Tafuta

Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Utoto Mtakatifu, chombo cha uinjilishaji kati ya watoto. Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Utoto Mtakatifu, chombo cha uinjilishaji kati ya watoto. 

Jubilei ya Miaka 180 ya Shirika la Utoto Mtakatifu: Watoto na Uinjilishaji wa Kina!

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Utoto Mtakatifu, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake, huku akikazia umuhimu wa waamini kujikita katika wokovu wa watu wote na kuendelea kuwafunda watoto na vijana ili wawe kweli ni mitume wamisionari. Mwaka 2023 Kanisa linaadhimisha pia Jubilei ya Miaka 150 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, changamoto kwa waamini kuwa ni mashuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Utoto Mtakatifu, lilianzishwa ili kujibu changamoto na hivyo kutoa mwaliko kwa wazazi na walezi kuwajengea watoto wao ari na moyo wa kimisionari ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, watoto yatima; watoto wanaokumbana na magonjwa, baa la njaa, ujinga na umaskini. Hata katika umaskini wao, watoto bado wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia! Kristo Yesu, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watoto katika maisha na utume wake. Watoto wanapaswa kujifunza na kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano, kwa kujaliana, kusaidiana na kusali pamoja; mambo msingi katika malezi na makuzi yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Mshikamano wa upendo, umewawezesha watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao kiasi cha kujinyima na kuchangia kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao! Leo hii, haki msingi za watoto sehemu mbali mbali za dunia zinaendelea kuvunjwa, kiasi kwamba, watoto wananyanyaswa na kudhulumiwa; wanapokwa haki yao ya utoto kwa kufanyishwa kazi za suluba; kwa kusumbuliwa na: umaskini, magonjwa, ujinga, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; kwa vita na majanga mbalimbali yanayoendelea kumwandama mwanadamu! Watoto hata katika changamoto zote hizi, bado wanaweza kusaidiwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari, kwa kujenga utamaduni wa: huruma, upendo na mshikamano. Kwa njia hii watoto wamesaidia kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuwapatia watoto wenzao mahitaji msingi kama vile: chakula, elimu, makazi na huduma bora ya afya.

Watoto ni mitume wamisionari, wajenzi wa amani
Watoto ni mitume wamisionari, wajenzi wa amani

Shirika la Utoto Mtakatifu lililoanzishwa kunako mwaka 1843 na Askofu Charles Toussaint de Frobin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy. Mwaka huu wa 2023, Shirika la Utoto Mtakatifu linaadhimisha Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwake. Askofu Charles de Frobin Janson kwa njia ya barua kutoka China, alitambua kwamba, kuna watoto wengi waliokuwa wanapoteza maisha yao kutokana na kukumbwa na baa la njaa pamoja na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi na huo ukawa mwanzo wa Shirika la Utoto Mtakatifu, ili kuhakikisha kwamba, watu wote wanapata wokovu kiroho na kimwili kwa sababu Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kuwakomboa watu wote! Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 180 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Utoto Mtakatifu, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake, huku akikazia umuhimu wa waamini kujikita katika wokovu wa watu wote na kuendelea kuwafunda watoto na vijana ili wawe kweli ni mitume wamisionari. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali ili Wakristo wote wajifunge kibwebe kushiriki katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wawe ni mashuhuda wa maisha yenye ladha ya tunu msingi za Kiinjili.

Watoto ni mitume wamisionari miongoni mwa watoto wenzao
Watoto ni mitume wamisionari miongoni mwa watoto wenzao

Kila mwaka ifikapo tarehe Mosi Mwezi Oktoba, Mama Kanisa humwadhimisha Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu kwa heshima ya Bikira na Mwalimu wa Kanisa na tangu mwaka 1927 aliteuliwa kuwa ni msimamizi wa wamisionari wote duniani pamoja na Mtakatifu Francisko Xsaveri. Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba linapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika kuombea shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwamko na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 huko Alencon na baadae kuhamia Lisieux nchini Ufaransa.  Theresa ni mtoto wa tisa kuzaliwa na kitinda mimba kwenye familia ya Mzee Luigi Martin na Zeria Guerin ambao sasa Kanisa limewaweka kuwa mfano na kioo kwa familia zote za Kikristo. Tarehe 19 Oktoba 2008 walitangazwa kuwa ni Wenyeheri na mwaka 2015 Kanisa limewatangaza kuwa watakatifu kwa kuzingatia walivyoishi na kuwalea watoto kiimani na katika maadili ya kikiristo. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu aliaga dunia tarehe 30 Septemba 1897, akatangazwa Mtakatifu mwaka 1925, na kunako mwaka 1927 Papa Pius XI akamtangaza kuwa ni msimamizi wa utume wa Kanisa.

Jubilei ya miaka 180 ya Shirika la Utot Mtakatifu
Jubilei ya miaka 180 ya Shirika la Utot Mtakatifu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwaka 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Ujumbe mahususi ni kwamba, kwa njia ya sala za waamini, hata kama ni kidogo kiasi gani zinaweza kusaidia kuchangia katika mchakato wa kumfanya Kristo Yesu afahamike na kupendwa, na katika hali ya ukimya, kuwasaidia wengine waweze kutenda mema. Sala ni tendo la kwanza la kimisionari linaloweza kutekelezwa na kila mtoto na kila mmisionari sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na hasa zaidi watoto kujenga mahusiano na mafungamano ya urafiki na Kristo Yesu, ili kweli watoto wamisionari waweze kuwa ni wajenzi wa amani. Baba Mtakatifu katika kumbukizi zote hizi, anapenda kuwashukuru na kuwapongeza Watoto wa Utoto Mtakatifu, ambao wamewawezesha waamini kuwa ni mashuhuda jasiri wa Injili, kwa kushirikishana kwa ukarimu na jirani ile amana na utajiri wa imani. Baba Mtakatifu anawashukuru wazazi na walezi wanaoendelea kupandikiza karama ya Utoto Mtakatifu na hivyo kuwawezesha kuwa ni washirika wake wa karibu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu anawataka Watoto wa Utoto Mtakatifu kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu. Baba Mtakatifu anawaalika watoto wamisionari kuendelea kujikita katika karama ya Askofu Charles Toussaint de Frobin Janson wa Jimbo Katoliki la Nancy sanjari na njia ndogo ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, daima kwa kuendelea kujikita katika kauli mbiu “Watoto wanasali kwa ajili ya watoto wenzano na wanawainjilisha watoto wenzao; watoto wanawasaidia watoto wenzao.” Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume ili ziwasindikize watoto wote katika maisha yao na kamwe wasisahau pia kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Utoto Mtakatifu
01 October 2023, 15:01