Tafuta

Papa amerudi kutoka Marsiglia na kuzungumza na waandishi:Maisha sio ya kuchezea

Papa Francisko akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege ya kurudi kutoka Ufaransa alisema uhamiaji unaoendeshwa vizuri ni hazina na alitoa onyo la kujihadhari na ukoloni wa kiitikadi unaoharibu maisha ya mwanadamu.Kwa upande wa vita vya Ukraine anasema hatupaswi kucheza na mauaji ya watu hao.

Vatican News

Baba Mtakatifu Francisko alirejea jijini Roma Jumamosi usiku 23 Septemba 2023 katika hitimisho la Ziara  yake ya Kitume ya siku mbili kwenda Marsiglia, kusini mwa Ufaransa. Alifanya mkutano wake wa kawaida na waandishi wa habari ndani ya ndege ya upapa, kwa kujibu maswali matatu. Kwa njia hiyo ifuatayo ni tafsiri ya Kiswahili kuhusu mkutano huo na waandishi wa Habari  ambapo kwa kawaida  utangulizi huanza kwa makaribisho kutoka kwa msemaji wa vyombo vya Habari Vatican Dk. Matteo Bruni: Habari za jioni, Baba Mtakatifu, jioni njema nyote. Asante kwa kuchukua muda huu kwenye ndege yetu ya kurudi. Ilikuwa ni safari maalum ambayo pia uliweza kuhisi, kama Mtukufu alivyosema, mapenzi yote ya Wafaransa waliokuja kusali nawe. Lakini nadhani bado kuna maswali au masuala machache ambayo waandishi wa habari wangependa kukuuliza. Labda ungependa kusema maneno machache kwetu.

Papa Francisko: Habari za jioni na asante sana kwa kazi yenu. Kabla sijasahau ninataka kusema mambo mawili. Leo nadhani ni ndege ya mwisho ya Roberto Bellino [Mhandisi wa Sauti na Barazala Kipapa la Mawasiliano, kwa sababu anastaafu (makofi). Asante, asante, asante! Jambo la pili ni kwamba leo ni siku ya kuzaliwa ya Rino, Rino asiyeweza kusema [Anastasio, mratibu wa Kampuni ya Ndege ITA wa safari za papa] (makofi). Sasa unaweza kuuliza swali lako.

Raphaële Schapira (TV ya Ufaransa)

Baba Mtakatifu, habari za jioni. Ulianza upapa wako huko Lampedusa, ukilaani kutojali. Miaka kumi baadaye unaomba Ulaya kuonesha mshikamano. Umekuwa ukirudia ujumbe huo kwa miaka kumi. Ina maana umeshindwa?

Papa Francisko: Ningesema hapana. Ningesema kwamba ukuaji umekuwa polepole. Leo kuna ufahamu wa tatizo la uhamiaji. Kuna fahamu. Na pia, kuna ufahamu wa jinsi imefikia hatua ... kama kiazi cha moto ambacho hujui jinsi ya kushughulikia. Angela Merkel aliwahi kusema kuwa unatatuliwa kwa kwenda Afrika na kutatua barani Afrika, kwa kuinua kiwango cha watu wa Kiafrika. Lakini kumekuwa na kesi ambazo ni mbaya. Kesi mbaya sana, ambapo wahamiaji, kama mchezo wa ping pong, wamerudishwa. Na inajulikana kuwa mara nyingi huishia kwenye lager; mwisho wao ni mbaya zaidi kuliko hapo awali.

Nilifuatilia maisha ya kijana Mahmoud aliyekuwa akijaribu kutoka nje... na mwisho akajinyonga. Hakufanikiwa kwa sababu hakuweza kustahimili mateso haya. Nakwambia usome kitabu hicho "Ndugu" - "Hermanito". Watu wanaokuja wanauzwa kwanza. Kisha wanachukua pesa zao. Kisha wanawafanya waite familia yao kwa simu ili kutuma pesa zaidi. Lakini ni watu maskini. Ni maisha ya kutisha. Nilimsikia mmoja ambaye usiku, wakati wa kupanda mashua, aliona chombo wazi sana, bila ulinzi wowote hakutaka kupanda. Na, boom boom. Mwisho wa historia. Ni utawala wa ugaidi. Wanateseka sio tu kwa sababu wanahitaji kutoka, lakini kwa sababu ni utawala wa ugaidi huko. Ni watumwa. Na hatuwezi - bila kuona mambo - kuwarudisha kama mpira wa ping pong. Hapana.

