wa pili aliyesema “hataki” lakini baadaye akatubu na kwenda shambani, si mkamilifu lakini ni mkweli kutoka nafsini mwake, ingawa ingependa tangu mwanzo kusema, “Nakwenda”, hapa anaonesha matokeo ya ujasiri wake, unaomwajibisha na kutenda ukweli katika mwanga angavu. Msingi huu wa ukweli unapelekea majadiliano yanayomrejesha katika hatua na njia sahihi. Kwa hakika ni mdhambi, lakini si fisadi. Ikumbukwe kwamba, kwa mdhambi daima kuna matumaini ya wokovu, lakini kwa fisadi kuna ugumu wake kutokana na unafiki pamoja na tabia yake ya kuficha ukweli, hali ambayo inampelekea kusutwa daima na dhamiri fuatizi!
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao mbele ya matukio haya mawili, ili kuangalia ikiwa kama wanaishi maisha katika mwanga wa ukweli na ukarimu, kwa kuendelea kujitahidi kutekeleza mapenzi ya Mwenyezi Mungu, tayari kusema, “Ndiyo” hata kama “Ndiyo” hii ina gharama zake! Hata pale inaposhindikana kutekeleza mapenzi ya Mungu, waamini wawe waaminifu na wa kweli mbele ya Mungu, tayari kumwonesha udhaifu na mapungufu yao. Baba Mtakatifu anawauliza waamini, Je? Pale wanapoteleza na kuanguka dhambini, wako tayari kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani? Au wanaendelea kujificha na kuona kwamba, mambo yote yako sawa, ili waonekane kama watu wema na wazuri. Kila mwamini ni mdhambi, lakini Je, katika maisha kuna ndago za ufisadi? Bikira Maria, kioo cha utakatifu, awasaidie waamini kuwa ni Wakristo wa kweli!