Tafuta

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya kiulimwengu ni kuanzia tarehe 4-hadi tarehe 29 Oktoba 2023: Ushiriki wa waamini walei. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya kiulimwengu ni kuanzia tarehe 4-hadi tarehe 29 Oktoba 2023: Ushiriki wa waamini walei.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Kiulimwengu Ni kuanzia Tarehe 4-29 Oktoba 2023

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 4 Oktoba anazindua rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume kwa ibada ya Misa Takatifu inayowashirikisha Makardinali wapya waliotangazwa na kusimikwa tarehe 30 Septemba 2023. Hii ni fursa ya kumsikiliza Roho Mtakatifu sanjari na ujenzi wa umoja na udugu wa watu wa Mungu. Hiki ni kipindi cha ukimya katika Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau.

Mkesha wa Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu
Mkesha wa Sala ya Kiekumene kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu

Wafuasi hawa baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, walirejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina maana ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza Ngazi ya Kiulimwengu yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 kwa Sala na Mkesha wa Kiekumene, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa ukimya, ili kumsikiliza Roho Mtakatifu na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa muhimu ya ujenzi wa umoja na udugu ndani ya Kanisa. Watu wa Mungu walisali pamoja na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujikita katika mageuzi yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulitakasa Kanisa kutokana na mapungufu yake. Ukimya ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni muhimu hata katika mchakato wa ujenzi wa umoja miongoni mwa Wakristo, kwani sala ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja.

Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo
Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo

Mara baada ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Mababa wa Sinodi, Dominika tarehe Mosi, Oktoba 2023 walianza mafungo ya kiroho yaliyoongozwa na Padre Timothy Radcliffe, aliyejikita katika kuonesha Kanisa la Kristo Yesu lisilo na mipaka linalotembesa katika njia ya matumaini. Na kwa upande wake, Sr Ignazia Angellini amekazia umuhimu wa watu wa Mungu kutembea bega kwa bega na Kristo Yesu, tayari kutoa baraka na kuwa ni baraka “Homo vivens, gloria Dei”, tayari kuliwezesha Kanisa kutembea katika njia ya amani. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi uwawezeshe watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu, Jiwe walilolikataa waashi, kielelezo cha utimilifu wa maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni muda muafaka wa kujenga ukimya, kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu tayari kujikita katika ujenzi wa kukutana na Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha.

Sinodi ya Maaskofu
03 October 2023, 15:28