Tafuta

Papa Francisko amekutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa Masista Wadogo wa Yesu "Piccole Sorelle di Gesù" Papa Francisko amekutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa Masista Wadogo wa Yesu "Piccole Sorelle di Gesù"  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mkutano Mkuu wa Shirika la Masista Wadogo wa Yesu: Mwanamke Msamaria

Baba Mtakatifu amekutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi na mbili wa Shirika la Masista Wadogo wa Yesu na kumpongeza Mama mkuu wa Shirika Sr. Eugeniya-Kubwimana kutoka Rwanda na washauri wake wakuu. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu umuhimu wa kumtafuta Mwenyezi Mungu, ushuhuda wa Injili pamoja na upendo kwa maisha yaliyofichika, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Yesu anakutana na Mwanamke Msamaria.” Rej. Yn 4:5-42.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Shirika la Masista Wadogo wa Yesu ni jumuiya ya kitawa inayoongozwa na maisha na nyaraka za Mtakatifu Charles de Foucauld, iliyoanzishwa na Dada Mdogo Magdeleine wa Yesu (Madeleine Hutin) tarehe 8 Septemba 1939.

Shirika la Masista Wadogo wa Yesu ilianzishwa 8 Septemba 1939
Shirika la Masista Wadogo wa Yesu ilianzishwa 8 Septemba 1939

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 2 Oktoba 2023 amekutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi na mbili wa Shirika la Masista Wadogo wa Yesu na kumpongeza kwa namna ya pekee Mama mkuu wa Shirika Sr. Eugeniya-Kubwimana kutoka Rwanda na washauri wake wakuu. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu umuhimu wa kumtafuta Mwenyezi Mungu, ushuhuda wa Injili pamoja na upendo kwa maisha yaliyofichika, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Yesu anakutana na Mwanamke Msamaria.” Rej. Yn 4:5-42. Baba Mtakatifu anasema, mchakato wa kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha ni jambo la muhimu sana, kama ilivyokuwa kwa yule Mwanamke Msamaria, ili kujenga utamaduni wa kusikiliza na kumwabudu Kristo Yesu kama alivyofanya Mtakatifu Charles, kiasi cha kumwezesha kuwa na mawazo na maono ya uwajibikaji sanjari na kujikita katika huduma kwa Kanisa. Kama ilivyokuwa kwa Mwanamke Msamaria, Kristo Yesu anawakirimia waja wake upendo na uwezo wa kupokea changamoto na kuzifanyia kazi mintarafu mwanga wa Injili.

Sr. Eugeniya Kubwimana, Mama Mkuu wa Shirika
Sr. Eugeniya Kubwimana, Mama Mkuu wa Shirika

Pili ni ushuhuda wa Injili unaofumbatwa katika udugu wa kimataifa unaoundwa na watawa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kielelezo cha maisha ya Kiinjili yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, baada ya kumtafuta na kumwona, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani, kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa wale wanaomtafuta, ili kuvunjilia mbali utamaduni wa kutoguswa na mahitaji ya wengine. Huu ni ushuhuda wa udugu unaotolewa kwa maskini, watoto wachanga, wazee, wasiokuwa na elimu, wagonjwa na wadhambi; mafundisho makuu kutoka kwa Kristo Yesu. Tatu ni upendo kwa maisha yaliyofichika, kielelezo makini cha Kristo Yesu, kinachopata chimbuko lake katika Fumbo la Umwilisho, Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Shirika la Masista Wadogo wa Yesu, wajikite katika kumwilisha ndani mwao maisha yasiyokuwa na makuu. Baba Mtakatifu anatambua fika changamoto wanazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na upungufu wa miito ya kitawa inayopelekea kufungwa kwa jumuiya na nyumba za kitawa. Watawa wenye umri mkubwa ni changamoto pevu, lakini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni chombo mahususi mikononi mwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwapelekea waja wake faraja ya Kiinjili. Baba Mtakatifu amewashukuru watawa hawa kwa utume wao Jimbo kuu la Roma, hasa miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hatarishi na wale wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii.

Masista Wadogo wa Yesu

 

 

02 October 2023, 14:23