Tafuta

Kazi ya uinjilishaji inatajirisha akili na moyo; inafungua upeo wa kiroho, inawafanya waamini kuwa wepesi kuutambua utendaji wa Roho Mtakatifu. Kazi ya uinjilishaji inatajirisha akili na moyo; inafungua upeo wa kiroho, inawafanya waamini kuwa wepesi kuutambua utendaji wa Roho Mtakatifu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu: Kutangaza na Kushuhudia Injili ya Kristo

Maadhimisho ya Sinodi yanaendelea kujikita katika dhana ya waamini kukutana na hivyo kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kutembea katika umoja. Mababa wa Sinodi wamegusia pia kinzani na upinzani unaoendelea kujitokeza katika Makanisa mahalia, mwaliko wa kufanya mang’amuzi ya pamoja. Ni mwaliko kwa Mama Kanisa kujimanua kutoka katika malimwengu ili kujivika Kristo Yesu na Injili yake, tayari kulikarabati Kanisa la Kristo

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Ufunguzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu aligusia changamoto alizokabiliana nazo Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akainua macho yake mbinguni na kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa hekima na akili anayeona mema yaliyofichika, yanayokuwa, mbegu ya Neno la Mungu linalopokelewa kwa moyo mnyoofu, mwanga wa Ufalme wa Mungu unaoendelea kung’ara hata katikati ya usiku wa giza. Kumbe, mwono wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, ni jicho linalopokea changamoto na mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi
Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi

Upendo wa Mungu unaganga na kuponya mapungufu na madhaifu ya binadamu na kwamba, huu ndio utume wa Kanisa linalopaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa upendo huu wa Mungu. Hatua ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliwahusisha watu wa Mungu katika hatua za awali na hivyo Kanisa limejifunza kutembea kwa pamoja katika umoja ili kujenga Kanisa la Kisinodi linalosikiliza kwa makini, huku wakiwa wameunga na Maaskofu wao chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha ushirika wa Kanisa, moja, takatifu, katoliki la mitume. Huu ni umoja na ushirika wa watu wa Mungu pamoja na viongozi wao wakuu, ushirika unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti, ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu, ili kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kumbe, Sinodi hii ni kielelezo cha umoja waamini, umoja wa Mama Kanisa na umoja wa kihierakia. LG 1. Huu ni umoja unaosimikwa katika tofauti msingi za: Miito, utume, hali ya maisha, amana na utajiri, karama na zawadi mbalimbali kutoka kwa Roho Mtakatifu. Sinodi hii ni chombo cha umoja na huduma kwa Kanisa na kwa ulimwengu katika ujumla wake! Kuna watu wameingia kwenye Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wakiwa na ajenda ya Mama Kanisa kutoa ruhusa kwa wanawake kupewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Maadhimisho ya Sinodi katika Makundi madogo madogo
Maadhimisho ya Sinodi katika Makundi madogo madogo

Ni wajibu na dhamana ya Maaskofu kuzungumza ukweli na uwazi, vinginevyo watatoa mwanya kwa watu wa nje kuzungumza wanavyotaka. Baba Mtakatifu anawasihi wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutekeleza dhamana na utume wao kwa ufanisi na kwa haki, kwa kutambua kwamba, kusikiliza ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu ansema kwamba, sasa Kanisa “limesimama dede” kama ilivyokuwa Siku ya Ijumaa Kuu na Jumamosi kuu, si kwa woga, bali kwa kujikita katika mchakato wa kusikiliza kwa makini. Huu ndio ujumbe mahususi kwa wakati huu wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Tofauti msingi kati ya Mababa wa Sinodi zinapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kujifunza sarufi ya dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamefafanuliwa kuhusu: Hati ya Kutendea Kazi: “Instrumentum laboris” inayogusia kuhusu: Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Sifa za Kanisa la Kisinodi; Mwelekeo wa Maadhimisho ya Kanisa la Kisinodi: Majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi. Huu ni umoja unaong’ara, alama na chombo cha ushirika na Mwenyezi Mungu na alama ya umoja kati ya binadamu. Uwajibikaji katika utume na jinsi ya kushirikishana karama katika huduma ya Injili. Ushiriki, utawala na madaraja: Je, ni mchakato, miundombinu na taasisi gani zinapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi?

Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Itakumbukwa kwamba, Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka katika: Majimbo, Mabaraza ya Maaskofu na katika maadhimisho ngazi ya Kimabara, sanjari na maadhimisho yaliyokuwa yakiendeshwa kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo kubainisha vipaumbele vya Makanisa mahalia vinavyofanyiwa kazi sasa katika Maadhimisho ya Sinodi. Lengo kuu ni kutekeleza utume wa Mama Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni muda wa kusikiliza kwa makini jinsi ambavyo limeishi na kutekeleza dhamana na utume wake; matatizo na changamoto zinazojitokeza. Changamoto kubwa katika maadhimisho ya Sinodi ni uwezo wa kuratibu kinzani ili ziweze kuwa ni chemchemi ya nguvu mpya ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni wakati ambapo utambulisho na wito wa Kanisa unajikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuhakikisha kwamba, matunda yaliyojitokeza yanamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Jumuiya za waamini sehemu mbalimbali za dunia. Tafakari ya Neno la Mungu na Ukimya unaosimikwa katika sala ni muhimu katika ushirikishaji wa maoni kutoka kwa Mababa wa Sinodi. Maadhimisho haya yanaendelea katika makundi madogo madogo kadiri ya lugha, yanayojulikana kama “Circoli minori” ili kujenga utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana ili kwa pamoja waweze kumsikiliza Roho Mtakatifu. Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anasema, Maadhimisho ya Sinodi yanakazia umuhimu wa kufanya mang’amuzi ya pamoja katika ukimya, kwa kusikilizana, katika imani, ushirika na katika maisha ya sala. Katika maadhimisho ya Sinodi, kinzani na tofauti za mawazo zinaendelea kujitokeza.

Kipaumbele cha kwanza ni kwa Kristo Yesu chemchemi ya upendo kamili
Kipaumbele cha kwanza ni kwa Kristo Yesu chemchemi ya upendo kamili

Mambo ambayo yamepatiwa kipaumbele hadi wakati huu ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Maadhimisho ya Liturujia mintarafu wito, karama na huduma za watu wa Mungu; Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umisionari kwa kukazia dhana ya ushirika na umoja. Utume wa Kanisa ni uchu kwa ajili ya Kristo Yesu na uchu kwa ajili ya watu wake kwa wakati mmoja na kwamba, huu ndio utamu wa kiroho wa kuwa Taifa la Mungu, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaogusa shida, mahangaiko na matumaini ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Yote haya yatendeke kwa heshima, upole na amani; unyenyekevu na kuendelea kujikita katika kutenda mema. Kwa kufanya hivyo furaha ya kimisionari ya kushirikishana maisha pamoja na watu waamini wa Mungu itajidhihirisha, pale waamini wanapojitahidi kuwasha moto wa upendo katika nyoyo za walimwengu. Kazi ya uinjilishaji inatajirisha akili na moyo; inafungua upeo wa kiroho, inawafanya waamini kuwa wepesi kuutambua utendaji wa Roho Mtakatifu. Huu ni utume wa kuleta mwanga, baraka, unaohuisha, unaofufua, unaoponya na kuwaweka huru watu wa Mungu. Kila mtu ni mtakatifu sana na anastahili upendo wa Mama Kanisa. Rej. Evangelii gaudium 268-274. Maadhimisho ya Sinodi yanaendelea kujikita katika dhana ya waamini kukutana na hivyo kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kutembea katika umoja. Mababa wa Sinodi wamegusia pia kinzani na upinzani unaoendelea kujitokeza katika Makanisa mahalia, mwaliko wa kufanya mang’amuzi ya pamoja. Ni mwaliko kwa Mama Kanisa kujimanua kutoka katika malimwengu ili kujivika Kristo Yesu na Injili yake, tayari kulikarabati Kanisa la Kristo Yesu, kama alivyofanya Mtakatifu Francisko wa Assisi. Ni wakati wa kufanya mageuzi ya kweli katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutoa kipambele cha kwanza kwa Kristo Yesu, ili awe kweli ni chemchemi upendo unaojikita katika medani mbalimbali za maisha!

Sinodi ya Maaskofu
09 October 2023, 13:22