Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 15 Oktoba 2023 atachapisha Waraka wa Kitume kuhusu Ujumbe wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 15 Oktoba 2023 atachapisha Waraka wa Kitume kuhusu Ujumbe wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu,   (Vatican Media)

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu: Jubilei ya Miaka 150 Tangu Kuzaliwa Kwake: Uaminifu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 15 Oktoba 2023 atachapisha Waraka wa Kitume kuhusu Ujumbe wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, kielelezo cha imani: “C’est la Confiance” Yaani “Ni Uaminifu”: Uso Mtakatifu kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 150 tangu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alipozaliwa huko nchini Ufaransa. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu awasaidie waamini waweze kuwa na imani thabiti na utume kwa Kanisa.

Na Sr. Veronica Silvester Buganga, CMTBG – Roma.

Kila mwaka ifikapo tarehe 1 Oktoba, Mama Kanisa humwadhimisha Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kwa heshima ya Bikira na Mwalimu wa Kanisa na tangu mwaka 1927 aliteuliwa kuwa ni msimamizi wa wamisionari wote duniani pamoja na Mtakatifu Francisko Xsaveri. Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba linapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika kuombea shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwamko na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 15 Oktoba 2023 atachapisha Waraka wa Kitume kuhusu Ujumbe wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa, kielelezo cha imani: “C’est la Confiance” Yaani “Ni Uaminifu”: Uso Mtakatifu kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 150 tangu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alipozaliwa huko nchini Ufaransa. Baba Mtakatifu anamwomba Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waweze kuwa na imani thabiti na waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kanisa. Theresa wa Mtoto Yesu alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 Alencon na baadae kuhamia Lisieux nchini Ufaransa.  Theresa ni mtoto wa tisa kuzaliwa na kitinda mimba kwenye familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin ambao sasa Kanisa limewaweka kuwa mfano na kioo kwa familia zote za Kikristo. Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto wao kiimani na katika maadili ya kikiristo. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu aliaga dunia tarehe 30 Septemba 1897, akatangazwa Mtakatifu mwaka 1925, mnamo mwaka 1927 Papa Pio XI akamtangaza kuwa ni msimamizi wa utume wa Kanisa.

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa

Katika maandiko yake anasema wito wangu ni upendo. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu katika umri mdogo amekutana na matatizo mengi na majaribu makubwa, kama vile kuuguliwa na wazazi, kwanza mama hadi akashindwa kumnyonyesha, pia kubaki yatima baada ya kifo cha mama yake. Akaanza kumzoea dada yake mkubwa lakini akapatwa na uchungu wa kutengana nae mwaka 1882 Paulina alipoingia kwenye Shirika la Wakarmeli. Theresa alitamani na yeye aingie utawani mapema iwezekanavyo ila kwa umri wake mdogo hakuweza kupokelewa kwenye monasteri kwa kuzingatia ugumu wa maisha ya sadaka za utawa wa ndani. Hakukata tamaa, mwaka 1887 akaenda hadi Roma kuhiji ili akutane na Papa Leo wa XIII, ili ampe ruhusa, Papa Leo XIII alimsikiliza na kumshauri asubiri bado ni mdogo, alisikitika ila akapokea kwa matumaini na utulivu. Kuingia Utawa wa Wakarmeli: Mungu hakukawaia kumwonjesha furaha ya uvumilivu na matumaini yake, mara baada ya hija Askofu alimruhusu, Theresa aliingia kwenye monasteri ya Wakarmeli tarehe 9 Aprili 1888 akiwa na umri wa miaka 15.  Aliweka Nadhiri za kwanza tarehe 8 Septemba 1890 sanjari na Sikukuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria. Aliifurahia siku hiyo kwa kuwa ni Bibi arusi wa Yesu na Mama wa roho za watu, tayari kujitoa kama sadaka ya kuteketezwa na upendo wa Mungu. Siku hiyo aliomba pia neema ya kuendelea kubaki akiwa mnyenyekevu na mtu mwenye kiasi. Katika monasteri yake alijishughulisha na kazi ndogo ndogo alizopewa na mkubwa wake. Kunako mwaka 1893 aliteuliwa kuwa mlezi wa wanovisi, akafanya utume huu kwa bidii. Alitamani kuona upendo unakuwa ni msingi wa maisha na utume wake, ili aweze kuwa yote kwa ajili ya wote.

Kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu
Kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu

Utakatifu wake unapata chimbuko lake katika fadhila ya: imani, matumaini na mapendo ya kina kwa Yesu Kristo uliomwezesha kufanya mang’amuzi na kuiishi njia yake ndogo ya: unyenyekevu, uvumilivu pamoja na kujiachia kabisa katika mikono ya Yesu na Bikira Maria. Aliamini na ndio ilikuwa dira ya maisha yake kuwa kila tendo hata kama ni dogo kiasi gani ukilifanya kwa upendo linaleta baraka na neema kubwa. Theresa wa Mtoto Yesu anatufundisha kuwa ni kwa njia ya sadaka ndogondogo tunapata utakatifu, matendo madogo ya kila siku kuyafanya kwa upendo thabiti yanamfurahisha Mungu. Mtakatifu Theresa alijitoa mzima mzima kwa Mungu. Aliunganisha mateso yake ya kila siku na yale ya Yesu Msulibiwa pamoja na dhoruba nyingi akajaliwa wepesi uliong’ara kwenye uso wake.  Aliteseka bila kupoteza furaha maana alishirikiana na Yesu kwa kila hali, alijisemea “Theresa peke yake hawezi kitu, Theresa na Yesu anaweza yote. Alionja na kuitegemea huruma ya Mungu, kiasi kwamba alijisikia kuwa Yesu ni rafiki yake wa karibu. Katika kutafakali fumbo la Umwilisho, katika sehemu ya mwisho ya maandishi yake kwenye picha ya Mtoto Yesu anasema “siwezi kumwogopa Mungu aliyejifanya mdogo hivi kwa ajili yangu…Mimi nampenda! Kwa kuwa yeye ni upendo na huruma tu!” Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, tangu utotoni alijengeka katika tunu msingi za Kikristo, akazama zaidi katika fumbo la Utatu Mtakatifu. Alikuwa na kiu kubwa ya kuwa mtakatifu, aliongozwa na Maandiko Matakatifu, hasa Injili na Nyaraka za Mtume Paulo.  Alisoma maisha ya watakatifu akaona elimu yao kuwa ni ya hali ya juu na akatafuta na kuvumbua njia iliyomfikisha haraka mbinguni. Ngazi iliyomsaidia kupanda kila siku kwenda juu, “Njia ndogo” inaakisiwa katika Injili ya Mathayo 18:3, “Msipoongoka na kuwa kama watoto wadogo hamtaingia katika ufalme wa mbingu”. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anasema sikimbilii ile nafasi ya kwanza bali ya mwisho, kama kielelezo cha unyenyekevu, imani na matumaini kama ya mtoto mikononi mwa baba alivyo salama, Theresa alimpenda saana baba yake na baba alimlea kama Malkia wake, Theresa anamfananisha na kumchukulia Mungu kama Mfalme wake.

Utakatifu unapata fadhila: imani, matumaini na mapendo
Utakatifu unapata fadhila: imani, matumaini na mapendo