Ndiyo maana nasisitiza kwamba kimsingi wahamiaji lazima wapokelewe, wasindikizwe, wapandishwe vyeo na wajumuishwe. Ikiwa huwezi kumuunganisha katika nchi yako, wasindikize na uwajumuishe katika nchi nyingine, lakini usiwaache mikononi mwa walaghai hawa wakatili. Suala la wahajiri ni hili: kwamba tuwarudishe na wanaangukia mikononi mwa hawa wanyonge wanaofanya maovu mengi. Wanawauza; wanawanyonya. Watu wanajaribu kukimbia. Kuna baadhi ya makundi ya watu wanaojitolea kuokoa watu kwa boti. Nilimwalika mmoja wao, mkuu wa “Mediterranea Saving Humans” kwenye Sinodi. Wanakusimulia historia za kutisha.

Katika safari yangu ya kwanza, ulikumbusha, nilikwenda Lampedusa. Mambo yamekuwa mazuri. Wameweza kweli. Kuna ufahamu zaidi. Hapo nyuma hatukujua. Zamani hawakutuambia ukweli. Nakumbuka kulikuwa na mhudumu wa mapokezi huko Mtakatifu Marta, Muethiopia, binti wa Waethiopia. Alizungumza lugha hiyo, na alikuwa akifuatilia safari yangu kwenye TV. Aliona kuna mtu ambaye alieleza, Mwethiopia maskini, ambaye alielezea mateso na mambo hayo. Na mfasiri - bibi huyo aliniambia - hakusema kila kitu; alipendeza hali. Ni vigumu kuamini. Mikasa ni mingi  sana.

Siku hiyo nilikuwepo. Daktari mmoja aliniambia: “Mtazame mwanamke huyo. Alitembea kati ya maiti akitafuta sura kwa sababu alikuwa akimtafuta binti yake. Hakumpata.” Tamthilia hizi...ni vyema tuzichukue mikononi. Itatufanya kuwa wanadamu zaidi na kwa hivyo pia watakatifu zaidi. Ni wito. Ninatamani ingekuwa kama kilio. Tuwe makini. Hebu tufanye kitu. Ufahamu umebadilika. Ina ukweli. Leo kuna fahamu zaidi. Sio kwa sababu nilizungumza, lakini kwa sababu watu wamegundua shida. Wengi wanazungumza juu yake. Ilikuwa ni safari yangu ya kwanza. Nataka kusema jambo moja zaidi. Sikujua hata Lampedusa ilikuwa wapi, lakini nilisikia hivyo: Nilisoma kitu, na katika maombi nilisikia “lazima uende” Kana kwamba Bwana alikuwa akinituma huko, katika safari yangu ya kwanza.

Sehemu I ya maswali na majibu ya Papa Francisko kwa waandishi 23.09.2023

Clément Melki - Agence France-Presse (AFP)

Asubuhi hii ulikutana na Emmanuel Macron baada ya kuelezea kutokubaliana kwako na euthanasia. Serikali ya Ufaransa inajiandaa kupitisha sheria yenye utata ya mwisho wa maisha. Unaweza kutuambia kwa ukarimu ulichomwambia rais wa Ufaransa kuhusu hili na kama unadhani unaweza kubadilisha mawazo yake.

Papa Francisko: Hatukuzungumza juu ya suala hili leo, lakini tulizungumza juu yake kwenye ziara nyingine tulipokutana. Nilizungumza kwa uwazi, alipofika Vatican, na nilizungumza maoni yangu waziwazi: maisha si ya kuchezewa, wala mwanzoni wala mwisho. Hatuwezi kucheza karibu. Haya ni maoni yangu: kulinda maisha, unajua? Kwa sababu basi tunamalizia na sera ya "hakuna maumivu", ya euthanasia ya kibinadamu. Katika hatua hii, ninataka kutaja kitabu tena. Tafadhali soma. Ni kutoka 1907. Ni kitabu kiitwacho Bwana wa Ulimwengu, kilichoandikwa na (Robert Hugh) Benson. Ni kitabu cha mwisho wa dunia kinaonesha jinsi mambo yatakavyo kuwa mwishoni. Tofauti zote huondolewa, ikiwa ni pamoja na maumivu yote. Euthanasia ni mojawapo ya mambo haya, kifo cha pole pole, uteuzi kabla ya kuzaliwa. Inatuonesha jinsi mtu huyu alivyokuwa ameona kabla baadhi ya migogoro ya sasa.

Leo tuwe makini na ukoloni wa kiitikadi unaoharibu maisha ya mwanadamu na kwenda kinyume na maisha ya mwanadamu. Leo, kwa mfano, maisha ya babu na bibi yanafutwa, na wakati utajiri wa binadamu unapoingia katika mazungumzo na wajukuu, unafutika. ‘Wamezeeka hivyo hawana faida.’ Hatuwezi kucheza na maisha. Wakati huu sikuzungumza na rais (kuhusu mada hii), lakini mara ya mwisho nilizungumza. Alipokuja nilimpa maoni yangu kuwa maisha si kitu cha kuchezewa. Ikiwa ni sheria ya kutomwacha mtoto akue tumboni mwa mama au sheria ya euthanasia katika ugonjwa au uzee, sisemi suala la imani. Ni suala la kibinadamu, suala la kibinadamu. 'Ni huruma mbaya'. Sayansi imekuja kugeuza baadhi ya magonjwa yenye uchungu kuwa matukio yenye uchungu kidogo, yakiambatana na dawa nyingi. Lakini maisha hayapaswi kuchezewa.

