Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kitendo cha mtu mmoja tarehe 28 Juni 2023 kuchoma baadhi ya kurasa za Quran Tukufu. Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kitendo cha mtu mmoja tarehe 28 Juni 2023 kuchoma baadhi ya kurasa za Quran Tukufu.  (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Kuhuzunishwa na Kitendo cha Kuchoma Quran Tukufu

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kitendo cha mtu mmoja tarehe 28 Juni 2023 kuchoma baadhi ya kurasa za Quran Tukufu kwenye mlango wa msikiti mkuu huko Stockholm nchini Sweden. Kamwe uhuru wa kidini usitumike vibaya kwa ajili ya kudhalilisha watu wengine ndani ya jamii, vitendo vya namna hii vinapaswa kukemewa na kulaaniwa na wapenda amani duniani. Kitendo hiki kinachoonesha chuki za kidini kimelaaniwa na kushutumiwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1.

Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.
Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.

Ni katika muktadha huu wa uhuru wa dini, Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kitendo cha mtu mmoja tarehe 28 Juni 2023 kuchoma baadhi ya kurasa za Quran Tukufu kwenye mlango wa msikiti mkuu huko Stockholm nchini Sweden. Kamwe uhuru wa kidini usitumike vibaya kwa ajili ya kudhalilisha watu wengine ndani ya jamii, vitendo vya namna hii vinapaswa kukemewa na kulaaniwa na wapenda amani duniani. Kitendo hiki kinachoonesha chuki za kidini kimelaaniwa na kushutumiwa na nchi mbalimbali duniani. Hii ni sehemu ya mahojiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Bwana Hamad Al-Kaabi, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Al-Ittihad linalochapishwa kila siku kwenye Falme za Kiarabu. Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu hali yake ya afya inayoendelea kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa hivi karibuni. Anawashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia wakati alipokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Anawashukuru na kuendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake, bila kuwasahau watu wote wenye mapenzi mema waliomwandikia ujumbe wa matashi mema na kusali kwa ajili yake.

Papa anawashukuru wote waliosali na kumwandikia ujumbe
Papa anawashukuru wote waliosali na kumwandikia ujumbe

Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 3 hadi 5 Februari 2019, aliadhimisha hija ya kitume ya ishirini na saba huko Abu Dhabi, kwenye Falme za Kiarabu, ili kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa majadiliano ya kidini ulionogeshwa na kauli mbiu "Udugu wa kibinadamu.” Anamshukuru na kumpongeza Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan kwa jitihada zake za makusudi anazoendelea kutekeleza kwa ajili ya kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, haki na amani duniani na kwamba, vijana wanapaswa kusaidiwa ili wasitumbukie katika makucha ya watu wanaoweza kuwavuruga na hatimaye, jamii ikatumbukia katika machafuko. Vijana walindwe dhidi ujumbe wa chuki na uhasama; ulaji wa kupindukia pamoja na maamuzi mbele. Vijana wajengewe uwezo wa kuratibu uhuru wao kibinadamu, kwa kufanya mang’amuzi na hatimaye, kuwajibika. Uhuru ni muhimu sana kwa sababu ni jambo linalomtofautisha mtu na mtu; uhuru wa mawazo ukuzwe kwani ni sehemu muhimu sana ya ukuaji na ukomavu wa mtu. Vijana wasifanyiwe mzaha na kuonekana kana kwamba hawana uwezo wa kufikiri na hatimaye, kufanya maamuzi. Wanatakiwa kufundwa ili kumwilisha ndani mwao ile kanuni ya dhahabu, hii ni sheria inayo mtaka mtu amtendee mwingine kama yeye ambavyo angependa kutendewa!

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Abu Dhabi 3-5 Feb. 2019
Hija ya Kitume ya Papa Francisko Abu Dhabi 3-5 Feb. 2019

Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu walitia mkwaju kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema majadiliano ya kidini si alama ya udhaifu, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Majadiliano ya kidini hayana mbadala, kwani waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano na Bwana Hamad Al-Kaabi, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Al-Ittihad anasema, wageni na watu mashuhuri wanapomtembelea mjini Vatican kati ya zawadi kubwa anazowapatia ni “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni hati muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini; haki, amani na maridhiano; ushirikiano na mafungamano ya kijamii yanayosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa sababu ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo ambayo hayapaswi kuwa na mipaka wala ubaguzi. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, vitendo vya kigaidi, uhamiaji wa shuruti, biashara ya binadamu na viungo vyake; sera za utoaji mimba na kifo laini ni vitendo vinavyotishia Injili ya uhai. Jumba la Familia ya Abraham, “Berit Abrahamu” ambalo linajumuisha: Sinagogi, Kanisa na Msikiti katika jengo moja, ambalo lilizinduliwa mwaka 2022 kama kielelzo cha utekelezaji wa “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Na kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kuhakikisha kwamba, matamko, sera na mipango mbalimbali inamwilishwa katika matendo, kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Papa Mahojiano
04 July 2023, 15:26