MAISHA YA SALA: Ni muungano wa karibu kabisa na Mungu, maneno yaliyotawala muda wa sala binafsi ni kumwambia “Yesu nakupenda, Mungu wangu nakupenda” aliziimba kwa furaha sifa kuu za Mungu, kwa Mtakatifu Teresia sala na sadaka ndizo nguzo kuu ambazo zilimwimarisha. “Sala ya 8 Septemba 1890.” Ee Yesu mpenzi wangu wa kimungu! Nisaidie nisipoteze vazi langu la pili la ubatizo! Nizuie utakapoona naelekea kutenda dhambi kwa makusudi hata kama ni ndogo, nisitafute kikingine isiopokuwa wewe, viumbe visiwe na thamani kwangu na mimi kwao ila wewe Yesu uwe yote, …Yesu nakuomba amani ya ndani na upendo ambao sio mimi ila wewe ndani yangu, niko radhi kufa shahidi kiroho au kiroho na kimwili ili kutimiza mapenzi yako na kuifikia sehemu ambayo ulitangulia kuniandalia. Yesu niwezeshe kuokoa roho nyingi, leo isipotee hata moja na roho zote za toharani zivushwe kwenda mbinguni. Amina. UTUME wake wa pekee ni kumfanya Yesu ajulikane na apendwe na watu wa nchi zote, alifanya hivyo kwa njia sala na sadaka ndogondogo.Theresa alikuwa na shauku kubwa ya kuwa mmisionari, alitamani afike duniani kote akihububiri upendo wa Mungu katika Fumbo la Msalaba na ufufuko wa Bwana harusi wake Yesu Kristo, hakuweza kwenda kimwili kwa vile alikuwa mtawa wa ndani pia afya yake kwa muda mrefu ilikuwa ni tete sana hivyo akatolea mateso ya ugonjwa na mateso mengine aliokutana nayo kwa ajili ya wamissionari, aliwaandikia barua kuwatia moyo na zaidi Theresa amefika duniani kote kwa njia ya sala. Katika kufanikisha adhima yake ya kumfanya Yesu atambulike na apendwe na watu wa mataifa yote alijitoa mhanga kwa ajili ya wongofu wa wakosefu wakubwa, akiamini katika upendo wa Mungu wenye huruma isiyo na mipaka. Aliwaombea wakosefu neema ya toba na wongofu wa ndani. Bwana Franzini alikuwa mfungwa aliyehukumiwa kunyongwa, Theresa alisoma katika gazeti habari zake na akapata uchungu kuwa hii roho inakaribia kuangamia maana Franzini hakuwa mchamungu, Mtakatifu Theresa akamsihi Yesu amguse amjalie neema ya kutubu dhambi zake ili baada ya adhabu ya kifo, roho yake isiende motoni. Yesu aliisikiliza sala ya Theresa na kumpa ishara ya wongofu wa huyo mfungwa Franzini ambaye alibusu Msalaba ishara ya toba na wongofu wa ndani. 

Mt. Theresa wa Mtoto Yesu: Sala kwa Mapadre
Mt. Theresa wa Mtoto Yesu: Sala kwa Mapadre

KUWAOMBEA MAPADRE: Siku iliyotangulia nadhiri zake, mbele ya Yesu wa Ekaristi Takatifu alijitafiti na kusema nimekuja kwenye Monasteli ya Wakarmeli kwa ajili ya kuziokoa roho, kusali hasa kuwaombea mapadre. Alitamani kuishi upendo wa kidugu katika jumuiya.  Alipenda kukaa karibu na masista wenzake hasa wale wasio mvutia na waliokuwa wanamsababishia mateso, wazee walalamishi aliwachukulia kwa upendo, kuwavumilia na kuwasamehe. Hamu kubwa ya Mtakatifu Theresa ilikuwa ni kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu, kukutana na kukaa na Yesu mpenzi wa moyo wake kila siku na katika uzima wa milele.  Maneno ya mwisho ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kabla ya kukata roho kwa ugonjwa wa Kifua kikuu, TB, uliomtesa kwa muda kitandani anasema “Mungu wangu nakupenda.” Maneno yaliyotawala maandishi yake yote “Yesu Nakupenda” kabla ya kifo aliahidi akisema “Nitakaa mbinguni nikiwatendea watu mema duniani, ndizo neema tele kabisa nitakazowanyeeshea mvua ya mawaridi. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Bikira na Mwalimu wa Kanisa katika maisha yake yameandikwa kwanza kwa lugha ya Kifaransa na baadaye yakafsiriwa kwa lugha mbalimbali.  Kwa lugha ya Kiswahili Kitabu cha maisha yake kinaitwa “Ua la Upendo” na kwa “Kihaya cha ndani kabisa” kinaitwa “Akamuli ke ngonzi”, yaani hadi raha katika masuala ya utamadunisho! Hapa kumenoga hadi raha!

Theresa wa Mtoto Yesu

 

13 October 2023, 14:41