Tafuta

Katekesi: Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume: Mt. Charles De Foucauld: Upendo

Papa Francisko: Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume: Ushuhuda wa Mtakatifu Shauku ya Uinjilishaji: Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., kuwa ni shuhuda aliyeamsha shauku ya uinjilishaji, kiasi cha kuwawezesha maskini kujenga udugu na Kristo Yesu na kwamba, kutokana na mang’amuzi na uzoefu wake na Mwenyezi Mungu akatekeleza safari ya mageuzi ya ndani kiasi cha kujisikia kuwa ni ndugu wa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema inayoongoza Mzunguko Mpya wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, Jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko huu wa katekesi ni kutaka kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu wa Katekesi, Baba Mtakatifu anasema, atajitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo.

Shauku ya uinjilishaji, bidii ya kitume ya mwamini.
Shauku ya uinjilishaji, bidii ya kitume ya mwamini.

Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., alizaliwa tarehe 15 Septemba 1858 huko mjini Strasbourg, Kaskazini Mashariki mwa Ufaransa. Aliuwawa kikatili tarehe 1 Desemba 1916. Tarehe 13 Novemba 2005, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Na tarehe 15 Mei 2022 Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa ni Mtakatifu na Mama Kanisa anamwadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 1 Desemba, siku ile aliyozaliwa mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Oktoba 2023 amemwelezea Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., kuwa ni shuhuda aliyeamsha shauku ya uinjilishaji, kiasi cha kuwawezesha maskini kujenga udugu na Kristo Yesu na kwamba, kutokana na mang’amuzi na uzoefu wake na Mwenyezi Mungu akatekeleza safari ya mageuzi ya ndani kiasi cha kujisikia kuwa ni ndugu wa watu wote. Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., alihangaika sana katika ujana wake, kiasi cha kuwa mbali na Mwenyezi Mungu katika maisha yake, akazama katika anasa, lakini siku moja akaonja toba na wongofu wa ndani wakati akiwa kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani kwenye Kiti cha Maungamano, akauachilia moyo wake kwa Kristo Yesu wa Nazareti na hii ikawa ni hatua yake ya kwanza katika mchakato wa uinjilishaji, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu katika akili na moyo wake, kiasi cha kumshuhudia katika maisha. Huu ni ushuhuda unaofumbatwa katika Kristo Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wake wa daima. Alivutwa na kujitahidi kumwiga Kristo Yesu katika maisha yake, kiasi cha kutembelea Nchi Takatifu ili kufuata nyayo za Kristo Yesu na hasa zaidi mjini Nazareti, ambako alifundwa chini ya shule ya Kristo Yesu, kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, kiasi cha kupata shauku ya kumtangaza na kumshuhudia, katika ukimya na kwa njia ya mifano hai ya maisha kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria alipomtembelea binamu yake Elizabeti, kwa sababu kwa mwamini kuishi ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Injili

Ni katika muktadha huu, Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., aliamua “kujichimbia” katika Jangwa na Sahara ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu katika hali ya ukimya, ili kukoleza pia majadiliano ya kidini, huku akijipambanua mwenyewe kuwa rafiki na ndugu, akiwa amebeba ndani mwake upole wa Yesu wa Ekaristi Takatifu kwani aliamini kwamba, maisha ya Kiekaristi ni chombo cha uinjilishaji na kwamba, Kristo Yesu ndiye Mwinjilishaji wa kwanza. Aliweza kushuhudia maisha haya ya sala kwa kusimama mbele ya Tabernakulo kwa muda mrefu sana, kwa kutambua kwamba, ni kwa njia ya Yesu wa Ekaristi Takatifu ndiye chemchemi ya nguvu za uinjilishaji na hivyo Kristo Yesu kumwezesha kuwafikia watu wa mbali na wale wa karibu. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwauliza waamini ikiwa kama wana imani katika nguvu ya Ekaristi Takatifu na ikiwa kama waamini wanathubutu kwanza kujichotea nguvu kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kabla ya kutoa huduma kwa jirani zao. Huu ni mwaliko kwa waamini kuanza na kuhitimisha siku kwa Ibada ya Misa Takatifu. Ikumbukwe kwamba, kila Mkristo ni mtume na kwamba, waamini walei ni wadau wakuu katika mchakato wa uinjilishaji kwani hawa ni msaada mkubwa wa kuona yale ambayo Padre anashindwa kuyaona na hivyo wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji kwa jirani zao kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya upendo na wema, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza, mkazo unaotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Waamini wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Waamini wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Dhamana na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa namna ya pekee, ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaobainisha: wito, utume na dhamana ya waamini walei katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Waamini walei ni wadau pia katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., ni kielelezo cha mchakato mpya unaowashirikisha waamini; mchakato unaowakutanisha na kuwajengea utamaduni wa kusikilizana na kujadiliana; kushirikiana na kuaminiana, daima wakiwa wameungana na Kanisa pamoja na wachungaji wao. Mtakatifu Charles Eugène de Foucauld de Pontbriand, PFJ., ni Nabii katika ulimwengu mamboleo katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya utume wa upole. Alijisikia kuwa ni “ndugu wa walimwengu wote” na kumkaribisha kila kila mtu, kielelezo cha nguvu ya uinjilishaji inayojikita katika upole. Itakumbukwa kwamba, mtindo wa Mungu unasimikwa katika maneno makuu matatu: Ukaribu, Huruma na Upole na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Ukristo. Kuishi wema wa Yesu kulimfanya atengeneze uhusiano wa kindugu na urafiki na maskini, na Watuareg, na wale walio mbali zaidi na mawazo yake. Kidogo kidogo vifungo hivi vilizalisha udugu, ushirikishwaji na utukufu wa utamaduni wa kila mmoja. Wema wake ukakutana na watu kwa urahisi kiasi cha kuwashirikisha tabasamu la kukata na shoka. Hakuna uinjilishaji wa shuruti, bali uinjilishaji wa kina unafumbatwa katika katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, na kwa njia ya ucheshi na upendo. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa kweli ni vyombo vya furaha, upole, huruma na ukaribu wa Kikristo kwa watu wa Mataifa.

Ushuhuda wa Injili
18 October 2023, 15:52

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >