Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na madhara makubwa yaliyosababishwa na majanga asilia nchini Slovenia na Georgia Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na madhara makubwa yaliyosababishwa na majanga asilia nchini Slovenia na Georgia   (BORUT ZIVULOVIC)

Papa Francisko Asikitishwa na Maafa Huko Slovenia na Georgia

Baba Mtakatifu amesikitishwa na madhara makubwa yaliyosababishwa na majanga asilia nchini Slovenia na Georgia na hivyo kupelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia na kwamba, anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anawashukuru watu wa kujitolea wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha na mli za watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 9 Agosti 2023 wakati wa Katekesi yake amejikita katika hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa nchini Ureno kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni iliyonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Baba Mtakatifu amesikitishwa na madhara makubwa yaliyosababishwa na majanga asili anchini Slovenia na Georgia na hivyo kupelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na majanga haya asilia na kwamba, anapenda kuwaonesha uwepo wake wa karibu. Anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kutoa msaada wao wa hali na mali kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu waliofikwa na majanga haya asilia.  Taarifa kutoka Slovenia zinasema kwamba, watu zaidi ya wanne wamepoteza maisha na kwamba, hasara iliyopatikana ni zaidi ya Euro milioni 500. Kwa upande wa Giorgia, watu waliopoteza maisha ni zaidi ya 16 na kwamba, watu wengine zaidi ya 200 wameokolewa na kupelekwa kwenye maeneo yenye usalama zaidi. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa mahujaji kutoka Malta, Nigeria, Tonga na Marekani.

Maafa makubwa yametokea nchini Slovenia
Maafa makubwa yametokea nchini Slovenia

Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, tarehe 9 Agosti 2023, Kanisa linaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, maarufu kama Edith Stein, Bikira na Shahidi; Msimamizi mwenza wa Bara la Ulaya. Shuhuda wa imani na mwanamke wa shoka, aliyejibidiisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika uaminifu na upendo. Ni shuhuda wa udugu kati ya Wayahudi na Wakristo na daraja makini la majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini hizi mbili. Baba Mtakatifu anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia maamuzi yake yanayofumbata ujasiri; yakamwilishwa katika wongofu kwa Kristo Yesu! Ni mfano bora wa kuigwa dhidi ya tabia na itikadi zinazopandikiza mbegu za chuki na uhasama kati ya watu. Baba Mtakatifu anamwomba, Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba, aliombee Bara la Ulaya ili lisikumbwe na ubaridi, Mwenyezi Mungu apewe sifa na mwanadamu na akombolewe! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni watu wa shukrani kwa wema na ukarimu wanaoupata kutoka kwa Mwenyezi Mungu pengine hata bila mastahili yao. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya ukaribu wa Mungu kwa watu wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha. Ushuhuda wa maisha yake usaidie kuchocheo majadiliano katika ukweli na uwazi; ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu dhidi ya mifumo yote ya ghasia na ubaguzi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru watu wa Mungu kutoka Poland waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao wakati wa hija yake ya kitume nchini Ureno.

Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba Utuombee
Mtakatifu Theresa Bernadetha wa Msalaba Utuombee

Kutoka katika sakafu ya moyo wake, Baba Mtakatifu anasema anatamani kuona amani ikitawala ulimwenguni. Kwa sasa kuna mahujaji wengi wanaokwenda kwenye Madhabahu ya Jasna Góra huko Częstochowa, nchini Poland kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho sehemu mbalimbali za dunia. Kati yao, wamo pia mahujaji kutoka nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anawataka mahujaji kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea hatima ya Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Ikumbukwe kwamba, Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao!

Papa Francisko anawashukuru watu wote wanaosali na kumwombea
Papa Francisko anawashukuru watu wote wanaosali na kumwombea

Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kuzidimisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!

Majanga asilia
09 August 2023, 14:33