Tafuta

2023.09.15 Papa akutana na washiriki wa Kongamano la V la waoblate wa kibenediktini. 2023.09.15 Papa akutana na washiriki wa Kongamano la V la waoblate wa kibenediktini.  (Vatican Media)

Papa amehimiza kujali maskini kwa mfano wa Mt.Benedikto

Katikitana na washiriki wa Kongamano la tano la Dunia la Waoblate wa Kibenediktini Papa amewasihi kwa mara nyingine tena wasijitolee katika ubinafsi na kutojali wale wanaohitaji na wasiingie kwenye mazungumzo ambayo yanachafua wengine.Waige mfano wa kuishi utauwa wa enzi za kati.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Tafakari ya ukarimu ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyoiendeleza kwa kutoa mwaliko kwa upya wa kuwa na heshima kwa wale wanaotafuta ukarimu na kuwapendelea maskini, imesikika katika hotuba kwa washiriki wa Kongamano la Tano la Wabenediktini Duniani, aliokutana nao katika  Ukumbi wa Clementina katika Jumba la kitume tarehe 15 Septemba 2023. Baba Mtakatifu amesem wakati mwingine inaonekana badala yake kwamba jamii yetu inasongwa polepole katika usalama uliotiwa muhuri wa ubinafsi, na kutojali. Leo majaribu ni kujifungia, na hii pia inafanywa kwa kuzungumza, kuwachafua wengine, kuwahukumu na kujifungia mwenyewe binafsi. Badala yake lugha ni kwa ajili ya kumsifu Mungu, si kwa ajili ya kuzungumza kuhusu wengine, Papa Francisko ameonya. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu amewakumbusha Wabenediktini kwamba Mtakatifu Benedikto, katika kanuni za Utawala wake, aliwataka kuwa na moyo uliopanuliwa na ukuu wa upendo usioelezeka, na hivyo Papa akaongeza kusema kwamba moyo huo uliopanuka ni sifa ya roho ya Benediktini  na ambayo ni siri ya kazi kuu ya uinjilishaji unaofanywa na utauwa uliozaliwa na mtakatifu wa Norcia. 

Papa pia amependa kutafakari mambo matatu yanayotokana na kupanuka kwa moyo kuwa ni  utafutaji wa Mungu, shauku ya Injili na ukarimu. Ikiwa utafutaji wa kudumu wa Mungu ndio kwanza kabisa unatofautisha maisha ya Kibenediktini, yenye lengo la kutambua mapenzi ya Muumba katika Neno lake, katika kutafakari kwa uumbaji, katika matukio ya kila siku na katika kazi hai kama maombi, shauku kwa ajili ya Injili ni bidii inayotokana nayo. Na kwa hivyo mwaliko wa Baba Mtakatifu  Fransisko kwa Wabenediktini ni kubadilisha mazingira ya maisha ya kila siku, kwa kufanya kazi kama chachu kwenye unga, kwa ustadi na uwajibikaji, na wakati huo huo kwa upole na huruma, kama utawa wa  Zama za Kati.

Papa amekutana na washiriki wa kongamano la tano la waoblate wabenediktini
Papa amekutana na washiriki wa kongamano la tano la waoblate wabenediktini

Pamoja na kielelezo chake cha maisha ya kiinjili kilichojikita kwenye kauli mbiu ya Shirika ora et labora", yaani Kazi na sala, Baba Mtakatifu amesema kilipelekea kuongoka kwa amani na kuunganishwa kwa watu wengi . Lengo ni kuleta Injili katika maisha ya kila siku. Kwa hiyo katika ulimwengu wa utandawazi lakini uliogawanyika, wenye pupa unaojitolea kwa ulaji, katika mazingira ambayo mizizi ya familia na kijamii wakati mwingine inaonekana karibu kuvunjika, pasiwepo na  Wakristo wanaonyoosha vidole, lakini wawe ni  mashuhuda wenye shauku ambayo inatoa nuru ya  Injili katika maisha kwa njia ya maisha, Papa amesisitiza.  Aidha amesema kuwa jaribio daima ni hili la kutoka kuwa mashuhuda wa Kikristo hadi kuwa washtaki wa Kikristo.  Amekazia Papa kuwa Kuna mshitaki mmoja tu ambaye ni shetani. Kwa hiyo amesisitiza kuwa “Tusicheze nafasi ya shetani, bali tucheze na nafasi ya Yesu,  ya shule ya Yesu, ya Heri yake.

Papa akisalimiana na mdogo wakati wa kuaga baada ya kukutana na waoblati wabenedikitini
Papa akisalimiana na mdogo wakati wa kuaga baada ya kukutana na waoblati wabenedikitini

Hatimaye Baba Mtakatifu akifafanua juu ya ukarimu alisisitizia ishara ambazo Mtakatifu Benedikto aliamuru katika suala hilo kwamba wema wa kuoneshwa kwa mgeni, kushiriki katika wakati wa sala, na kushirikisha kile ambacho mtu anacho.  Na baadaye kuwa na  wasiwasi wa akiba hasa kwa ajili ya maskini na mahujaji kwa sababu ni hasa ndani yao kwamba Kristo anapokelewa kwa njia maalum sana alisema Mtakatifu Benedikto. Kwa hiyo Papa ameongeza kusema kuwa kama Waoblate , monasteri zao  kuu ni ulimwengu, jiji, mahali pa kazi, na hapo wameitwa kuwa mifano ya ukarimu kwa heshima kwa wale wanaobisha mlango wao na kwa upendeleo kwa maskini. Pamoja na hayo yote, Papa ametoa mwaliko wa utakatifu  kuwa ni kuendelea kupanua mioyo yao, na kuukabidhi kila siku kwa upendo wa Mungu, bila kukoma kuutafuta, kuushuhudia kwa shauku na upendo, lakini zaidi ya yote ni kuukaribisha kupitia kwa maskini zaidi.

Hotuba ya Papa kwa waoblate wabenediktini
15 September 2023, 17:10