Tafuta

Ziara ya Papa Mongolia:kuendeleza umoja na maana ya utakatifu wa ardhi hiyo

Papa akiwa ndani ya Kanisa Kuu la Ulaanbaatar na Jumuiya ya kikanisa,amejikita kutazama mizizi ya Kikristo katika ardhi hiyo yenye hisia kali ya utakatifu.Licha ya kuwa Kanisa dogo ni la thamani na imani ya kweli inayohesabika.Papa amehimiza kuendeleza umoja na urahisi,kujitoa kwa huduma za afya,kukuza utamaduni na haadhi ya watu.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akikutana na Kanisa la Mongolia katika Kanisa Kuu la Watakatifu Petro na Paulo, Jumamosi tarehe 2 Septemba 2023, ameanza kusema kuwa:“Asante, Mheshimiwa, kwa maneno yako mazuri. Asante Sr. Salvia, Padre Peter Sanjaajav na Rufina kwa ushuhuda wenu. Asante, nyote, kwa uwepo wenu na imani yenu. Nina furaha kuwa nanyi nyote. Furaha ya Injili ndiyo imewatia moyo ninyi, mliowekwa wafu wanaume na wanawake katika maisha ya kitawa na katika huduma iliyowekwa wakfu, kuwa hapa na kujiweka wakfu, pamoja na dada na kaka zenu walei, kwa ajili ya huduma ya Bwana na ya wengine.” "Ninamshukuru Mungu kwa hili, nikitumia maneno ya sala nzuri ya sifa, Zaburi 34, ambayo ninayanukuu ili nishirikishe mawazo fulani nanyi. Zaburi inatualika:  “Kuonja na kuona ya kuwa Bwana ni mwema” (Za 34, 9). “Onjeni muone”, ni kwa sababu furaha na wema wa Bwana si wa haraka; zinabaki ndani yetu, zikitoa ladha kwa maisha yetu na kutufanya tuone mambo kwa njia mpya, kama alivyosema, Rufina, katika ushuhuda wake mzuri.”

Papa akibusu sanamu ya Bikira Maria
Papa akibusu sanamu ya Bikira Maria

Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amependa basi  , kuonja" ladha ya imani katika nchi hiyo kwa kukumbuka zaidi ya nyuso zote, historia na maisha yaliyotumiwa kwa ajili ya Injili. Kutoa maisha kwa ajili ya Injili. Hiyo ni njia nzuri ya kufafanua wito wa kimisionari wa Wakristo, na hasa jinsi wito huo unavyoishi na Wakristo  wa hapo.  Kwa njia hiyo ameanza kwa kumkumbuka Askofu Wenceslao Selga Padilla, aliyekuwa Msimaimizi wa Kitume wa kwanza, mwanzilishi wa historia ya kisasa ya Kanisa la Mongolia, aliyejenga Kanisa Kuu hilo. Hapo  hata hivyo, imani hairudi nyuma hadi miaka ya tisini ya karne iliyopita; ina mizizi ya kale. Matukio ya milenia ya kwanza na kazi ya uinjilishaji iliyofanywa na wamisionari wa mapokeo ya Kisiria kando ya Barabara ya Hariri ilifuatwa na mhubiri wa ajabu wa kimisionari.

Papa Francisko ahutubia Kanisa la Mongolia
Papa Francisko ahutubia Kanisa la Mongolia

Tunawezaje kushindwa kutaja utume wa kidiplomasia wa karne ya kumi na tatu, na utunzaji wa kitume uliodhihirishwa na uteuzi, karibu mwaka 1310, wa Yohana wa Montecorvino kama Askofu wa kwanza wa Khanbalik, akiwa na jukumu la eneo hilo kubwa la ulimwengu chini ya uongozi wa Yuan wa Kimongolia? Alitoa tafsiri ya kwanza ya Zaburi na Agano Jipya katika lugha ya Kimongolia. Historia hii kuu ya mapenzi kwa ajili ya Injili ilichukuliwa upya kwa namna ya ajabu, ambapo mnamo mwaka 1992 wamisionari wa kwanza wa Shirika la Moyo Safi wa Maria walijiunga na washiriki wa Taasisi nyingine, mapadre wa jimbo na walei wamisionari. Miongoni mwao wote, Papa alipenda  kubainisha nguvu na bidii ya Padre Stephen Kim Seong-hyeon. Tutambue pia, wale watumishi wengi waaminifu wa Injili nchini Mongolia ambao walikuwa hapo pamoja nao muda huo   na ambao, baada ya ku jitolea maisha yao kwa ajili ya Kristo, wanaweza “kuona” na “kuonja” maajabu ambayo wema wake unaendelea kutimiza ndani yao na kupitia wao, amewashukuru Papa.

