Tafuta

28 Julai 1993, Makanisa mawili ya Jimbo kuu la Roma yaani Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran na Kanisa la “San Giorgio huko Velabro”  yaliposhambuliwa na Kikosi cha Kigaidi cha Mafia, "Cosa Nostra" 28 Julai 1993, Makanisa mawili ya Jimbo kuu la Roma yaani Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran na Kanisa la “San Giorgio huko Velabro” yaliposhambuliwa na Kikosi cha Kigaidi cha Mafia, "Cosa Nostra"  (ANSA)

Kumbukizi ya Miaka 30 ya Ulipuaji wa Makanisa Jimbo kuu la Roma: 1993-2023

Ilikuwa ni usiku wa tarehe 27 Julai kuamkia tarehe 28 Julai 1993, Makanisa mawili ya Jimbo kuu la Roma yaani Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran na Kanisa la “San Giorgio huko Velabro” yaliposhambuliwa na Kikosi cha Kigaidi cha Mafia, maarufu kama “Cosa Nostra.” Jumla ya watu ishirini na wawili walijeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi haya ya kigaidi. Papa Francisko anawataka watu wa Mungu kusimama kidete kulinda ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni usiku wa tarehe 27 Julai kuamkia tarehe 28 Julai 1993, Makanisa mawili ya Jimbo kuu la Roma yaani Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran na Kanisa la “San Giorgio huko Velabro”  yaliposhambuliwa na Kikosi cha Kigaidi cha Mafia, maarufu kama “Cosa Nostra.” Jumla ya watu ishirini na wawili walijeruhiwa vibaya kutokana na mashambulizi haya ya kigaidi. Ni katika muktadha huu, waamini wa Jimbo kuu la Roma wakiwa wameungana na viongozi wa Serikali, wamefanya maandamano ya amani, huku wakiwa na mienge mikononi mwao, kama alama ya kumbukizi ya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma na“San Giorgio huko Velabro.” Washiriki wa maandamano haya wamewakumbuka na kuwaombea wahanga wa mashambulizi haya ya kigaidi, miaka thelathini iliyopita! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake uliosomwa kwa niaba yake na Askofu Baldassare Reina, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anelezea kuhusu ushiriki wake kwenye maandamano haya, watu waliosadaka maisha yao kulinda tunu msingi za kijamii zinazosimikwa katika demokrasia, haki na uhuru; na kwamba, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, tayari kujenga ubinadamu mpya.

Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wakiandama kumbukumbu ya miaka 30
Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma wakiandama kumbukumbu ya miaka 30

Baba Mtakatifu anasema, mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Makanisa yalisababisha mahangaiko makubwa kwa waamini na hasa wanaotoka Jimbo kuu la Roma, kwa vitendo hivi vya kigaidi vinavyoendelea kuitikisa Italia inayozidi kupekenywa kutokana na umaskini wa hali na kipato. Kumbukumbu hii ni mwaliko kwa wananchi wote wa Italia kila mtu kadiri ya nafasi na wajibu wake kutekeleza dhamana hii, wakati mwingine hata kwa kuhatarisha maisha. Hii ndiyo sadaka na majitoleo ya wale walioamini na kusadaka maisha yao kwa ajili ya kulinda na kutetea tunu msingi za kijamii zinazosimikwa katika demokrasia, haki na uhuru kamili. Huu ni mwaliko wa nguvu katika dhamiri ya watu wa Mungu nchini Italia, huku wakisukumwa na dhamiri nyofu kuwajibika katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni mpya wa upendo. Baba Mtakatifu amekazia kwa mara nyingine tena maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwamba, watu wa Mungu wanatamani maelewano na amani sanjari na kujitahidi kujenga utamaduni wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko analaani mifumo yote inayopingana na sheria ambayo kwa bahati mbaya bado inaendelea kuwatesa watu wa Mungu hata katika ulimwengu mamboleo. Hii ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na hasa zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Papa Francisko anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa matumaini
Papa Francisko anawataka vijana kuwa ni mashuhuda wa matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini; wawe na ujasiri bila kupepesa pepesa macho dhidi ya vikosi cha ugaidi. Vitendo vya kigaidi vinazamisha mizizi yake mahali penye woga na wasi wasi, kiasi hata cha kutawala akili na nyoyo za watu. Baba Mtakatifu anawataka wale wote walioshiriki katika maandamano haya kati kati ya usiku wa manane, wawe ni chachu ya kuleta mabadiliko na mashuhuda wa: uhuru na haki. Anawaalika viongozi wa Serikali na Kanisa kushirikiana kwa karibu ili kujenga na kudumisha ubinadamu mpya. Wawe watumishi waaminifu wa watu wa Mungu, kwa njia ya wema, huruma na upole na hasa zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, siku ya mwisho watu watahukumiwa kadiri ya matendo yao. Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Rej. Mt 25:31-46. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka waandamanaji wote hawa usiku huu wa manane chini ya ulinzi na tunza ya Watakatifu Petro na Paulo, walinzi na waombezi wa Mji wa Roma pamoja na kuwazamisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.”

Vitendo vya Kigaidi

 

28 July 2023, 14:15