Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, 2023 Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama ufunguzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, 2023 Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama ufunguzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu: Mahubiri ya Papa Francisko: Ufunguzi

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amegusia changamoto alizokabiliana nazo Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akainua macho yake mbinguni na kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa hekima na akili anayeona mema yaliyofichika, yanayokuwa, mbegu ya Neno la Mungu linalopokelewa kwa moyo mnyoofu, mwanga wa Ufalme wa Mungu unaoendelea kung’ara hata katikati ya usiku wa giza. Hii ni changamoto ya kujikita katika toba na wongofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Awamu ya Kwanza Ngazi ya Kiulimwengu yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 kwa Sala na Mkesha wa Kiekumene, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa ukimya, ili kumsikiliza Roho Mtakatifu na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa muhimu ya ujenzi wa umoja na udugu ndani ya Kanisa. Watu wa Mungu walisali pamoja na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujikita katika mageuzi yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulitakasa Kanisa kutokana na mapungufu yake. Ukimya ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni muhimu hata katika mchakato wa ujenzi wa umoja miongoni mwa Wakristo, kwani sala ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha.

Ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu
Ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, 2023 Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Katika mahubiri yake amegusia changamoto alizokabiliana nazo Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akainua macho yake mbinguni na kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa hekima na akili anayeona mema yaliyofichika, yanayokuwa, mbegu ya Neno la Mungu linalopokelewa kwa moyo mnyoofu, mwanga wa Ufalme wa Mungu unaoendelea kung’ara hata katikati ya usiku wa giza. Kumbe, mwono wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, ni jicho linalopokea changamoto na mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Mwinjili Mathayo katika sehemu hii ya Injili 11:2-24 anaelezea changamoto katika maisha na utume wa Kristo Yesu, licha ya miujiza aliyotenda, bado watu walikuwa na shingo ngumu kiasi cha kushindwa kutubu na kumwongokea Mungu; Kristo Yesu akashutumiwa kuwa ni mlafi na mnywaji, lakini pamoja na mambo yote haya anainua macho yake kumtukuza Mwenyezi Mungu. Mwanzoni mwa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu anasema, Baba Mtakatifu, Mababa wa Sinodi wanahitaji jicho la Kristo Yesu linalobariki na kupokea kwa ukarimu na wala si jicho linalosheheni majanga ya maisha ya mwanadamu, sera na mikakati ya kisiasa au mapambano ya kiitikadi. Sinodi si bunge linalotaka kufanya mabadiliko.

Kanisa linalotoa kièaumbele cha pekee kwa uwepo angavu wa Mungu
Kanisa linalotoa kièaumbele cha pekee kwa uwepo angavu wa Mungu

Mwono wa Kristo, ni chemchemi ya baraka unaendelea kuwa na utulivu, licha ya changamoto alizopambana nazo katika maisha na utume wake, mwaliko kwa Kanisa linalotafakari matendo makuu ya Mungu ili kupata mang’amuzi mapya na kuendelea kujikita zaidi katika amana ya utajiri wa ukweli wa Kanisa uliopokelewa tangu zamani za kale na hivyo kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kuangalia njia mpya za kuishi. Mama Kanisa anaalikwa kukabiliana na changamoto na matatizo katika ulimwengu mamboleo likiwa limeungana, kwa kukuza na kudumisha ushirika unaosimikwa katika unyenyekevu, ili kutoa baraka na kusujudi, kwa kumtambua Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi na kwamba, Kanisa lione fahari kwa Msalaba wa Kristo Yesu, ili hatimaye, kufikia faraja ya Kiinjili tayari kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kujikita katika ukimya, kama lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ili kuliwezesha Kanisa kumwangalia mwanadamu kwa jicho la huruma; Kanisa ambalo linasimikwa katika umoja, udugu; Kanisa linalosikiliza na kujadiliana; Kanisa linalo bariki na kutia moyo; Kanisa linalowasaidia wale wote wanaomtafuta Mwenyezi Mungu; Kanisa linalojali watu na kuwaelekeza katika uzuri wa imani. Hili ni Kanisa ambalo linatoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu. Huu ndio utashi wa Kristo Yesu kwa Kanisa na mchumba wake. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linapaswa kuwa na jicho la ukarimu ili kuweza kukabiliana na matatizo na changamoto mamboleo zinazojitokeza katika tamaduni na shughuli za kichungaji. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni hija ya watu wa Mungu, ili kujenga na kukuza umoja na urafiki, ili kujenga Kanisa linalojadiliana, tayari kuwakaribisha wote wasumbukao na wenye kuelemewa na mizigo, watu waliopoteza mwelekeo, wale wanaohisi kwamba, wako mbali na hivyo kushindwa kuona tena lango la matumaini, Kanisa liko kwa ajili yao!

Makardinali wapya waliotangazwa tarehe 30 Septemba 2023
Makardinali wapya waliotangazwa tarehe 30 Septemba 2023

Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu licha ya matatizo na changamoto mamboleo, kuepukana na kishawishi cha kutumbukia na hivyo kuwa ni Kanisa lenye “shingo ngumu” linalojizatiti dhidi ya ulimwengu, na kutazama nyuma; kishawishi cha kuwa ni Kanisa vuguvugu, linalojisalimisha kwa mitindo ya ulimwengu; Kanisa lililochoka na linalojitafuta lenyewe. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wa Mungu kutembea kwa pamoja, katika hali ya unyenyekevu, imara na wenye furaha, huku wakifuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, fukara na mpenda amani, aliyebahatika kuwa na Madonda Matakatifu ya Yesu, ili kujivika Kristo aliacha yote, akajisadaka kwa ajili ya kukarabati Kanisa la Kristo. Sinodi inawakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mama Kanisa anahitaji kutakaswa, kukarabatiwa, kwani watu wote ni wadhambi waliosamehewa dhambi zao, kumbe kuna haja ya kurejea daima kwenye kisima ambacho ni Kristo Yesu ili aweze kuwaelekeza katika njia ya Roho Mtakatifu ili kuwafikia watu wote kwa njia ya Injili. Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, alijizatiti zaidi katika kujenga na kudumisha umoja, majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kutumia silaha za Injii yaani: unyenyekevu na umoja, sala na upendo, changamoto kwa watu wa Mungu kumwilisha tunu hizi katika vipaumbele vya maisha yao. Huu ni mwaliko wa kuendelea kumwilisha matumaini licha ya wasiwasi, lakini ikumbukwe kwamba, Maadhimisho ya Sinodi ni Mwaliko wa Roho Mtakatifu, mahali pa neema na ushirika, ili kuweza kulipyaisha Kanisa la Kristo. Huu ni wakati wa kujiweka wazi kwa Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wa Mungu waambatane na Roho Mtakatifu katika imani na furaha!

Misa ya Sinodi ya Maaskofu
04 October 2023, 14:26