Tafuta

Wajumbe 800 wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat kutoka Hispania, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangua kuanzishwa kwao. Wajumbe 800 wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat kutoka Hispania, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangua kuanzishwa kwao.  (Vatican Media)

Bikira Maria wa Rozari Takatifu: Urafiki wa Kijamii na Udugu wa Kiulimwengu

Papa amewapongeza wajumbe wote kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Udugu wao, Siku ambayo Kanisa linaadhimisha pia Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ucha Mungu maarufu, urafiki wa kijamii na udugu wa ulimwengu wote", lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, haki na amani vinang’ara na kushamiri. Amewashukuru wajumbe hawa kumtembelea wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu sanjari na Upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani wenye shida. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu! Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, tarehe 7 Oktoba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Kwa namna ya pekee anapenda kutoa mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi hiki cha Mwezi wa Oktoba, kujibidiisha kusali Rozari Takatifu, huku wakimwachia nafasi Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza kwenda kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu! Mwaka 1573 Baba Mtakatifu Gregory XIII alitangaza Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu iadhimishwe tarehe 7 Oktoba. Na kunako mwaka 1884 Baba Mtakatifu Leo XIII alitangaza rasmi kwamba mwezi wote wa kumi utakuwa mwezi wa kusali Rozari Takatifu akiwa na kumbukumbu ya ushindi ambao Wakristo waliupata dhidi ya Waislam katika vita vya Lepanto tarehe 7 Oktoba 1571. Lengo kubwa la kutangaza mwezi Oktoba kuwa mwezi wa Rozari lilikuwa kumheshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria ambaye kwa maombezi yake Wakristo walipata ushindi tarehe 7 Oktoba 1571. Wajumbe 800 wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat kutoka Hispania, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat, kuanzia Jumamosi tarehe 7 Oktoba hadi 9 Oktoba 2023 wanafanya hija ya maisha ya kiroho mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Wajumbe wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat
Wajumbe wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat

Hii ni hija muhimu sana kuwahi kufanywa na wajumbe wa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat mjini Roma tangu mwaka 1950. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa wajumbe hawa, Jumamosi tarehe 7 Oktoba 2023, amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Udugu wao, Siku ambayo Kanisa linaadhimisha pia Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ucha Mungu maarufu, urafiki wa kijamii na udugu wa ulimwengu wote", lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, haki na amani vinang’ara na kushamiri. Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe hawa kumtembelea wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kielelezo cha ukaribu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ambao kamwe hawaachi pweke, kwani amemtoa Mama wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu aweze kuwalinda na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao. Bikira Maria amekuwa ni mwenza wa safari ya maisha yao ya kiroho katika kipindi chote cha miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat, Bikira Maria Malkia na Mama wa kazi nzima ya uumbaji. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na wa Kanisa, ambaye anaheshimika sana na kwamba, katika kipindi cha miaka 800 kuna waamini waliokimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa kusali na kutafakari ya Rozari Takatifu; kwa kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Montserrat pamoja na kumshukuru Bikira Maria, kwa kutenda kile ambacho Kristo Yesu amewaamuru kutenda. Rej. Yn 2:5.

Jubilei ya Miaka 800 ya Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat
Jubilei ya Miaka 800 ya Udugu wa Mama wa Mungu wa Monserrat

Baba Mtakatifu Francisko anasema nguvu ya kuinjilisha ya matendo ya kiibada ya waamini wengi ni njia muafaka inayojenga na kudumisha vifungo vya urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mungu na hivyo kukua na kuimarishana, kama sehemu ya uinjilishaji. Matendo haya ya kiibada huwawezesha waamini kuona jinsi ambavyo imani ikishapokelewa, hujumuishwa katika utamaduni na daima kurithishwa na kwamba, hii ni nguvu ya kiimisionari na kielelezo cha maisha ya kitaalimungu yanayorutubishwa kwa kazi ya Roho Mtakatifu aliyemiminwa ndani ya roho zao Rej. Rum 5:5. Bikira Maria ni wakili mwaminifu anayeingilia kati na kuleta ufumbuzi wa kudumu kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria ni Mama anayewaelekeza waamini kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii kati ya watu wa Mataifa, ili waweze kumfuasa na kuonana na Uso wa Kristo Yesu, tayari kujikita katika njia ya amani, utu wema, usikivu na majadiliano yanayosimikwa katika uvumilifu na imani. Bikira Maria anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha ndani mwao udugu wa kibinadamu, tayari kujenga ulimwengu mpya unaowawezesha watu wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja, wanaoheshimiana na kuthaminiana; katika ulimwengu ambamo haki na amani vinang’ara na kushamiri. Bikira Maria: Nyota ya Uinjilishaji mpya na Mama wa uinjilishaji awashike mkono na kuwasaidia kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, utume na zawadi wanayopaswa kuitekeleza.

Bikira Maria
07 October 2023, 15:17