Tafuta

Ujumbe wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Akili Bandia na Amani.” Ujumbe wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Akili Bandia na Amani.”   (REUTERS)

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani 2024: Akili Bandia na Amani

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2024 unogeshwe na kauli mbiu “Akili Bandia na Amani.” Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine anakazia umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yawe ni kwa ajili ya huduma, ustawi maendeleo na mafao ya wengi, utunzaji bora wa mazingira, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ukuzaji na uendelezaji wa amani ulimwenguni ni sehemu muhimu ya ujumbe wa Kanisa wa kuendeleza kazi ya ukombozi hapa duniani. Kwa kweli, Kanisa katika Kristo ni Sakramenti au alama na chombo cha amani ambacho kipo hapa ulimwenguni kwa ajili ya ulimwengu. Ukuzaji wa amani ya kweli ni dalili ya imani ya Kikristo katika yale mapendo ambayo Mungu anayo kwa kila binadamu. Kutoka imani ya ukombozi katika mapendo ya Mungu, dunia inajitokeza kwa mwonekano mpya na inajitokeza pia njia mpya ya kuwasogelea wengine bila kujali iwapo hao wengine ni mtu mmoja mmoja au watu wengi kwa pamoja. Hii ni imani inayobadilisha na kuyafanya maisha yaonekane mapya baada ya kupata msukumo wa amani ambayo Kristo aliwaachia wafuasi wake (taz. Yn 14: 27). Baada ya kuguswa na imani hii, Kanisa linakusudia kukuza umoja wa Wakristo na ushirikiano mzuri kati ya waamini wa dini zingine. Tofauti ya dini kamwe isiwe sababu ya migogoro. Ule utafutaji wa amani kwa pamoja kwa upande wa waamini ni chanzo muhimu cha umoja wa watu. Kanisa linawasihi watu binafsi mmoja mmoja, watu wote kwa jumla, Madola na Mataifa kuwa pamoja katika kuimarisha amani ikiweka msisitizo wa pekee wa nafasi muhimu ya sheria ya Kimataifa. Kanisa hufundisha kwamba amani ya kweli hupatikana kwa njia ya kusamehe na kwa upatanisho. Si rahisi kwa mtu kusamehe, pale anapokabiliwa na matatizo makubwa yanayotokana na mapambano ya vita kwa kuwa vurugu kama hizo hasa “zinapokuwa zimekithiri na kuonesha ukali mkubwa wa mateso ya hali ya juu zinamwachia mtu maumivu makali. Mateso haya yanaweza kupozwa tu kwa pande zote husika kufikiria kwa dhati na kwa kina njia zinazoweza kuyaondoa matatizo yaliyopo na kuwa na msimamo madhubuti na wa ujasiri wa kujutia yale yaliyopita. Uzito wa hayo yaliyopita ambayo hayawezi kusamehewa unaweza kupokelewa tu pale msamaha wa pande zote mbili unapotolewa na kupokelewa.

Kauli mbiu: Akili Bandia na Amani 2024
Kauli mbiu: Akili Bandia na Amani 2024

Huu ni mchakato mrefu na mgumu, lakini hata hivyo si kitu ambacho hakiwezi kupatikana. Tendo la pande mbili zisizoelewana kusameheana lisiondoe haja ya kutafuta haki na wala lisizibe njia inayoelekea kwenye ukweli. Kwa kweli, huu ni muda mzuri na unaofaa ambao unaweza kutumiwa na vyanzo, vyenye nia ya kuanzisha vyombo vya Kimataifa vya kisheria. Kwa mujibu wa kanuni ya mamlaka ya kisheria ya kiulimwengu ikiongozwa na utaratibu wa kiutendaji ambao unaheshimu haki za mshtakiwa na za wahanga, vyombo hivyo vya sheria vinaweza kuuyakinisha na kuubainisha ukweli wa uhalifu uliotendeka wakati wa mapambano ya kivita. Hata hivyo, ili mahusiano yaweze kuimarika kiasi cha kuyafanya mawazo ya upande mmoja yakubaliwe na upande wa pili kwa nia ya kuwa na upatanisho, ni lazima kudadisi na kupata taarifa zaidi ya ile taarifa ya tabia tu ya kiuhalifu ya kutenda na kutotenda kosa na utaratibu wa ulipaji wa fidia. Ni lazima, hata hivyo, kukuza na kuendeleza heshima ya kuwa na haki kwa masuala ya amani. Haki hii inafanya kuwe na matumaini ya ujenzi wa jamii ambamo kuna miundo ya ushirikiano badala ya ile miundo ya matumizi ya mabavu kwa madhumuni ya kufikia yale ambayo ni ya manufaa kwa wote. Kanisa hutumia sala katika harakati zake za kutafuta amani. Sala huufungua moyo na kuuweka wazi, si tu kwa uhusiano wake wa karibu na Mungu, bali pia kwa uhusiano na wengine wenye heshima, uelewa, taadhima na mapenzi mema.

Siku ya 57 ya Kuombea Amani Ulimwenguni
Siku ya 57 ya Kuombea Amani Ulimwenguni

Sala inaongeza ujasiri na inatoa msaada kwa “wote ambao ni marafiki wa amani, na pia wale wapendao amani na wanaojitahidi kuikuza amani hiyo katika mazingira yao wanamoishi. Sala ya Liturujia ni “kilele ambako tendo la Kanisa huelekea na hapohapo ni chanzo na asili ya nguvu zake. Kwa namna ya pekee adhimisho la Ekaristi, “chanzo na kilele cha maisha ya Kikristo,” ni chemchemi ya uwajibikaji wa kweli wa Kikristo kwa ajili ya amani. Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1968 alianzisha Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Ulimwenguni, ili kukuza na kudumisha amani sanjari na ujenzi wa amani, hasa mwanzoni mwa mwaka, ili walimwengu waweze kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa amani. Hii ni sehemu muhimu sana ya mwendelezo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Amani hujieleza yenyewe kwa njia ya amani tu, na haiwezi kamwe kutenganishwa na madai ya haki. Amani hii inakuzwa na kuendelezwa kwa kujitoa sadaka, upole, huruma na mapendo ya kila mtu. Rej. Mafundisho Jamii ya Kanisa 516-450. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, Ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi Januari 2024 unogeshwe na kauli mbiu “Akili Bandia na Amani.” Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine anakazia umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi yawe ni kwa ajili ya huduma, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia isaidie kukuza na kudumisha huduma ya haki na amani duniani. Inapendeza kuona kwamba, mkataba huu, unawashirikisha pia viongozi wa kidini, waamini na watu wenye mapenzi mema, kielelezo makini cha mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na wahitaji zaidi, huku haki msingi za binadamu zikipewa msukumo wa kwanza. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo msingi ya kuzingatia ni kanuni maadili, elimu na haki msingi za binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasaidie kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani duniani.

Amani Duniani 2024
10 August 2023, 15:40