Tafuta

2023.08.31 Viaggio Apostolico in Mongolia 2023.08.31 Viaggio Apostolico in Mongolia  (Vatican Media) Tahariri

Fundisho la kisinodi kutoka 'zizi dogo' la Mongolia

Mkurugenzi wetu wa Tahariri anatoa maoni yake kuhusu ushuhuda wa utume katika maneno ya mhudumu wa kichungaji Rufina Chamingerel na katika msisitizo wa Papa Francisko wa maelekezo ya thamani kwa ajili ya kazi ya sinodi.

Na Andrea Tornielli

Jina lake ni Rufina Chamingerel, ni muhudumu wa kichungaji ambaye siku ya Jumamosi tarehe 2 Septemba 2023 alihutubia maneno machache kwa Papa Francisko wakati wa mkutano katika Kanisa kuu la Ulaanbaatar. Yeye alisema kuwa ; “Bado sijui jinsi ya kutafsiri neno ‘jumuiya’ katika lugha yetu ... Kanisa letu liko katika awamu ile ya kawaida ya watoto ambao mara kwa mara huwauliza wazazi wao maswali ... Tuna bahati sana kwa kuwa hatuna vitabu vingi vya katekesi katika lugha yetu, lakini tuna wamisionari wengi ambao ni vitabu hai. Ningependa kusisitiza ufanisi wa Sinodi ya kisinodi. Wakati wa Sinodi waamini wetu, hasa wachungaji, waliweza kuelewa vyema zaidi hali halisi ya Kanisa na kuwa na maono kamili zaidi kwa ajili ya parokia zetu”. Maelekezo ya thamani kwa ajili ya Sinodi ya kisinodi inatoka katika  ‘zizi dogo’ la Kikatoliki katika nyika za Kimongolia. Kazi ya kisinodi iliyoshuhudiwa hapa ilifanya “hali halisi ya Kanisa ieleweke vyema.”

Mara baada ya maelezo ya Rufina Papa Francisko katika hotuba yake kwa Wakatoliki wa Mongolia alitaka “kusisititiza  neno hili: ‘umoja.’ Kwa sababu, alieleza kuwa  “Kanisa haliwezi kueleweka kwa msingi wa kigezo cha utendaji kamili: hapana, Kanisa si shirika linalofanya kazi” bali “ni kitu kingine.” Neno “Umoja” linaeleza vyema nini maana ya Kanisa: “Katika mwili huu wa Kanisa, Askofu hatendi kama msimamizi wa vipengele mbalimbali labda kwa kuzingatia kanuni ya wengi, bali kwa kanuni ya kiroho, ambayo kwayo Yesu mwenyewe anakuwapo katika nafsi ya Askofu ili kuhakikisha umoja  katika Mwili wake wa Fumbo”. “L'Eglise est une Communion” yaani Kanisa ni Umoja ni jina la kitabu kilichoandikwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na Mdominikani  Jérôme Hamer, aliyekuwa katibu wa baadaye wa Baraza la Kipapa  la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Kadinali. Mafundisho ya Kanisa la umoja, lilithibitisha Sinodi ya Maaskofu ya mnamo mwaka 1985, kuwa  ni “wazo kuu na la msingi katika nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican”.

Papa Francisko ameeleza mara nyingi kwamba kanuni ya mchezo wa kidemokrasia ya  walio wengi na walio wachache haitumiki katika maisha ya Kanisa na haiheshimu asili yake. Kwa hiyo kutoka katika mji mkuu wa Mongolia, Papa alisema: “Umoja katika Kanisa si suala la utaratibu na heshima, wala si mkakati mzuri wa ‘kufanya timu’; ni suala la imani na upendo kwa Bwana, ni uaminifu kwake. Kwa hiyo ni muhimu vipengele vyote vya kikanisa viungane kumzunguka Askofu, anayemwakilisha Kristo aliye hai katikati ya Watu wake, akijenga umoja huo wa sinodi ambayo tayari ni tangazo na ambalo linasaidia katika kutamadunisha imani.” Sinodi, ambayo sasa iko juu yetu, ni fursa ya kupata uzoefu na kukua katika ufahamu wa maana ya kuishi umoja wa kikanisa, si kulingana na mantiki ya kidunia, si kulingana na ‘ajenda’ za uwongo za mtu binafsi au za kikundi, lakini kwa kugundua tena umoja katika sala na kusikilizana, kila mtu kuacha aongozwe na Roho na hivyo kuweka katika ukuu wa vitendo mwelekeo wa kuwa Kanisa. Na mwelekeo uliopo katika Kanisa tangu asili yake.


Akipokea tuzo ya “è giornalismo”, yaani “ni uandishi” mnamo Agosti 26, Papa Francisko alisema: “Kwa hakika katika wakati huu, ambapo mengi yanasemwa na machache yanasikilizwa, na ambayo hisia ya hatari ya kawaida inadhoofika, Kanisa zima limeanza mchakato wa  safari ya kugundua tena neno pamoja. Lazima tugundue tena neno pamoja. Kutembea pamoja. Kujiuliza maswali pamoja. Kuchukua jukumu pamoja  la utambuzi wa jumuiya, ambalo kwetu sisi ni sala, kama Mitume wa kwanza walivyofanya: ni sinodi, ambayo tungependa kuifanya iwe tabia ya kila siku katika usemi wake wote. Kwa kusudi hili hasa, katika mwezi mmoja, maaskofu na walei kutoka sehemu zote za dunia watakusanyika hapa Roma kwa ajili ya Sinodi ya kisinodi: kusikiliza pamoja, kutambua pamoja, kusali pamoja.” Kutoka Mongolia, moyoni mwa Asia, Kanisa changa lililo na umbali wa kilomita nyingi kutoka Roma lakini karibu sana na moyo wa Papa, linakuja na fundisho kwa ajili ya Sinodi ya mababa na akina mama ambao katika siku chache zijazo  watakusanyika karibu na Mrithi wa Petro ili kuomba, kusikilizana na kutambua kwa pamoja ni jinsi gani ya kutangaza Injili kwa wanawake na wanaume wa wakati wetu.

04 September 2023, 15:32