Tafuta

Mwenyeheri Giuseppe Beotti alijisadaka kuwalinda, kuwatetea na kuwasaidia Wayahudi hata kuweza kukimbilia nchini Uswisi. Mwenyeheri Giuseppe Beotti alijisadaka kuwalinda, kuwatetea na kuwasaidia Wayahudi hata kuweza kukimbilia nchini Uswisi.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mwenyeheri Don Giuseppe Beotti: Ukarimu wa Kichungaji kwa Wayahudi

Mwenyeheri Don Giuseppe Beotti ni mchungaji aliyeonesha upendo wa kichungaji, kama chaguo makini la maisha na utume wake. Katika umaskini wake, akageuza Parokia kuwa ni chemchemi ya amana na utajiri wa Kanisa, kwa kusaidiwa zaidi na wanaparokia walionesha moyo wa ukarimu na upendo kwa wahamiaji na wakimbizi. Alijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwalinda kondoo aliokabidhiwa na Mama Kanisa, kielelezo cha upendo na ukarimu wa kichungaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu, tarehe 30 Septemba 2023 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Don Giuseppe Beotti aliyeuwawa kikatili kunako tarehe 20 Julai 1944 kutoka na chuki dhidi ya imani (Odium fidei). Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria Assunta na Santa Giustina di Piaccenza” Jimbo Katoliki la Piaccenza-Bobbio, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe Mosi Oktoba 2023 alimtaja Mwenyeheri Don Giuseppe Beotti kwamba, alikuwa ni mchungaji kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwalinda kondoo aliokuwa amekabidhiwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Kifo chake ni matokeo ya upendo wa dhati kwa Wayahudi ambao wengi wao walikuwa ni wahamiaji kutoka nchini Yugoslavia.

Mwenyeheri Giuseppe Beotti: Mfano wa Upendo wa kichungaji kwa Wayahudi
Mwenyeheri Giuseppe Beotti: Mfano wa Upendo wa kichungaji kwa Wayahudi

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Wenyeheri na Watakatifu, katika mahubiri yake anasema, Don Giuseppe Beotti alijisadaka kuwalinda, kuwatetea na kuwasaidia kukimbilia nchini Uswisi. Lakini kwa utawala wa Kinazi, ukarimu kwa Wayahudi lilikuwa ni kosa la jinai, na adhabu yake ilikuwa ni kifo! Ni mchungaji aliyeonesha upendo wa kichungaji, kama chaguo makini la maisha na utume wake. Katika umaskini wake, akageuza Parokia kuwa ni chemchemi ya amana na utajiri wa Kanisa, kwa kusaidiwa zaidi na wanaparokia walionesha moyo wa ukarimu na upendo kwa wahamiaji na wakimbizi. Don Giuseppe Beotti alionesha upendo na ukarimu, kiasi hata cha kutoa hifadhi kwa Mapadre waliokuwa uhamishoni! Lakini jambo ambalo liliwachukiza watawala wa kinazi ni kile kitendo cha Don Giuseppe Beotti kugawa chakula kwa maskini na wahitaji zaidi mbele ya Kanisa, kitendo ambacho kilishuhudiwa na utawala wa kinazi na kuamua kumfutilia mbali kutoka katika uso wa nchi. Kardinali Marcello Semeraro, anasema, Mwenyeheri Don Giuseppe Beotti ni kiongozi aliyejipambanua katika kuonesha umoja na mshikamano katika maadhimisho ya Ibada na Liturujia Takatifu yaliyomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku kwa njia ya huduma. Itakumbukwa kwamba, tangu Kanisa la Mwanzo sadaka na ukarimu kwa maskini kimekuwa ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Don Beotti
03 October 2023, 14:32