Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 19 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza tafakari mintarafu wakimbizi na wahamiaji mintarafu Injili ya Msamaria Mwema. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 19 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza tafakari mintarafu wakimbizi na wahamiaji mintarafu Injili ya Msamaria Mwema.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko: Shuhudieni Injili ya Msamaria Mwema Kwa Wakimbizi na Wahamiaji

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 19 Oktoba 2023 ameongoza tafakari mintarafu wakimbizi na wahamiaji katika mwelekeo wa Injili ya Msamaria Mwema. Mwinjili Luka anakazia kuhusu Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alimwona mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai. Huu ndio mwaliko anaoutoa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1. Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana na: mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, kunako mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha baharini na jangwani
Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaopoteza maisha baharini na jangwani

Maadhimisho ya Siku ya 109 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki.” Kauli mbiu hii inapania pamoja na mambo mengine kukuza tafakari na ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe. Kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia nk. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 19 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ameongoza tafakari mintarafu wakimbizi na wahamiaji katika mwelekeo wa Injili ya Msamaria Mwema. Mwinjili Luka anakazia kuhusu Msamaria mmoja katika kusafiri kwake, alimwona, akamhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai. Huu ndio wito na mwaliko anaoutoa Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.
Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaohatarisha sana maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufungua malango yake kwa wakimbizi na wahamiaji, kama ilivyokuwa kwa Msamaria alithubutu kuokoa maisha yam tu yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Hata leo hii kuna watu wanaohatarisha maisha yao huko jangwani, misituni na kwenye mito, maziwa na bahari. Ni watu wanaoteswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi, kiasi hata cha kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Mara nyingi hawa ni watu wanaokimbia: majanga asilia, vita pamoja na vitendo vya kigaidi kama inavyojitokeza kwa sasa. Kuna watu ambao hawawajali hata kidogo, kielelezo cha ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa huruma na mapendo kwa sababu huu ndio utambulisho wa Mwenyezi Mungu katika mioyo ya wanadamu. Itakumbukwa kwamba, mtindo wa Mungu unasimikwa katika maneno makuu matatu: Ukaribu, Huruma na Upole na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Ukristo uliopelekea yule Msamaria mwema kutangaza na kushuhudia wema wa Mungu na udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kama Msamaria Mwema kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji katika mateso yao.

Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.
Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Hii ni changamoto ya kujiandaa kikamilifu katika mchakato wa kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; iwe ni fursa kwa jamii kuku ana kukomaa katika ukarimu, kwa kuwashirikisha pamoja na kujenga mazingira ya amani na utulivu. Ni vyema jamii ikajenga utamaduni wa kudumisha usalama barabarani, ili kusitokee watu wakaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Hii ni changamoto ya kujizatiti kikamilifu katika mapambano ya mitandao ya biashara haramu ya binadamu pamoja na utumwa mamboleo, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanatumia njia halali katika kupata hifadhi. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na majadiliano ya sera za kisiasa mintarafu idadi ya watu duniani, pamoja na ukuaji wa uchumi, ili wakimbizi na wahamiaji waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini zinazowajibisha ili kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji linalotarajia kuongezeka maradufu kwa siku za usoni.

Papa Wakimbizi
20 October 2023, 14:32