Tafuta

Mwinjili Luka anawakumbusha waamini kwamba, utume wa Kanisa unawezekana tu, ikiwa kama wakristo watajifungamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala. Mwinjili Luka anawakumbusha waamini kwamba, utume wa Kanisa unawezekana tu, ikiwa kama wakristo watajifungamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala. 

Mtakatifu Luka Mwinjili: Shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu Kwa Watu wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 18 Oktoba 2023 amesema, Mwinjili Luka anawakumbusha waamini kwamba, utume wa Kanisa unawezekana tu, ikiwa kama wakristo watajifungamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala pamoja na kujiaminisha mikononi mwake, tayari kuyafanya mapenzi yake. Kitaaluma Mwinjili Luka alikuwa ni daktari na mmissionari mwenza wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Ushuhuda wa Imani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 18 Oktoba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Luka, Mwinjili na mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume kinachofafanua: taalimungu, historia na imani ya Kanisa la mwanzo chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu tangu siku ile ya Pentekoste ya kwanza, mwanzo wa Kanisa la Kristo na tangu wakati huo, Roho Mtakatifu anawaongoza waamini kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu: “Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.” Mdo 1:8. Kristo Yesu ni Masiha aliyesubiriwa na Taifa la Israeli; alikuwa ni utukufu kwa Israeli na mwanga wa Mataifa. Rej. Lk 2:23. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini, wadhambi na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote hawa waweze kushuhudia na kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 18 Oktoba 2023 amesema, Mwinjili Luka anawakumbusha waamini kwamba, utume wa Kanisa unawezekana tu, ikiwa kama wakristo watajifungamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala pamoja na kujiaminisha mikononi mwake, tayari kuyafanya mapenzi yake. Kitaaluma Mwinjili Luka alikuwa ni daktari na mmisionari mwenza wa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Ni mwinjili pekee anayesimulia maisha ya utoto wa Yesu katika familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa namna ya pekee, Mwinjili Luka anaguswa na mahangaiko ya wagonjwa na maskini, ndiyo maana Injili hii inaitwa Injili ya faraja inayojikita katika sadaka ya Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu! Luka kwa njia ya Kitabu cha Matendo ya Mitume analionesha Kanisa ambalo limefuata mafundisho ya Mitume ili kukuza na kudumisha: umoja, ushirika na upendo unaopata chimbuko lake katika maadhimisho ya Sala ya Kanisa na Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa!

Mwinjili Luka ni mwandishi pia wa Kitabu cha Matendo ya Mitume
Mwinjili Luka ni mwandishi pia wa Kitabu cha Matendo ya Mitume

Na Padre Liston Lukoo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Dar es Salaam.

"Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. basi, mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake"(Lk 10:2). Leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mt. Luka, Mwinjili. Yeye si mmoja kati ya Mitume kumi na wawili, bali anatajwa kuwa alifuatana na Mt. Paulo katika safari zake za kimisionari na kichungaji (Mdo 16:10; 2Tim 4:11; Flm 1:23).  Mt. Paulo anamtambulisha kwetu kama "Daktari wetu mpendwa"(Kol 4:14). Huyu ndiye mwandishi wa Injili kama ilivyoandikwa na Luka na kitabu cha Matendo ya Mitume kinachosimulia miaka ya mwanzo ya Kanisa. Kwa asili, historia inamtaja Luka kuwa na asili ya Ugiriki, mpagani aliyeongoka na kuwa mkristo. Tunaposoma injili ya Luka, tunagundua kwamba aliandika zaidi juu ya uhusiano kati ya Kristo na watu wa tabaka la chini: fukara; wakosefu; wanawake… Kama mwandishi wa Injili, Luka aliandika Injili yake kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu baada ya kusikiliza simulizi za wale walioshi na kumsikia Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani. Mwinjili Luka anaandika Injili yake akitofautiana na Wainjili wengine, hasa Mwinjili Marko na Mwinjili Yohane, kwa kuwa ni Luka na Mathayo pekee ndio walioandika habari za utoto wa Yesu, japo hata wao pia wanatofautiana.  Ni Luka pekee ambaye anasimulia habari za kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, kupashwa habari Bikira Maria kwamba atakuwa Mama wa Mungu na kutolewa Yesu hekaluni.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu

Kama Mwinjili, Luka anaonekana katika picha akiwa pamoja na ng'ombe kama ishara ya sadaka, kwa maana injili yake inatoa habari za Zakaria, kuhani wa Kiyahudi mwenye jukumu la kumtolea Mungu sadaka za wanyama. Utambulisho huu unaonekana katika maono ya Ufunuo wa Yohane (Ufu 4:7). Mwinjili Luka anamwona Yesu kama Mtumishi wa watu na sadaka kwa ajili ya ulimwengu mzima. Mwinjili Luka ameliachia Kanisa hazina kubwa kwa maisha yetu ya kiroho. Ametuachia Habari Njema kwa ajili ya wokovu wetu. Ametuachia utajiri mkubwa juu ya umuhimu wa sala kwa mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe. Aidha, Luka ametuachia mfano mzuri wa kuwa watu wa huruma na kusamehe kwa mfano wa Yesu mwenyewe, na hasa kwa mfano wa hadithi ya Baba Mwenye Huruma, maarufu kama Injili ya Mwana Mpotevu. (Lk 15:11-32). Mwinjili Luka anaweza kufananishwa na wale Sabini na wawili ambao Bwana aliwatuma wawili wawili wamtangulie kule ambako Yeye mwenyewe alitaka kwenda (Rej. Lk 10:1). Ni ukweli kwamba hatuwezi wote kuwa Mitume kwani "Mungu ameweka katika kanisa: kwanza Mitume, pili manabii, tatu waalimu..."(1 Kor 12:28).

Mtakatifu Luka, Mwinjili na Mwandishi wa Kitabu cha Matendo ya Mitume
Mtakatifu Luka, Mwinjili na Mwandishi wa Kitabu cha Matendo ya Mitume

Tutambue kwamba katika hadhi yetu ya ubatizo kila mmoja ni miongoni mwa wale sabini na wawili wanaotumwa kupeleka Habari Njema ya wokovu. Utume huu si wa maaskofu tu, au mapadre tu au watawa tu, bali ni wajibu wa kila mmoja. Sikukuu ya Mtakatifu Luka inatufundisha kwamba: Ni Yesu mwenyewe tu ndiye anayeita na kumtuma yule amtakaye (Lk 10:1). Aidha, kila anayeitwa na kutumwa anaalikwa kumtumainia Mungu katika utume wake (Lk 10:4); kwani Mungu anajua mahitaji ya kila mmoja wetu. “Ninyi msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi, kwa maana hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja nayo. Bali tafuteni ufalme wa Mungu, na hayo mtaongezewa” (Lk 12:29-31). Tunapomwomba Mungu apeleke watenda kazi katika mavuno yake, tunajiombea sisi sote wabatizwa ili tuwe tayari kutumwa na kutenda kazi ya Bwana, kuuambia ulimwengu kwamba "Ufalme wa Mungu umekaribia..."(Lk 10:9). Mt. Luka, Mwinjili atuombee ili tuweze kutimiza vyema wajibu wetu wa ubatizo: kuwa wamisionari.

Mwinjili Luka

 

18 October 2023, 15:31