Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Julai mwaka 2023 anasali kwamba, wakatoliki waweze kulifanya adhimisho la Ekatisti Takatifu kuwa ni kitovu cha maisha yao Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Julai mwaka 2023 anasali kwamba, wakatoliki waweze kulifanya adhimisho la Ekatisti Takatifu kuwa ni kitovu cha maisha yao  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Julai 2023: Ekaristi Takataifu Iwe Kitovu cha Maisha ya Wakatoliki

Katika nia zake za jumla kwa mwezi Julai mwaka 2023 Papa anasali kwamba, wakatoliki waweze kulifanya adhimisho la Ekatisti Takatifu kuwa ni kitovu cha maisha yao; Ekaristi inabadilisha mahusiano ya kibinadamu kwa kina na kufungua njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na ndugu zao! Huu ni mwaliko wa kumwabudu Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu ya Pasaka ya Kristo, ni utekelezaji wa matoleo minthili ya Sakramenti ya Sadaka yake moja, katika Liturujia ya Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wake. Ni kumbukumbu endelevu inayotangaza maajabu yaliyotendwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu wake “fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.” Ni ukumbusho wa Pasaka, mwenyezi Mungu alipowakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri. Katika Agano Jipya, kumbukumbu hii hupata maana mpya. Mama Kanisa anapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu anafanya ukumbusho wa Pasaka ya Kristo Yesu, aliyejisadaka mara moja tu Msalabani na kila mara Fumbo hili linapoadhimishwa, kazi ya ukombozi inaendelea kutekelezwa. Ekaristi Takatifu inafumbata maneno na matendo ya Kristo Yesu; inawaonjesha waamini Fumbo la Pasaka, yaani mateso yake na Roho wake. Waamini wanapompokea kwa imani na uchaji wanakuwa na uhakika kwamba, wanapendwa na Kristo Yesu. Ekaristi Takatifu inawaundia waamini kumbukumbu ya shukrani, kwani wanajitambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Baba wa milele! Hii ni kumbukumbu huru kabisa, kwani upendo na msamaha wa Kristo Yesu unaganga na kuponya madonda na majeraha ya zamani na hivyo kuleta amani moyoni mwa waamini.

Ni matumaini ya Papa Francisko: Ekaristi Kiini cha Maisha ya Wakatoliki.
Ni matumaini ya Papa Francisko: Ekaristi Kiini cha Maisha ya Wakatoliki.

Hii ni kumbukumbu yenye uvumilivu kwani hata katika magumu ya maisha, bado waamini wanatambua kwamba, Roho wa Kristo Yesu yuko ndani mwao. Ekaristi Takatifu inawatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu kwani hata katika safari ambayo ni ngumu kiasi gani, waamini wanatambua kwamba, hawako pweke, na kamwe Kristo Yesu hawezi kuwageuzia kisogo na kwamba, kila wakati wanapomwendea anawapatia nguvu mpya kwa njia ya upendo wake. Ekaristi Takatifu inawakumbusha waamini kwamba, hawapo peke peke, bali ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na familia ya Mungu kama ilivyojionesha kwenye Agano la Kale ilipokusanyika kwa ajili kuokota manna iliyoshuka kutoka mbinguni. Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, anawaalika waamini kumpokea kwa pamoja na kumshiriki kati yao. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa ushirika unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano wa waamini.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa

Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbukumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa ushirika wa kweli. Kwa maisha ya Ekaristi Tatakatifu, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Julai mwaka 2023 anasali kwamba, wakatoliki waweze kulifanya adhimisho la Ekatisti Takatifu kuwa ni kitovu cha maisha yao; Ekaristi ambayo inabadilisha mahusiano ya kibinadamu kwa kina na kufungua njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na ndugu zao! Huu ni mwaliko wa kumwabudu Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Waamini wanaposhiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anakuja kwa waja wake na kuwaimarisha katika upendo, kama alivyopenda mwenyewe! Anawakirimia waamini ujasiri wa kukutana na jirani zao, ili kutoka katika ubinafsi na uchoyo wao, tayari kuwaendea na kushikamana na wengine katika huduma ya upendo. Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu Kristo Yesu anajisadaka mwenyewe ili aweze kuwa ni chakula na kinywaji cha waja wake. Na kwa kulishwa Mwili wake Mtakatifu, waamini wanapaswa kujisadaka na kujimega kama Ekaristi Takatifu kwa jirani zao. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni muda muafaka wa kukutana na Kristo Yesu, tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kama Kristo Yesu alivyofundisha kupenda.

Papa Nia Julai

 

 

04 July 2023, 16:28