Tafuta

Roho Mtakatifu ndiye mjenzi wa Kanisa la Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kutoa kipaumbele cha pekee katika kumsikiliza. Roho Mtakatifu ndiye mjenzi wa Kanisa la Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kutoa kipaumbele cha pekee katika kumsikiliza.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Roho Mtakatifu, Usikivu na Umakini wa Habari

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 4 Oktoba 2023 jioni alipata fursa ya kutoa hotuba kwa Mababa wa Sinodi, akielezea historia ya Sinodi ya Maaskofu kwa Kanisa Katoliki, hija inayotekelezwa na Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa uinjilishaji, mjenzi wa umoja, ushirika na faraja kwa Kanisa; Roho Mtakatifu ndiye mjenzi wa Kanisa la Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kutoa kipaumbele cha pekee katika kumsikiliza katika kufunga na ukimya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhana ya Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Tangu wakati huo, miaka 60 imekwisha gota, Kanisa limekwisha adhimisha Sinodi kadhaa ambazo zimejadili tema mbalimbali mintarafu maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyofunguliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2023 hadi tarehe 29 Oktoba 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Mtakatifu Paulo VI ndiye Muasisi wa Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki
Mtakatifu Paulo VI ndiye Muasisi wa Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki

Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 4 Oktoba 2023 jioni alipata fursa ya kutoa hotuba kwa Mababa wa Sinodi, akielezea historia ya Sinodi ya Maaskofu kwa Kanisa Katoliki, hija inayotekelezwa na Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa uinjilishaji, mjenzi wa umoja, ushirika na faraja kwa Kanisa; Roho Mtakatifu ndiye mjenzi wa Kanisa la Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kutoa kipaumbele cha pekee katika kumsikiliza. Baba Mtakatifu anawasihi wadau wa tasnia ya habari kuwajulisha watu wa Mungu umuhimu wa kumsikiliza Roho Mtakatifu, kazi ambayo wanapaswa kuifanya vyema na kwa haki; kusikiliza ni kipaumbele cha Mama Kanisa katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu.

Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo
Sinodi ni wakati muafaka wa ujenzi wa ukimya na udugu wa Kikristo

Baba Mtakatifu anasema, tangu Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, azindue maadhimisho haya, imekwisha gota miaka 60 yenye mabadiliko makubwa, kiasi cha kutoa uhuru kwa Mababa wa Sinodi kupigia kura tema zinazojadiliwa na wakati wa maadhimisho ya Sinodi. Utafiti uliofanywa mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yaliyoongozwa na kauli mbiu ni: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ikolojia fungamani unaonesha upendeleo wa Maaskofu katika dhana ya Sinodi. Huu ulikuwa ni muda wa toba na wongofu wa ndani; ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani, umoja na udugu wa kibinadamu; upendo na mshikamano wa dhati, ili wote waweze kupata utimilifu wa maisha. Maaskofu walivutiwa sana na dhana ya Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, wengine walitamani Kanisa liadhimishe Sinodi kuhusu maisha na wito wa Mapadre na tatu baadhi ya Maaskofu walipendekeza Kanisa lijikite katika kujadili masuala jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Sinodi si Bunge wala mkutano wa marafiki unaopania kupata suluhu ya matatizo na changamoto mamboleo, jambo la msingi ambalo watu wa Mungu wanapaswa kutilia maanani ni kwamba, Mhusika mkuu wa maadhimisho ya Sinodi ni Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kumwachia nafasi katika majadiliano yao.

Maadhimisho ya Sinodi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria
Maadhimisho ya Sinodi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria

Roho Mtakatifu ni mdau mkuu katika maisha na utume wa Kanisa, ndiye anayelisongesha Kanisa mbele! Rej. Mdo 19:1-2. Ujio wa Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste ya kwanza, wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Rej Mdo 2:13. Lugha iliyosikika ni lugha ya upendo, umoja na ushirika na ndiye anayetekeleza historia ya wokovu, ili kujenga ushirika unaofumbatwa katika utofauti wa karama, miito na maisha ya watu wa Mungu. Roho Mtakatifu ni mfariji kama inavyoshuhudiwa kwenye Injili ya Msamaria mwema. Rej. Lk 10:34-35. Roho Mtakatifu analiwezesha Kanisa kutenda wema, licha ya mapungufu na madhambi yanayomwandama mwanadamu. Roho Mtakatifu ndiye anayelilinda, kulitegemeza na kulitunza Kanisa; ndiye Mhusika mkuu anayelijenga na kulidumisha Kanisa katika maisha na utume wake. Kumbe kwa wale waliobatizwa wanahimizwa kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo katika umoja na “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu.” Rej. Ef 4:30. Umbeya na majungu ni kati ya mambo yanayomhuzunisha Roho Mtakatifu, na kama Mababa wa Sinodi hawataondokana na “ndago” hizi, kwa hakika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, yatakuwa ni shughuli pevu! Mababa wa Sinodi waongozwe na kanuni ya kuzungumza katika ukweli na uwazi, ili waweze kuimarishana katika imani. Maadhimisho ya Sinodi ni kuliwezesha Kanisa kutembea katika umoja na ushirika. Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum laboris” ni matunda ya ushirikiano na mshikamano chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aliongoze Kanisa.

Sinodi na ujenzi wa urika wa Maaskofu ili kumsikiliza Roho Mtakatifu
Sinodi na ujenzi wa urika wa Maaskofu ili kumsikiliza Roho Mtakatifu

Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Baba Mtakatifu anakaza kusema, kusikiliza ni sehemu muhimu sana ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu. Na hii ni sehemu muhimu pia kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano. Baba Mtakatifu anawasihi waandishi wa habari kuwasaidia watu wa Mungu kuelewa dhana ya kusikiliza katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kazi na utume wa waandishi wa habari ni muhimu sana. Maadhimisho ya Sinodi, yamekuwa yakikabiliana na changamoto mbalimbali, kwa mfano anasema Baba Mtakatifu Francisko maadhimisho ya Sinodi ya Familia, watu waliingia kwenye Maadhimisho haya wakiwa na “ajenda za mitaani” kwamba, ilikuwa ni fursa kwa waamini walioachika wakaoa au kuolewa kuruhusiwa kupokea Ekaristi Takatifu. Wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, watu wakaibuka na dhana ya “Mapadre walioa.”

Kusikiliza; ukimya na Umaskini wa Vyombo vya Mawasiliano ni muhimu sana
Kusikiliza; ukimya na Umaskini wa Vyombo vya Mawasiliano ni muhimu sana

Kuna watu wameingia kwenye Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wakiwa na ajenda ya Mama Kanisa kutoa ruhusa kwa wanawake kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni wajibu na dhamana ya Maaskofu kuzungumza ukweli na uwazi, vinginevyo watatoa mwanya kwa watu wa nje kuzungumza wanavyotaka. Baba Mtakatifu anawasihi wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutekeleza dhamana na utume wao kwa ufanisi na kwa haki, kwa kutambua kwamba, kusikiliza ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kusema kwamba, sasa Kanisa “limesimama dede” kama ilivyokuwa Siku ya Ijumaa Kuu na Jumamosi kuu, si kwa woga, bali kwa kujikita katika mchakato wa kusikiliza kwa makini. Huu ndio ujumbe mahususi kwa wakati huu wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu.

Papa Hotuba Sinodi
05 October 2023, 14:52