Kwa nini mtu yeyote atoe maisha yake kwa ajili ya Injili? Hilo ni swali  ambalo Papa amependa kuuliza. Kama Rufina alivyosema, maisha ya Kikristo yanasonga mbele kwa kuuliza maswali, kama watoto ambao kila mara wanauliza mambo mapya, kwa sababu katika umri wao hawaelewi kila kitu. Maisha ya Kikristo hutuvuta karibu na Bwana na daima huuliza maswali, ili kwamba tumfahamu zaidi Bwana, kuelewa vizuri mafundisho yake. Kwa hiyo kutoa maisha kwa ajili ya Injili ni kwa sababu “unamuonja” Mungu aliyejifanya aonekane, anayeweza kuguswa na kukutana naye ndani ya Yesu. Ndiyo, Yesu ndiye habari njema, inayokusudiwa kwa watu wote, ujumbe ambao Kanisa linapaswa kutangaza daima, likiwa ndani ya maisha yake na “kunong’oneza” moyo wa kila mtu na tamaduni zote. Lugha ya Mungu mara nyingi sana ni kunong'ona polepole, ambayo huchukua muda wake; Mungu anazungumza kwa njia hiyo. Uzoefu wa upendo wa Mungu katika Kristo ni nuru safi inayoangaza na kubadilisha sura zetu. Baba Mtakatifu amesema, maisha ya Kikristo yanazaliwa kwa kuutafakari uso wa Bwana; inahusu upendo, kukutana na Bwana kila siku katika neno lake na katika Mkate wa Uzima, na katika nyuso za wengine, wahitaji na maskini ambao Yesu yumo ndani yao.

Kanisa la Mongolia limemkumbatia Papa
Kanisa la Mongolia limemkumbatia Papa

Papa aidha amesema kwamba Sr Salvia alikumbusha jambo hilo katika ushuhuda wake na hivyo amemshukuru. Yeye amekuwa hapo kwa zaidi ya miaka ishirini na amejifunza jinsi ya kuzungumza na watu hao. Katika miaka hii thelathini na moja ya uwepo nchini Mongolia, wao mapadre, watu waliowekwa wakfu na wachungaji, wamejiingiza katika mipango mbali mbali ya upendo ambayo inachukua nguvu zao nyingi na kuakisi uso wa huruma wa Kristo, yaani Msamaria Mwema. Hii, kwa njia fulani, ni kadi yao ya kupiga simu, na imewafanya waheshimiwe kwa manufaa mengi yanayotolewa kwa watu wengi katika nyanja mbalimbali: kuanzia usaidizi wa kijamii na elimu, huduma za afya na uhamasishaji  wa utamaduni. Kwa hiyo Papa Francisko amewahimiza kuendelea katika njia hiyo, ambayo imeonekana kuzaa matunda na ya manufaa kwa watu wapendwa wa Mongolia, kwa ishara za upendo na matendo ya upendo. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amewasihi waonje na kumwona Bwana, ili kuendelea kurudi kwenyemtazamo" huo wa asili ambao kila kitu kilianzia. Vinginevyo, amsema nguvu zetu zitashindwa na kazi yetu ya uchungaji itahatarisha kuwa tasa wa huduma, orodha ya majukumu ambayo mwishowe husababisha uchovu na kufadhaika. Lakini tunapobaki katika kuwasiliana na uso wa Kristo, tukimtafuta katika Maandiko na kumtafakari katika ibada ya kimya kimya mbele ya hema, tunakuja kumwona katika nyuso za wale tunaowahudumia na kupata furaha ya ndani ambayo, hata katikati ya magumu huleta amani mioyoni mwetu.

