Tafuta

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania  (REUTERS)

Salam za Pongezi kwa Makardinali Wapya! Kardinali Protase Rugambwa! TEC

Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Ukardinali umegawanyika katika ngazi kuu tatu: Kardinali Askofu, Kardinali Padre na Kardinali Shemasi. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawapongeza Makardinali wapya na hasa wanaotoka Barani Afrika, kielelezo cha ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Kimsingi, idadi ya Makardinali inapaswa kuwa ni Makardinali 137, Idadi ya Makardinali wenye sifa za kuchagua au kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ikiwa kama kutafanyika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.Takwimu zinaonesha kwamba hadi mwezi Septemba 2023 Bara la Ulaya lina na Makardinali 53 kati yao Makardinali kutoka Italia 15; Amerika ya Kaskazini wapiga kura ni 15, Marekani ikiwa na wapiga 11 na 4 ni kutoka Canada. Makardinali kutoka Amerika ya Kusini wapiga kura ni 19 na Bara la Afrika wapiga kura ni 23, Barani Asia, Makardinali wapiga kura ni 23 wakati ambapo Oceania wapiga kura ni 3. Hawa ni Makardinali wanaoonesha ukatoliki wa Kanisa, wanaotumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu kwa watu wote wa Mataifa. Makardinali hawa wameingizwa kwenye Jimbo kuu la Roma ili kuonesha mahusiano na mafungamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Ukardinali umegawanyika katika ngazi kuu tatu: Kardinali Askofu, Kardinali Padre na Kardinali Shemasi.

Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini
Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini

Uteuzi wa Makardinali wapya na hatimaye kusimikwa kwao ni changamoto kubwa inayowataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Jicho la kibaba linalooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ni chachu ya matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kutawala katika maisha ya watu! Makardinali kutoka Afrika ni: Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, nchini Tanzania. Kardinali Protase Rugambwa alizaliwa tarehe 31 Mei 1960 huko Bunena-Bukoba nchini Tanzania, akapata Daraja Takatifu ya Upadri kutoka mikononi mwa Mtakatifu Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania tarehe 2 Septemba 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Baada ya kulitumikia Baraza kwa vipindi viwili na muda wake ulipogota ukomo, kadiri ya Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu Mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu Mwandamizi wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Kardinali Stephen Brislin, Askofu mkuu Jimbo kuu la Cape Town
Kardinali Stephen Brislin, Askofu mkuu Jimbo kuu la Cape Town

Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini ambaye alizaliwa huko Alodu Jimbo Katoliki la Torit, Sudan Kusini kunako tarehe 10 Januari 1964. Alijiunga na Seminari ndogo ya Torit, kati ya mwaka 1978 - 1981 na baadaye akaendelea na seminari ya Wau, tangu 1981- 1983. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 21 Aprili 1991, akapewa daraja takatifu ya Upadre katika Jimbo Katoliki la Torit Sudan ya Kusini. Tarehe 3 Januari 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa jimbo Katoliki la Torit, Sudan Kusini. Katika maisha na utume wake amewahi kuwa: Jaalim na Profesa na Dekano wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini. Kardinali Stephen Brislin Askofu mkuu wa Jimbo kuu la “Cape Town”, Afrika ya Kusini alizaliwa tarehe 24 Septemba 1956 huko Welcome. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 19 Novemba 1983 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Kroonstad, Afrika ya Kusini. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 17 Oktoba 2006 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kroonstad na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 28 Januari 2007. Na ilipogota tarehe 18 Desemba 2009 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Cape Town, Kaapstad, Afrika ya Kusini na tarehe 30 Septemba 2023 anasimikwa kuwa Kardinali. Jimbo kuu la Tabora, Jimbo kuu la Juba pamoja na Jimbo kuu la Cape Town, Kaapstad, Afrika ya Kusini, kwa mara ya kwanza katika historia majimbo haya makuu yamepata Kardinali tayari kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza wa Mungu.

