Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Agosti 2023 alifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Agosti 2023 alifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Ufunguzi: Upendo na Ushuhuda wa Vijana

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Agosti 2023 alifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa kuwakaribisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kuwakumbusha kwamba, kila mmoja wao anaitwa kwa jina ili kusherehekea upendo wa Mungu katika maisha yao; Mwenyezi Mungu anawafahamu na kuwapenda jinsi walivyo na kwamba, Kristo Yesu anawathamini na kuwatumainia. Vijana wajikite katika elimu na masomo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 Agosti 2023 anashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Agosti 2023 alifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa kuwakaribisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kuwakumbusha kwamba, kila mmoja wao anaitwa kwa jina ili kusherehekea upendo wa Mungu katika maisha yao; Mwenyezi Mungu anawafahamu na kuwapenda jinsi walivyo na kwamba, Kristo Yesu anawathamini na kuwatumainia. Kanisa ni Jumuiya ya watu walioitwa na kwamba, ndani ya Kanisa kuna nafasi kwa kila mtu, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya ni kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mwaliko huu unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa vijana wa kizazi kipya katika kutenda mema, kwa kuonesha huruma na upendo kwa jirani, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya wengine. Kama vile Kristo Yesu alivyowatuma wafuasi wake sabini na wawili, wakiwa kama kondoo kati ya mbwa mwitu, lakini Kristo Yesu amewaandalia furaha isiyokuwa na kifani, kwani kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko karibu sana na wao kama vijana watambue kwamba, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Rej. Lk 10:9.

Papa Francisko anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa upendo
Papa Francisko anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa upendo

Jambo la msingi kwa vijana ni kuhakikisha kwamba, wako tayari na kwa njia yao ataweza kutenda miujiza kama alivyofanya alipomwita Abrahamu, Baba wa imani, Musa mtumishi wake mwaminifu, Mtakatifu Petro hata katika ukuu na udhaifu wake na Mtakatifu Paulo Mtume, na Mwalimu wa Mataifa aliyelidhulumu Kanisa; wote hawa wakaunganika na wito wa Mungu na hatimaye, wakawa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Bikira Maria aliyejifunua na kujiachilia mbele ya Mwenyezi Mungu na hivyo akabarikiwa kuwa ni chombo cha furaha na matumaini. Kwa walimwengu. Vijana watambue kwamba, wanaitwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu anawapenda upeo, changamoto kubwa mbele ya vijana ni kuitana kwa majina. Pili wajitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya wokovu wa walimwengu. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujishikamanisha na Kristo Yesu, ili upendo na furaha yao iweze kuongezeka maradufu!

Vijana wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Vijana wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurrentes" ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 13 Agosti 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina na hatimaye kuzinduliwa rasmi 9 Juni 2017. Kwa sasa Taasisi hii inapania pamoja na mambo mengine: kuendelea kuwa ni mahali pa kuwafunda vijana kutambua na kushuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Kukuza elimu fungamani na angavu, ili kudumisha makuzi na malezi bora kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kujenga na kudumisha madaraja na utamaduni wa watu kukutana. Hii ni fursa ya kuthamini na kuheshimu tofauti zao msingi pamoja na kila mtu kuendeleza utambulisho wake. Taasisi hii inaendelea kukua na kupanuka kiasi cha kuanza kujitambulisha kuwa ni Jumuiya ya urafiki wa udugu wa kibinadamu unaowaunganisha wanafunzi kutoka katika shule na taasisi za elimu 4,000 katika nchi 190. Ni taasisi ambayo inasikiliza na kujibu sauti na kilio cha vijana wa kizazi kipya. Inataka kuwajengea uwezo kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo na hatimaye, kuwawezesha pia kusherehekea Injili ya uhai. Huu ndio utamaduni mpya unaounganisha: kichwa, moyo na mikono. Taasisi hii imejenga utamaduni wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kukutana na kusakata rumba kwa pamoja, matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu!

Papa awataka vijana kujikita katika elimu na masomo
Papa awataka vijana kujikita katika elimu na masomo

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 3 Agosti 2023 katika hija yake ya Kitume nchini Ureno amegusia kuhusu: Matatizo, changamoto na matumaini ya vijana wa kizazi kipya. Amekazia umuhimu wa elimu na masomo ili kujenga ulimwengu ulio bora zaidi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa upande wa vijana kutoka nchini Kenya, wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kukutana na vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, ili kuadhimisha Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Mwaliko kwa vijana kutoka nchini Kenya ni kwamba, vijana wanatakiwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano; wawe ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kwa hakika, vijana wamefurahi kukutana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko huko Lisbon nchini Ureno. Hii imekuwa ni kwa vijana kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Ujumbe mahususi kwa vijana ni upendo na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani. Vijana watambue kwamba wanalo jukumu zito la kulinda, kutunza na kudumisha amani na wakati wao ndio huu. Vijana wanahimizwa kujihusisha na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Shukrani zangu za dhati zinamwendea Padre Bernardo Suate anayeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya 37 a Vijana Ulimwenguni kwa mahojiano haya.

Vijana Makaribisho
04 August 2023, 13:48