“Hiki ndicho tunachohitaji, leo na siku zote: si watu wanaokimbia huku na kule, wakiwa na shughuli nyingi na waliokengeushwa, wanaotekeleza miradi lakini pia nyakati fulani wanaoonekana kuchukizwa na maisha ambayo kwa hakika si rahisi. Badala yake, Mkristo ni yule anayeweza kuabudu, akiabudu kimya kimya. Na kisha, nje ya ibada hii ni chemchem ya shughuli.” Walakini, wasisahau kuabudu. Ka sababu amesema “Tumepoteza kwa kiasi fulani maana ya kuabudu katika karne hii na, kutenda. Tunahitaji kurudi kwenye chanzo, kwenye uso wa Yesu na kuonja uwepo wake, kwa kuwa yeye ni hazina yetu (rej. Mt 13:44), lulu ya thamani kubwa ambayo ni thamani yake kutumia kila kitu (taz. Mt 13:45-46). Baba Mtakatifu amewambia kaka na dada wa Kimongolia, ambao wana ufahamu mkubwa wa mambo matakatifu na kama ilivyo kawaida hapo Asia historia ya kale na changamano ya kidini, kutafuta ushuhuda wao na wanaweza kutambua kama ni wa kweli. Huu ni ushuhuda ambao lazima wa utoe, kwa sababu Injili haikui kwa kugeuza watu imani, Injili inakua kwa kutoa ushuhuda, Papa alibainisha.

Watawa wakitumbuiza wakati wa Mkutano katika Kanisa Kuu la Jiji la Mongolia
Watawa wakitumbuiza wakati wa Mkutano katika Kanisa Kuu la Jiji la Mongolia

Bwana Yesu, kwa kuwatuma wanafunzi wake ulimwenguni, hakuwatuma kueneza nadharia za kisiasa, bali kushuhudia  maisha yao upya wa uhusiano wake na Baba yake, ambaye sasa ni “Baba yetu” (taz. Yoh 20:17) na  ambaye ni chanzo cha udugu thabiti na kila mtu binafsi na watu. Kanisa lililozaliwa kutokana na mamlaka hayo ni Kanisa maskini, linalotegemezwa tu kwa imani ya kweli na kwa uwezo usio na silaha na wa kupokonya silaha kwa Bwana Mfufuka, na linaloweza kupunguza mateso ya wanadamu waliojeruhiwa. Kwa sababu hiyo, Serikali na Taasisi za kiulimwengu hazina chochote cha kuogopa kutokana na kazi ya Kanisa ya uinjilishaji, kwa kuwa Kanisa halina ajenda ya kisiasa ya kuendeleza, bali linategemezwa na nguvu tulivu ya neema ya Mungu na ujumbe wa huruma na ukweli unaokusudiwa kukuza wema wa wote. Ili kutekeleza utume huo, Kristo aliliunda Kanisa lake kwa namna ambayo inatukumbusha maelewano yaliyopo kati ya viungo mbalimbali vya mwili wa mwanadamu.  Kwa hiyo Papa ameeleza kuwa Yeye ndiye kichwa, ambaye anatuongoza daima, akimimina ndani ya mwili wake, yaani ndani yetu,  Roho wake, akifanya kazi zaidi ya yote katika ishara hizo za maisha mapya ambazo ni sakramenti. Ili kuhakikisha ukweli na ufanisi wa mwisho, alianzisha utaratibu wa makuhani, uliowekwa na ushirika wa karibu naye, Mchungaji Mwema ambaye hutoa maisha yake kwa ajili ya kundi. Kwa kumgeukia kuhani,  Padre Peter,  Baba Mtakatifu amesema aliitwa kwa utume huo na amemshukuru kwa kushirikisha uzoefu wake. Vivyo hivyo, hata Watu watakatifu wa Mungu huko Mongolia wana utimilifu wa karama za kiroho, amethibitisha.

