Tafuta

Baba Mtakatifu anawasihi waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani bila kuchoka kwani kwa sasa hali ni tete huko Palestina, Israel pamoja na Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu anawasihi waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani bila kuchoka kwani kwa sasa hali ni tete huko Palestina, Israel pamoja na Ukanda wa Gaza.  

Papa Francisko Atoa Wito wa Kusitisha Vita Ukanda wa Gaza

Baba Mtakatifu anawasihi waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani bila kuchoka kwani kwa sasa hali ni tete huko Palestina, Israel pamoja na Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu anawataka wahusika kutoa mwanya kwenye Ukanda wa Gaza ili misaada ya kiutu iweze kuwafikia waathirika wa vita, lakini jambo la msingi ni kusitisha vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye Ijumaa tarehe 27 Oktoba 2023 ili kufunga, kusali na kufanya toba ili kuombea amani sehemu mbalimbali za duniani. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha vita, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Kwa hakika vita si suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu bali ni chanzo kikuu cha maafa yanayowatumbukiza watu wengi katika hali ya umaskini, magonjwa na ujinga. Mwaliko huu wa sala ulitolewa pia kwa waamini wa Makanisa na dini mbalimbali ulimwenguni. Siku hii ilihitimishwa kwa Ibada maalum ya kuombea amani duniani, majira ya Saa 12: 00 jioni kwa saa za Ulaya kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni siku ambayo ilipata mwitikio mkubwa kutoka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alitumia fursa hii, kuwashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuungana pamoja naye: kufunga, kusali na kufanya toba kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawasihi waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani bila kuchoka kwani kwa sasa hali ni tete huko Palestina, Israel pamoja na Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu anawataka wahusika kutoa mwanya kwenye Ukanda wa Gaza ili misaada ya kiutu iweze kuwafikia waathirika wa vita, lakini jambo la msingi ni kusitisha vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu.

Papa Francisko akiongoza sala ya kuombea amani duniani
Papa Francisko akiongoza sala ya kuombea amani duniani

Kwa upande wake Kardinali Pierbattista Pizzaballa, OFM., Patriaki wa Yerusalemu, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 ameiweka wakfu Nchi Takatifu chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. “Ee Bikira Maria, Mama wa Mungu na Mama yetu, Malkia wa Palestina na wa Nchi Takatifu, wakati huu wa majaribu tunakugeukia wewe kwa sababu unatupenda na unatujua: Hakuna wasiwasi wa mioyo yetu ambao umefichwa kwako. Mama wa rehema, ni mara ngapi tumeona utunzaji wako wa macho na uwepo wako wa amani! Huachi kutuongoza kwa Kristo Yesu, Mfalme wa Amani. Hata hivyo ubinadamu umepotoka kutoka kwenye njia hiyo ya amani. Umesahau mambo tuliyojifunza kutokana na misiba ya hivi karibuni, sadaka za mamilioni ya watu waliotumbukia katika vita. Kwa dhambi zetu tumevunja moyo wa Baba yetu wa mbinguni, ambaye anatamani tuwe ndugu wamoja. Sasa kwa aibu tunalia: Utusamehe, Bwana! Mama Mtakatifu, katikati ya mapambano na udhaifu wetu, katikati ya Fumbo la uovu ambalo ni uovu na vita, unatukumbusha kwamba, Mungu kamwe hawaachi waja wake, lakini anaendelea kututazama kwa upendo. Amekupa sisi na kuufanya Moyo wako Safi kuwa kimbilio la Kanisa na kwa wanadamu wote. Sasa tunabisha kwenye mlango wa Moyo wako Mtakatifu. Sisi ni watoto wako wapendwa. Tuna hakika kwamba, katika nyakati za taabu zaidi za historia yetu, hautakuwa kiziwi kwa maombi yetu na utatusaidia. Ndivyo ulivyofanya kule kwenye harusi ya Kana ya Galilaya, ulipomwomba Yesu, ili kuhifadhi furaha ya karamu ya arusi, ulimwambia: "Hawana divai" (Yn 2: 3). Sasa, Ee Mama, rudia maneno hayo, kwani katika siku zetu wenyewe tumeishiwa na divai ya matumaini, furaha imetoweka, udugu umefifia. Tumesahau ubinadamu wetu na kutapanya zawadi ya amani. Tunahitaji sana msaada wako wa mama!

Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu
Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu

Malkia wa Rozari, utufanye kutambua hitaji letu la kusali, kufanya toba na kuongoka. Waongoze viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na wale wanaoamua hatima ya Mataifa, ili waamue mintarafu: haki na ukweli, na kufanya kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Malkia na mama yetu, waoneshe wenyeji wa nchi yako njia ya udugu wa kibinadamu. Katikati ya ngurumo za silaha, geuza mawazo yetu kuwa ya amani, na panga zetu ziwe majembe. Mguso wako wa kimama utulize wale wanaoteseka na kukimbia kutokana na vita. Kukumbatio lako la kimama liwe ni faraja kwa wale waliojeruhiwa au kulazimishwa kukimbia kutoka majumbani mwao, waliopoteza wanafamilia wao, wafungwa na waliopotea na mateka. Mama Mtakatifu wa Mungu, uliposimama chini ya Msalaba, Yesu, akiona mwanafunzi kando yako, alisema: "Tazama mwana wako" (Yn 19:26). Kwa njia hii, alimkabidhi kila mmoja wetu kwako. Kwa mwanafunzi, na kwa kila mmoja wetu, alisema: "Tazama, Mama yako" (Yn 19:27). Mama Maria, sasa tunatamani kukukaribisha katika maisha yetu na historia yetu. Katika saa hii, wakati watu wa Nchi Takatifu wanakugeukia wewe, moyo wako unadunda kwa huruma kwao na kwa watu wote wanaoangamizwa na vita, njaa, ukosefu wa haki, na umaskini. Kwa hivyo, Mama wa Mungu na Mama yetu, kwa Moyo wako Safi tunajikabidhi kwa dhati na kujiweka wakfu sisi wenyewe, Kanisa letu, wanadamu wote, watu wa Mashariki ya Kati, na haswa watu wa Nchi Takatifu, ambayo ni nchi yako, kwa kuwa uliifadhilisha kwa kuzaliwa kwako, fadhila zako na huzuni zako, na kutoka hapo umemtoa Mkombozi kwa ulimwengu. Jalia kwamba vita viishe, na amani isambae katika miji na vijiji vyetu. Kwa maombezi yako, rehema ya Mungu imwagike duniani na sauti ya amani irudi ili kuadhimishwa katika siku zetu. Uliwahi kukanyaga mitaa ya nchi yetu; tuongoze sasa kwenye njia za amani. Amina.”

Kuombea Amani
31 October 2023, 14:33