Mahojiano Maalum kati ya Papa Francisko na Shirika la Habari la Argentina Telam!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na Shirika la Habari la Argentina Télam kuhusu: Mgogoro wa ubinadamu; Manabii wa uwongo, vita na madhara yake; Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Kazi kama kipimo cha utu, heshima na haki msingi za binadamu, matumizi ya teknolojia ya akili bandia na matumaini kama fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesu na kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kuhusu mgogoro wa ubinadamu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mchakato wa maisha ya ndani ya mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa jamii kuwafunda vijana wa kizazi kipya kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, amana na utajiri mkubwa wa maisha ya mwanadamu yanayofumbatwa katika tafakari inayojikita katika lugha ya kichwa, moyo na mikono. Baba Mtakatifu anasema, kazi ni kipimo cha utu, heshima na haki msingi za binadamu: Utu, heshima na haki msingi za mwanadamu ndicho kipimo halisi cha heshima ya kazi. Kazi ni kwa ajili ya mwanadamu na wala si mwanadamu kwa ajili ya kazi na kwamba, kazi ni sehemu ya utambulisho wa mwanadamu. Huu ni mwendelezo wa ushiriki wa mwanadamu katika kazi ya uumbaji na mchango wake katika kazi ya ukombozi. Kutokana na madhara ya dhambi ya asili, Kristo Yesu alitoa mwelekeo mpya wa kazi, kuwa ni kielelezo cha ukombozi; utu na heshima ya binadamu. Kielelezo cha kazi na utume huu, ni mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu!
Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo muhimu sana katika sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Binadamu wanapaswa kuangaliana na kuchukuliana kama ndugu wamoja na kwamba, kazi nzima ya uumbaji ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na inashangaza sana machoni pa binadamu! Kazi inamtambulisha mwanadamu na kumwezesha kutekeleza karama na mapaji mbalimbali aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Kwa njia ya kazi, mwanadamu anashiriki pia katika mpango wa kazi ya uumbaji iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu na hivyo kushiriki pia katika mchakato wa mshikamano na jirani zake. Licha ya shida na magumu yanayojitokeza katika kazi, lakini inamwezesha mtu kukua na kukomaa, pamoja na kutekeleza ndoto za maisha yake. Baba Mtakatifu anakazia kuhusu haki msingi za wafanyakazi, vinginevyo watageuka na kuwa ni watumwa wa kazi, Baba Mtakatifu anasema, baadhi ya watu wanamsema kuwa ni Mkomunisti, lakini yeye anafuata tunu msingi za Kiinjili.
Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya teknolojia ya “akili bandia” katika sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolojia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya “akili bandia” kutokana na mchango wake mkubwa! Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu wa kuwa wazi na makini katika kukabiliana na matumizi ya teknolojia ya akili bandia. Kuhusu migogoro, kinzani na vita sehemu mbalimbali za dunia, jambo la msingi ni kujikita katika ulinzi na usalama; majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kutafuta na kukuza msingi wa haki na amani. Vita ni adui mkubwa wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani, ustawi na mafao ya wengi, kwa kushirikiana na kushikamana na wote.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Mtakatifu Yohane XXIII alitia nia ili kuhakikisha kwamba, Kanisa linafanya mageuzi makubwa, nia ambayo ilitekelezwa kwa maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na baadaye Sinodi za Maaskofu zilizoasisiwa na Mtakatifu Paulo VI. Hii inatokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya taalimungu, taalimungu maadili pamoja na sayansi ya Kanisa sanjari na ufasiri wa Maandiko Matakatifu kadiri ya mwanga wa Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesu na kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanaweza kuhesabiwa haki kwa neema yake ili wapate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama tumaini lao. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Mwanadamu akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821. Baba Mtakatifu anasema, analo wazo la kutembelea Argentina, lakini kwa sasa anapenda kujielekeza zaidi katika hija ya kitume itakayomwezesha kutembelea nchi ya Papua New Guinea.