Papa aliwasalimia mmoja mmoja katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na Paulo
Papa aliwasalimia mmoja mmoja katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na Paulo

Kwa mtazamo huo, Papa Francisko amewasihi waone katika askofu wao kuwa si hori bali picha hai ya Kristo Mchungaji Mwema, ambaye huwakusanya na kuwaongoza watu wake; mfuasi aliyejazwa na karama ya kitume ya kujenga udugu wao katika Kristo na kuutia mizizi kwa undani zaidi katika taifa hilo na urithi wao adhimu wa kiutamaduni. Ukweli, basi, kwamba Askofu wao na Kardinali ni ishara kubwa zaidi ya ukaribu. Wao wote ingawa wako mbali kimwili, lakini wako karibu sana na moyo wa Petro. Na kwa upande wake, Kanisa zima liko karibu na wao na jumuiya yao, ambayo ni ya Kikatoliki kweli, ya ulimwengu wote, na inaelekeza upendo wa kaka na dada zetu wote duniani kote kwa Mongolia, katika kumiminika kwa umoja  wa kikanisa. Papa Francisko amependa kusitizia juu ya neno hilo la umoja. Kanisa haliwezi kueleweka kwa maneno ya kiutendaji tu. Hapana, Kanisa sio biashara, halikui kwa kugeuza watu imani, kama alivyokwisha taja. Kanisa ni kitu kingine. Neno “umoja” linaeleza vizuri ni maana ya  Kanisa. Katika kundi hilo la Kanisa, askofu sio msimamizi wa vipengele vyake mbalimbali, hata pengine kwa kuzingatia kanuni ya wengi, bali anaongoza kwa msingi wa kanuni ya kiroho, ambayo kwayo Yesu mwenyewe anakuwapo katika nafsi ya Askofu kwa utaratibu ili kuhakikisha unaendelea umoja katika Mwili wake wa fumbo.

Kwa maneno mengine, Papa amefafanua kuwa umoja katika Kanisa sio juu ya utaratibu na heshima, wala sio mkakati mzuri wa kazi ya pamoja"; unahusu imani na upendo kwa Bwana, na juu ya uaminifu kwake. Kwa hiyo, ni muhimu kwa washiriki wote wa kikanisa kubaki na umoja thabiti karibu na Askofu, anayemwakilisha Kristo akiwa hai katikati ya Watu wake, na kujenga ushirika wa kisinodi tunaohubiri na ambao unasaidia sana kukuza imani. Papa akiendelea kueleza Wamisionari hao kuhusiana na neno, “onjeni muone” zawadi waliyo nayo, amesema ni ile ya  onjeni na muone uzuri wa kujitoa kabisa kwa Kristo aliyewaita kuwa mashuhuda wa upendo wake hapo Mongolia. Waendelee kufanya hivyo kwa kusitawisha umoja. Wafanye hivyo kupitia usahili wa maisha yasiyo na mali, kwa kumwiga Bwana, aliyeingia Yerusalemu akiwa amepanda mwanapunda na ambaye, msalabani, alivuliwa hata vazi lake. Daima wawe karibu na watu, kwa ukaribu huo ambao ni njia ya Mungu. Mungu yuko karibu, mwenye huruma na mpole.

Watawa wa Shirika la Mama Tereza wa Kalkuta wako mstari mbele katika utume nchini Mongolia
Watawa wa Shirika la Mama Tereza wa Kalkuta wako mstari mbele katika utume nchini Mongolia

Kwa hiyo Ukaribu, huruma na upole, ndivyo Papa amependa kukazia na kwamba  wawatendee watu hivyo, kwa kuwajali kibinafsi, kujifunza lugha yao, kuheshimu na kupenda utamaduni wao, bila kujiruhusu kujaribiwa na aina za usalama za ulimwengu huu, lakini kubaki thabiti katika Injili kupitia maisha ya kiadili na ya kiroho. Pia ushauri mwingine wa Papa ni kuwa rahisi na ukaribu! Kwa hiyo amewasihi wasichoke kumpelekea Yesu nyuso na hali wanazokutana nazo, matatizo na mahangaiko. Watenge wakati kwa sala ya kila siku, ambayo itawawezesha kudumu katika kazi ya utumishi na kupata faraja kutoka kwa “Mungu wa faraja yote” ( 2 Kor 1:3 ), na hivyo kuleta tumaini kwa mioyo ya wale wote wanaoteseka. Papa amesema kuwa ukaribu na Bwana hutuhakikishia kwamba, kama vile Zaburi 34 inavyotuambia, “wale wamchao hakosi kitu...; wale wamtafutao Bwana hawakosi kitu kizuri” (Zab 34, 9-10). Kwa hakika, makosa na matatizo ya maisha pia huwaathiri waamini, na waeneza-Injili ambao hawakoshwi na mzigo wa wasiwasi ambao ni sehemu ya hali yetu ya kibinadamu. Mtunga Zaburi hasiti kusema juu ya waovu na watenda mabaya, lakini anatukumbusha kwamba Bwana husikia kilio cha wanyenyekevu na huwaokoa na taabu zao zote, kwa kuwa yu karibu nao waliovunjika moyo, naye huwaokoa waliovunjika moyo”(Zab 34, 18-19). Kwa sababu hiyo, Kanisa linajionesha mbele ya walimwengu kama sauti ya mshikamano na wote walio maskini na wahitaji; linakataa kukaa kimya mbele ya dhuluma na linafanya kazi kwa utulivu ili kuhamasisha hadhi kwa kila mwanadamu.