Javier Martínez-Brocal – ABC

Baba Mtakatifu, asante kwa kuchukua muda kujibu maswali yetu, kwa safari hii nzito na nene. Hadi mwisho ulizungumza kuhusu Ukraine na Kadinali Zuppi amewasili Beijing. Je, kuna maendeleo yoyote katika tume hizi? Angalau juu ya suala la kibinadamu la kurudi kwa watoto? Kisha swali kali kwa kiasi fulani: wewe binafsi unapataje ukweli kwamba tume hizi hazijaweza kupata matokeo yoyote madhubuti hadi sasa. Katika katekesi ulizungumza juu ya kufadhaika. Je, unahisi kuchanganyikiwa? Asante.

Papa Francisko: Hiyo ni kweli, baadhi ya kuchanganyikiwa kunaonekana, kwa sababu Sekretarieti ya Vatican  inafanya kila kitu kusaidia hili, na hata "Tume ya Zuppi" imekwenda huko. Kuna kitu kinaendelea vizuri kwa watoto, lakini vita hii inanifanya nifikirie kwamba kwa kiasi fulani imeathiriwa sio tu na shida ya Kirussi / Kiukraine, lakini pia na uuzaji wa silaha, biashara ya silaha. Mchumi mmoja alisema miezi michache iliyopita kwamba leo hii vitega uchumi vinavyotoa mapato mengi zaidi ni viwanda vya kutengeneza silaha, [ambavyo] kwa hakika ni viwanda vya kifo!

Watu wa Kiukraine ni watu waliouawa; wana historia ya kifo cha kishahidi, historia inayowafanya wateseke. Sio mara ya kwanza: wakati wa Stalin, waliteseka sana, sana; ni watu waliouawa kishahidi. Lakini hatupaswi kuchezea mauaji ya watu hawa; inabidi tuwasaidie kutatua mambo kwa njia inayowezekana kabisa. Katika vita, kinachowezekana ni kile kinachowezekana, bila kuwa na udanganyifu: kana kwamba kesho viongozi wawili wa vita watatoka kula pamoja. Lakini kadiri inavyowezekana, pale tunapofikia hatua ya kufanya linalowezekana. Sasa nimeona kwamba baadhi ya nchi zinarudi nyuma, kwamba hazitoi silaha, na zinaanzisha mchakato ambapo mashahidi watakuwa watu wa Kiukraine. Na hilo ni jambo baya!

Umebadilisha mada, ndiyo maana ningependa kurudi kwenye somo la kwanza, Safari. Marsiglia ni ustaarabu wa tamaduni nyingi, tamaduni nyingi, ni bandari ya wahamiaji. Wakati mmoja kulikuwa na wahamiaji kwenda Cayenne, wale waliohukumiwa kifungo waliondoka hapo - Askofu mkuu (wa Marsiglia alinipatia Manon Lescaut) ili kunikumbusha historia hiyo. Lakini Marsiglia ni utamaduni wa kukutana! Jana katika mkutano na wawakilishi wa madhehebu  mbalimbali wanaishi pamoja: Waislamu, Wayahudi, Wakristo, lakini kuna kuishi pamoja, ni utamaduni wa usaidizi; Marsiglia ni muundo mzuri wa  ubunifu; ni utamaduni huu wa ubunifu. Bandari ambayo ni ujumbe katika Ulaya: Marsiglia inakaribisha. Inakaribisha na kuunda mchanganyiko bila kukataa utambulisho wa watu. Tunapaswa kufikiria upya suala hili kwa sehemu nyingine: uwezo wa kukaribisha.

Kurudi kwa wahamiaji, kuna nchi tano ambazo zinateseka kutokana na wahamiaji wengi, lakini katika baadhi ya nchi hizi, kuna miji tupu. Nafikiria kesi halisi ninayoijua, kuna mji ambao kuna wazee 20 na hakuna zaidi. Tafadhali acha miji hii ifanye juhudi za kujumuika. Tunahitaji kazi; Ulaya ina haja yake. Uhamiaji uliofanywa vizuri ni utajiri; ni utajiri. Hebu tuzingatie sera hii ya uhamiaji ili izae zaidi na kwa sababu inatusaidia sana. Sasa  chakula cha jioni kinafika kwa ajili ya kuaga Rino na Roberto. Hebu tuishie hapa; asante sana kwa kazi yenu na maswali yenu.

Alihitimisha Baba Mtakatifu Franciskona katika mabano kwenye tafsiri ni maneno ambayo yanapaswa kufafanuliwa kwa kirefu zaidi

24 September 2023, 07:51