Kardinali Luis Pascual Dri, Umri miaka 96 huduma ya Upatanisho
Kardinali Luis Pascual Dri, Umri miaka 96 huduma ya Upatanisho

Kardinali Luis Pascual Dri, Mtawa Mfranciskani Mkapuchini alizaliwa tarehe 17 Aprili 1927, Entre Rios, Argentina. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa tarehe 21 Februari 1945 akaweka nadhiri za kwanza na mwaka 1949 akaweka nadhiri za daima. Tarehe 29 Machi 1952 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Alibahatika katika maisha na utume wake kuwa Gambera wa Seminari ya Serafico di Villa Gdor; Mlezi wa Wanovisi, Paroko na kuanzia mwaka 2007 akajichimbia kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei “Santuario di Nuestra Señora de Pompeya.” Nchini Argentina. Leo hii ana umri wa miaka 96 na anaendelea kuwahudumia watu wa Mungu kwa kutoa Sakramenti ya Upatanisho! Chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, tayari kuomba huruma, msamaha na upendo wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawapongeza Makardinali wapya
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawapongeza Makardinali wapya

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC anawapongeza Makardinali wapya 21 walioteuliwa na hatimaye kusimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Makardinali wapya wanakuwa ni wajumbe wa Baraza la Makardinali, chombo cha juu kabisa cha ushauri kwa Baba Mtakatifu. Kati yao kuna Makardinali wapya watatu kutoka Barani Afrika: Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini; Kardinali Stephen Brislin Askofu mkuu wa Jimbo kuu la “Cape Town”, Afrika ya Kusini pamoja na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Askofu Flavian Matindi Kassala katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuonesha furaha kubwa kwa watu wa Mungu nchini Tanzania waliopokea uteuzi wa Kardinali Protase Rugambwa kwa mshangao mkubwa, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumrejesha Tanzania kama zawadi kubwa baada ya utume uliotukuka katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Jimbo kuu la Tabora likampokea kwa shangwe kubwa. Shangwe hii ikaongezeka zaidi tarehe 9 Julai 2023 baada ya Baba Mtakatifu kumteuwa Askofu mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa kuwa ni kati ya Makardinali wapya walioteuliwa na Baba Mtakatifu, ambao wamesimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Makardinali wapya 21 wakiingia kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro
Makardinali wapya 21 wakiingia kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC linawapongeza Makardinali wapya na kwamba, uwakilishi wao una maana yake: makuzi na ukomavu wa imani. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC linampongeza sana Kardinali Protase Rugambwa kwa kurejea nchini Tanzania akiwa na uzoefu na mang’amuzi mapana juu ya mchakato wa uinjilishaji wa watu. Leo tarehe 30 Septemba 2023 Tanzania inaandika historia nyingine tena kwa kupata Makardinali watatu: Kardinali Laurian Rugambwa, Kardinali Polycarp Pengo na sasa Kardinali Protase Rugambwa. Hii ni furaha kubwa kwa Tanzania ambayo haina sifa kubwa sana, lakini inathaminiwa na kuheshimiwa sana na kwamba, huu ni upendeleo wa pekee kwa Bara la Afrika, lakini Tanzania kwa namna ya pekee. Askofu Flavian Matindi Kassala anakaza kusema, kuna matarajio makubwa kwa Kardinali Protase Rugambwa kwa Jimbo kuu la Tabora, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzannia na Kanisa Barani Afrika, kwa kuwa ni Mshauri wa Baba Mtakatifu mwenye umri wa ujana, mwenye uzoefu na mang’amuzi mapana mintarafu mchakato wa uinjilishaji wa watu wa Mungu.

Wakati wa uundaji wa makardinali

Uteuzi huu ni kielelezo cha ukomavu na udumifu wa imani na ukomavu wa majimbo ya Tanzania yanayoadhimisha Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Iringa, Miaka 60 ya Jimbo kuu la Arusha pamoja na Jubilei ya Jimbo kuu la Songea. Hiki ni kipindi ambacho watu wa Mungu nchini Tanzania wamejaa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga kuwekwa na kusimikwa rasmi kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Iringa, Jimbo kuu la Songea na Jimbo kuu la Arusha. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania kumsindikiza Kardinali Protase Rugambwa kwa sala, kwa upendo na ushuhuda wa imani tendaji katika medani mbalimbali za maisha. Tanzania inaheshimika na kuaminika, kumbe kuna haja ya kuendelea kuheshimiana, kuthaminiana, kusameheana, kupendana na kushauriana bila kusahau kupongezana pale mambo mema na mazuri yanapotendeka. Hizi ni tunu msingi za watanzania zinazobebwa na asili ya watanzania kutoka kwa waasisi wa Taifa la Tanzania. Kardinali Protase Rugambwa, karibu katika utume kwa watu wa Mungu Tanzania, Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake.

Pongezi kwa Makardinali wapya 2023
30 September 2023, 14:12