Tafuta

Papa Francisko: Tarehe 30 Septemba 2023 Kusimikwa kwa Makardinali wapya 21 kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Papa Francisko: Tarehe 30 Septemba 2023 Kusimikwa kwa Makardinali wapya 21 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.  (Vatican Media)

Makardinali Wapya: Ujio wa Roho Mtakatifu: Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki la Mitume

Ni katika asili ya watu wa Mungu, Roho Mtakatifu ametenda kazi ya kutangaza na kushuhudia Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu, Fumbo ambalo limewafikia watu wa Mataifa katika lugha zao za asili, kupitia kwa wazazi, makatekista, mapadre, wamisionari bila kuwasahau mabibi na mababu. Makardinali wapya wanaitwa na kutumwa kuwa ni wainjilishaji, kwani wao wameinjilishwa kwanza, tayari kupyaisha kumbukumbu na zawadi ya imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 aliwateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia zaidi uwakilishi wa Makardinali toka sehemu mbalimbali za dunia, kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste ya kwanza, hawa ni Makardinali na Maaskofu wa nyakati hizi, ili kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; tayari kusimama kidete na kuwa ni wainjilishaji, huku wakimwilisha ndani mwao, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuendelea kumwaminia Roho Mtakatifu anayetengeneza utofauti na umoja; kiongozi mpole na thabiti. Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu, Ubatizo na kuzaliwa kwa Kanisa na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila Taifa chini ya mbingu, Rej. Mdo 2: 1-11. Baba Mtakatifu anasema, hawa ni mfano wa Makardinali na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, mshangao wa Roho Mtakatifu na kwamba, Makardinali wapya nao wanafananishwa na kundi lile la Waparthi, Wamedi na Waelami na kwamba, Mitume wote walikuwa wanatoka Galilaya.

Makardinali Wapya: Wainjilishaji na Mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo
Makardinali Wapya: Wainjilishaji na Mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kati ya Wayahudi na waongofu anajiweka pia yeye mwenyewe akiwa mstari wa mbele, watu ambao walibahatika kuwa ni wadau wa Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, Ujio wa Roho Mtakatifu aliyeliwezesha Kanisa: moja, takatifu katoliki na la mitume kuzaliwa. Huu ni mwaliko wa kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe. Kugundua ile zawadi ya kuinjilishwa na kwa kupokea zawadi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, “Kerygma”, na hatimaye kufanyika kuwa ni sehemu ya Mama Kanisa anayezungumza lugha zote na ndiyo maana ya kuwa ni Katoliki. Baba Mtakatifu anasema, kabla ya mtu kuwa ni: Mtume, Padre, Askofu au Kardinali walikuwa ni Waparthi, Wamedi na Waelami, kielelezo makini cha neema ya Injili kwa watu wa Mataifa. Ni katika asili ya watu wa Mungu, Roho Mtakatifu ametenda kazi ya kutangaza na kushuhudia Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu, Fumbo ambalo limewafikia watu wa Mataifa katika lugha zao za asili, kupitia kwa wazazi, makatekista, mapadre, wamisionari bila kuwasahau mabibi na mababu. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu kuwa ni wainjilishaji, kwa sababu kwanza kabisa wameinjilishwa, tayari kupyaisha kumbukumbu na zawadi ya imani. Pentekoste kama Ubatizo ni tukio ambalo Mwenyezi Mungu anaendelea kulipyaisha Kanisa na watoto wake kila wakati, ili kuendelea kuishi leo ya Mungu mintarafu imani. Makardinali wapya wameteuliwa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, zawadi ya Roho Mtakatifu aliyewainjilisha watu wao, leo hii Roho Mtakatifu anapyaisha ndani mwao wito na utume wa Kanisa kwa ajili ya Kanisa.

Makardinali wapya: Changamoto ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Makardinali wapya: Changamoto ni ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Baraza la Makardinali linapaswa kufanya kazi kwa umoja mintarafu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kila Kardinali anapaswa kushirikisha karama na vipaji vyake, ili kwa pamoja waweze kutoa sauti moja inayosikilizwa na wote. Huu ni wito wa kusikilizana, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, kwa kujikita katika kipaji cha ugunduzi na uaminifu katika ujenzi wa umoja wa Kanisa. Makardinali wapya wajifunze kuwa wamoja katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, daima watambue kwamba, wanaye Roho Mtakatifu, Mwalimu kiongozi, anayewawezesha kutembea huku wakiwa wameshikamana. Roho Mtakatifu anaunda tofauti na kukuza umoja, ndiye kiongozi mpole na mwenye nguvu, ambaye Baraza la Makardinali wanajiaminisha kwake, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Maria.

Makardinali wapya limekuwa ni tukio la kiekumene.
Makardinali wapya limekuwa ni tukio la kiekumene.

Kardinali Robert Francois Prevost, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu kwa niaba ya Makardinali wapya amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwateuwa kuwa ni wahudumu wa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia kwa furaha Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwashirikisha katika dhamana ya kuliongoza Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa kujikita zaidi na zaidi katika fadhila ya unyenyekevu! Hii ni huduma na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hata ikibidi kuyamimina maisha yao “Usque ad effusionem sanguinis.” Kikao hiki cha Makardinali kinafanyika mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kusikilizana kama njia ya kuiishi imani sanjari na ukuaji wa kidugu kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wagonjwa na mazingira. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutembea kwa umoja na mshikamano, katika umoja na tofauti zao msingi, kila mwamini akiendelea kugundua ndani mwake wito wake, tayari kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni alama muhimu sana kwa kila mbatizwa, kujenga umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kutangaza, kuungama na kumwilisha imani katika matendo. Makardinali wapya, wamemwomba Baba Mtakatifu kuwakumbuka na kuwaombea ili, kuliwezesha Kanisa la Kiulimwengu, kuwa tayari kufungua malango yake kwa haraka, tayari kuwasikiliza watu wote wa Mungu.

Kipindi Maalum
30 September 2023, 13:39