Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Kufunga Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu : 29 Oktoba 2023

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Majira ya Saa 4:00 za Asubuhi kwa Saa za Ulaya, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika awamu ya kwanza, ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu "Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume." Huu ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Awamu ya Kwanza Ngazi ya Kiulimwengu yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 kwa Sala na Mkesha wa Kiekumene, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa ukimya, ili kumsikiliza Roho Mtakatifu na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa muhimu ya ujenzi wa umoja na udugu ndani ya Kanisa. Watu wa Mungu walisali pamoja na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujikita katika mageuzi yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulitakasa Kanisa kutokana na mapungufu yake. Ukimya ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni muhimu hata katika mchakato wa ujenzi wa umoja miongoni mwa Wakristo, kwani sala ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja.

Tarehe 29 Oktoba 2023 Papa Francisko anafunga Maadhimisho ya Sinodi
Tarehe 29 Oktoba 2023 Papa Francisko anafunga Maadhimisho ya Sinodi

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, 2023 Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Katika mahubiri yake aligusia changamoto alizokabiliana nazo Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akainua macho yake mbinguni na kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa hekima na akili anayeona mema yaliyofichika, yanayokuwa, mbegu ya Neno la Mungu linalopokelewa kwa moyo mnyoofu, mwanga wa Ufalme wa Mungu unaoendelea kung’ara hata katikati ya usiku wa giza. Kumbe, mwono wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, ni jicho linalopokea changamoto na mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho ya Sinodi, ujenzi wa umoja, ushiriki na utume
Maadhimisho ya Sinodi, ujenzi wa umoja, ushiriki na utume

Baba Mtakatifu anasema, Mwinjili Mathayo katika sehemu hii ya Injili 11:2-24 anaelezea changamoto katika maisha na utume wa Kristo Yesu, licha ya miujiza aliyotenda, bado watu walikuwa na shingo ngumu kiasi cha kushindwa kutubu na kumwongokea Mungu; Kristo Yesu akashutumiwa kuwa ni mlafi na mnywaji, lakini pamoja na mambo yote haya akainua macho yake kumtukuza Mwenyezi Mungu. Mwanzoni mwa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu anasema, Baba Mtakatifu, Mababa wa Sinodi wanahitaji jicho la Kristo Yesu linalobariki na kupokea kwa ukarimu na wala si jicho linalosheheni majanga ya maisha ya mwanadamu, sera na mikakati ya kisiasa au mapambano ya kiitikadi. Sinodi si bunge linalotaka kufanya mabadiliko. Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum laboris” kwa Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023, inagusia kuhusu: Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Sifa za Kanisa la Kisinodi; Mwelekeo wa Maadhimisho ya Kanisa la Kisinodi: Majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi.

Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa
Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa

Huu ni umoja unaong’ara, alama na chombo cha ushirika na Mwenyezi Mungu na alama ya umoja kati ya binadamu. Uwajibikaji katika utume na jinsi ya kushirikishana karama katika huduma ya Injili. Ushiriki, utawala na madaraja: Je ni mchakato, miundombinu na taasisi gani zinapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi? Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu. Mababa wa Sinodi wametekeleza dhamana hii kwa mikutano pamoja na majadiliano yaliyofanyika kwenye makundi madogo madogo kadiri ya lugha, yanayojulikana kama “Circoli minori” ili kujenga utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana ili kwa pamoja waweze kumsikiliza Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Majira ya Saa 4:00 za Asubuhi kwa Saa za Ulaya, anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika awamu ya kwanza, ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu.

Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa
Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa linawahitaji viongozi wanaoweza kujisadaka katika maisha yao kwa ajili ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Viongozi wa Kanisa waoneshe dira na njia ya kufuata kwa mfano na ushuhuda wa maisha yao. Dhana ya ushiriki na uwajibikaji imeendelea kupewa kipaumbele cha pekee anasema, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Ushiriki mkamilifu katika uongozi, toba na wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari, tayari kushirikishana karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Kanisa linahamasishwa kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake.

Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo
Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo

Mababa wa Sinodi wanakazia pia wongofu wa ndani na majiundo ya awali na endelevu kwa watu wa Mungu ndani ya Kanisa, ili kukua na kuendelea kukomaa kama Kanisa, tayari kujikita katika mabadiliko ya mawazo. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu limekuwa ni jukwaa la kusikilizana, kubadilishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wa Kanisa, tayari kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa, tayari kutembea kwa pamoja, ili kufikia malengo ya Kanisa: kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Askofu mkuu Tarcisius Isao Kikuchi, SVD, wa Jimbo kuu la Tokyo nchini Japan, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, Katibu mkuu Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC., ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, amefisia sana dhana ya ukimya katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu; mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalofumbatwa katika umoja na utofauti wa tamaduni na mahali wanapotoka watu wa Mungu. Caritas Internationalis itaendelea kuwa ni chombo cha huduma na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake sanjari na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene sehemu mbalimbali za dunia. Naye Sr. Mary Teresa Barron, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amejikita katika ushuhuda wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi mintarafu Kanisa Katoliki Barani Afrika kwa kukazia umuhimu wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo.

Sinodi ni chombo cha umoja na huduma
Sinodi ni chombo cha umoja na huduma

Jumuiya ndogondogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani” Koinonia.” Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia.” Lengo kuu ni kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Kimsingi, Jumuiya ndogondogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, ni chombo kinachosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maisha ya Jumuiya ndogondogo za Kikristo sanjari na maisha ya kitawa ni vielelezo tosha kabisa vya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na kwamba, kila mwamini anayo nafasi, wajibu, dhamana na haki zake katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Sinodi Ya Maaskofu
21 October 2023, 13:45