Baba Mtakatifu amesema, katika safari yao kama wanafunzi wamisionari, wana usaidizi wa hakika kwa maana ya Mama yetu wa mbinguni, ambaye Papa amesema ahata yeye alifurahishwa  sana kugundua ambaye  alitaka kuwapatia ishara inayoonekana ya uwepo wake mpole na wa kujali kwa kuruhusu mfano wake kupatikana kwenye takataka. Katika mahali pa takataka, sanamu hiyo nzuri ya Mama Safi ilionekana. Yeye mwenyewe akiwa huru na asiyetiwa unajisi na dhambi, alitaka kujisogeza karibu na sisi hadi ashuke kwa tabia za jamii, ili kutoka kwenye uchafu wa mrundo la takataka usafi wa Mama mtakatifu wa Mungu, Mama yetu wa mbinguni, uweze kuangaza. Pia Baba Mtakatifu alieleza jinsi alivyojifunza kuhusu tamaduni nzuri ya Kimongolia ya suun dalai ijii, mama mwenye moyo mkubwa kama bahari ya maziwa. Kulingana na Historia ya Siri ya Wamongolia, mwanga kutoka kwenye sehemu ya juu ya geri ilimpatia mimba malkia wa ibada Alungoo; Kwa hiyo wao hata hivyo, wanaweza kutafakari katika umama wa Bikira Maria utendakazi wa nuru ya kimungu ambayo, kutoka juu, kila siku unasindikiza hatua za Kanisa lao.

Ziara ya Papa Nchini Mongolia
Ziara ya Papa Nchini Mongolia

Kwa njia hiyo Papa amesema wanapoinua macho yao kwa Maria, basi, wanaweza kupata burudisho, wakijua kwamba kuwa mdogo sio tatizo, bali ni rasilimali. Mungu anapenda udogo, na kupitia huo anapenda kutimiza mambo makuu, kama vile Maria mwenyewe anavyoshuhudia (rej. Lk 1:48-49). Papa amewaomba kwa hiyo wasiwe na wasiwasi juu ya idadi ndogo, mafanikio machache, au kutokuwa na umuhimu dhahiri. Hivyo sivyo ambavyo Mungu atenda  kazi. La muhimu ni kukazia mtazamo wao kwa Mama yetu Maria, ambaye katika udogo wake ni mkuu kuliko mbingu, kwa maana ndani yake alimzaa Yule ambaye mbingu na mbingu za juu haziwezi kumtosha (rej. 1 Wafalme 8:27). Papa ameomba wajikabidhi kwake, wakiomba ari iliyofanywa upya na upendo motomoto unaotoa ushuhuda wa Injili bila kuchoka na kwa furaha. Kuendelea! Aidha Baba Mtakatifu amewaomba wamisionari hao wawe jasiri, wasichoke kusonga mbele. Amewashukuru kwa ushuhuda wao! Bwana mwenyewe amewachagua na kuwaamini; “Mimi nipo pamoja nanyi na kwa moyo wangu wote ninawambia: asante; asante kwa ushuhuda wenu, asante kwa maisha yenu yaliyomiminwa kwa ajili ya Injili! Mdumu katika maombi na ubunifu katika upendo, thabiti katika umoja, wenye furaha na wapole katika kila kitu na kwa kila mtu. Ninawabariki kutoka moyoni mwangu, na nitawaweka katika maombi yangu. Na ninawaomba, tafadhali, msisahau kuniombea.” Papa Francisko amehitimisha hotuba yake.

02 September 2023, 14:06