Tafuta

2023.01.04  Picha ya Papa Pio VII. 2023.01.04 Picha ya Papa Pio VII. 

Papa akumbuka Papa Pio VII,kuwa alikuwa balozi wa amani

Katika ujumbe kwa askofu,Douglas Regattieri,wa Cesena-Sarsina Baba Mtakatifu Francisko anakumbuka sifa za Papa Chiaramonti miaka 200 iliyopita baada ya kifo chake kwamba alijua jinsi ya kuishi kwa unyenyekevu wa kuigwa mfano na kuonesha uwezo na busara,mbele ya wale waliokuwa wanamzuia Libertas Ecclesiae.

Na Angella Rwezaula, Vatican.

Kitendo cha Kamanda kupanda kuta za Jumba kuu na kuingia kwenye chumba cha Papa, kumteka nyara na kumpeleka Ufaransa  ilikuwa hatima ambayo Papa Pio VII aliteseka  kati ya usiku wa tarehe  5 na 6 Julai 1809, wakati uhusiano na Mtawala Napoleon ulikuwa umefikia kiwango cha chini kabisa na Roma alikuwa amechukuliwa na askari wake. Kutoka hapo kulianza misukosuko ya Papa Chiaramonti, mwenye asili ya Cesena  Italia kama mtangulizi wake Pio  VI, ambaye alipanda hadi kiti cha Petro mnamo tarehe 21 Machi 1800. Licha ya "fedheha ya uhamisho" huko Fontainbleau, ambayo ilidumu hadi Januari 1814, Papa Pio VII alijua jinsi kuishi kwa unyenyekevu wa kuigwa mfano sawa na aliokuwa ameonesha, pamoja na"uwezo na busara, kabla ya "wale waliozuia Libertas Ecclesiae". Haya yanaoneka katika Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika fursa ya miaka mia 200 tangu kifo cha Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII.

Uhuru wa Kikanisa na urithi wa kiroho

Katika Ujumbe huo aliouelekeza kwa Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo la Cesena - Sarsina, Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kuwa, maadhimisho muhimu ya kumbukumbu ya miaka mia mbili ya kifo cha Mtumishi wa Mungu Papa Pius VII ni tukio la furaha kwake kutoa salamu za dhati kwake, kwa ndugu mpendwa, na jumuiya nzima ya kiraia na kikanisa ya Cesena-Sarsina, ambayo inakumbuka pamoja na  shukrani mwana mashuhuri, mchungaji shupavu, mlinzi makini wa Kanisa. Kwa wale wanaoshiriki katika mipango mingi inayoonesha"mwaka wa Chiaramonti", amependa kuwasilisha ukaribu wake wa kibaba pamoja na mawazo ya matashi mema. Katika kusoma tena maisha ya Mtangulizi huyo anayeheshimika, mtu mwenye imani kubwa, upole, ubinadamu na huruma, ambaye alijitokeza kwa ajili ya umahiri wake na busara mbele ya wale walikuwa wanazuia Libertas Ecclesiae, yaani uhuru wa kikanisa,  hisia za shukrani na kusifiwa zinaibuka kwa ajili ya urithi wa kiroho uliobaki na unyoofu wa Kiinjili aliouunga mkono kwa majaribu magumu katika kipindi cha miaka ishirini na tatu ya Upapa wake.

Kujitolea kupunguza mateso

Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba licha ya msukosuko wa kisiasa na kijamii uliotokea karne hiyo, yeye, kwa kuaminiwa akijiachia kwa mapenzi ya Mungu, alikubali fedheha ya uhamisho kwa unyenyekevu wa kielelezo, akimtolea Bwana kila kitu kwa manufaa ya Kanisa. Aidha Papa ameandika kuwa Papa Chiaramonti alikuwa mtu mwenye akili ya kuona mbali, ambaye alijighushughulisha kwanza katika Abasia ya Wabenediktini ya Cesena na baadaye ile yaMtakatifu Paolo Nje ya Ukuta jijini  Roma, na hivyo kupata maandalizi makubwa ya kitaalimungu ambayo yalitolewa kwa ulimwengu wa kitaaluma. Zaidi ya hayo, pamoja na utamaduni uliothibitishwa aliojipambanua nao, pamoja na fadhila dhahiri alizokuwa nazo, katika umri mdogo aliitwa kuwa Askofu katika majimbo mawili tofauti. Kama mchungaji alisimama nje kwa ajili ya karama yake na wema wa roho; kwa hakika, katika kipindi cha miaka ya huduma yake ya uaskofu hakusita yeye binafsi kufanya kila awezalo kuwajali watu, akijitolea kupunguza mateso mengi ya wale waliokuwa wakikabiliwa na hali mbaya.

Hakuogopa vizuzi katika kutangaza Injili 

Kwa hakika, Papa Francisko amesema kuwa tukizingatia kipindi cha kihistoria ambacho Papa Pius VII aliishi, hatuwezi kujizuia kuona hekima kuu ambayo kwayo aliweza kuwa “balozi wa amani” kwa wale waliotumia mamlaka ya muda. Akiwa amekabiliwa na hali ya kisiasa yenye utata na kitendo cha kustaajabisha ambacho kilitishia salus animarum, yaani afya ya roho  yeye, kwa utulivu wa mtu ambaye daima anatumaini uingiliaji kati wa Mungu, alifanya kila kitu bila kushindwa katika utume wake kama "mlinzi na kiongozi wa kundi" na, licha ya vizuizi vilivyowekwa, aliendelea bila woga wowote kutangaza nguvu ya faraja ya Injili ya Kristo, kulingana na roho ya Heri inayowaita wapatanishi watoto wa Mungu (Rej. Mt 5:9). Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anawakabidhi waamini wa Jimbo hilo jukumu la kujulisha ipasavyo maisha na kazi ya kichungaji ya Mrithi huyo mpendwa wa Mtume Petro, mwananchi mwenzao, ili aweze kuamsha shauku hiyo hiyo katika huduma ya wengine na kujenga jamii yenye maelewano, na kuonesha amani kama njia ya matumaini, mazungumzo ya heshima na upatanisho wa Kikristo.  Papa akiwakabidhi chini ya  ulinzi wa kimama wa Bikira Maria, na akiomba maombezi ya Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII, kwa hiari yake amewambariki  kila mmoja, na amewaomba, tafadhali, wasisahau kumuombea.

Papa katika Ujumbe wake anamsifu Papa Pio VII kwa uvumilivu na unyenyekevu
13 October 2023, 11:23