Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Unabii Unasimikwa Katika Utangazaji na Ushuhuda Amini

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa bahati mbaya sana baadhi ya waamini wanauelewa potofu kuhusu “Nabii”. Kuna baadhi ya watu wanamwona kuwa kama mganga wa kienyeji na mpiga ramli dhana ìinayowatumbukiza wengi katika usomaji wa nyota na ushirikina. Wegine wanamwona Nabii kama mjumbe wa Agano la Kale aliyetabiri ujio wa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Nabii ni Mtumishi na Mjumbe wa Mungu na ni mlinzi katika jamii anamoishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utume wa kinabii ni chombo cha utafutaji wa haki, amani na maridhiano ulimwenguni. Kila mbatizwa anashiriki katika kazi tatu za Kristo Yesu, yaani Ufalme, Ukuhani na Unabii; Kama unavyotukumbusha Waraka wa kwanza wa Mtume Petro, “bali ninyi ni uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhila zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (I Petro 2,9). Nabii ni mjumbe wa Neno la Mungu kwa wanadamu. Neno ambalo, kama anavyofafanua Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika barua yake ya Kitume “Verbum Domini” (Neno la Bwana), ya kuwa ni Neno la upatanisho, maana ni katika Neno hilo, Mwenyezi Mungu amevipatanisha vitu vyote naye. Nabii ana wajibu wa kuhakikisha kuwa ujumbe huo unamfikia mlengwa ili apate kuokolewa. Asipotimiza wajibu huo lawama ni juu yake yeye kwa kutomsaidia mhusika aweze kutubu na kumwongokea Mungu. Wakati wote nabii ananena kwa jina la Bwana, kile ambacho Bwana mwenyewe amependa kuwaarifu waja wake. Kristo, Bwana wa haki na amani, ndiye mtawala mkuu na wa pekee wa ulimwengu wote. Naye anautaka ulimwengu huu uwe umejaa amani, haki na mapendo. Kama mtumishi wa Bwana Nabii anaufikisha ujumbe aliokabidhiwa jinsi ulivyo. Yeye hahubiri mambo yake binafsi, bali anapeleka ujumbe wa Mwenyezi Mungu, mwaliko wa kuishi fadhila ya imani yao katika utafutaji wa haki, amani na maridhiano. Mkristo kwa Sakramenti ya ubatizo ametiwa mafuta na kuwekwa wakfu kuwa mwinjili, kuwa mtumishi wa Neno la Mungu. Hivi anaitwa kuwa mwaminifu katika utume wake, bila kuona aibu, bila kukata tamaa wala kueneza mambo yake na vionjo vyake binafsi. Mkristo mwaminifu anaipeleka Injili ya Kristo, Injili ya haki, amani na maridhiano kila mahali na kila wakati.

Nabii ni mjumbe wa Mungu anayesimamia haki na amani
Nabii ni mjumbe wa Mungu anayesimamia haki na amani

Ni mtumishi anayesimamia amani na haki za watu wa Mungu katika ujumla wao kwa njia halali, hata ikimlazimu kuutoa uhai wake kwa ajili ya utumishi wake huo mwaminifu. Waamini wakristo katika kuishi uaminifu wa utume wao wa kinabii wanaalikwa kuwa ni wapole, welevu, wanyenyekevu, watiifu, wavumilivu, wanaoishi katika matumani na katika mapendo. Nabii ni mtu wa Mungu kwa kuwa ana mahusiano ya karibu sana na Mwenyezi Mungu katika mwenendo wake na maisha kwa ujumla. Ili kuudumisha uhusiano huo, Nabii anakuwa ni mtu wa sala ya kweli na ya rohoni. Ni kwa mahusiano hayo, Nabii anakuwa na namna ya kufikiri kulingana na mwenendo wa kimungu. Mahusiano kati ya Nabii na Mwenyezi Mungu yanaugusa ubinadamu wake, namna yake ya kuishi, namna yake ya kuongea, namna yake ya kutenda na namna yake ya kuona mambo. Kumbe basi, Mungu anaingia katika maisha ya nabii na kumbadili kwa undani kabisa katika maisha yake. Kwa sababu hiyo, anaumwilisha ujumbe anaopewa na Mwenyezi Mungu na unakuwa sehemu ya maisha yake. Matokeo yake ni kwamba, maisha yake Nabii mwenyewe yanakuwa ushuhuda na ishara ya ujumbe wa Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anafundisha kuwa tafsiri ya kina ya Maandiko Matakatifu inapatikana kutoka kwa wale wanaoruhusu kuongolewa na kuumbwa upya na Neno la Mungu kwa kulisikiliza, kulisoma na kulitafakari kwa undani na kwa imani. Nabii anawekwa na Mwenyezi Mungu kuwa mlinzi katika jamii anamoishi, kuwa mlinzi wa familia ya Mungu katika ujumla wake. Katika huduma hii ya ulinzi, Nabii anakuwa macho ya jumuiya husika. Waamini wabatizwa wote wana wajibu wa kuendelea kuwa walinzi katika jumuiya wanamoishi. Wanapaswa kuyafumbua maovu yanayoikabili jamii na yanayofanya wanyonge waendelee kuteseka, na wengi wao kunyimwa mahitaji na haki zao msingi. Anapoyafunua mabaya ndani ya jamii ili kuyatafutia tiba muafaka, Nabii mwenyewe anapaswa kuwa wa kwanza kuachana na uovu huo na hivi kuimwilisha haki na amani, na kuwa mpatanishi, kwani Bwana asema “heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5,9). Ili kufanikisha utume huu Nabii anapaswa kuwa mtu wa karibu sana na familia ya Mungu katika jumuiya anamoishi.

Nabii anapaswa kuwa ni mtu wa sala
Nabii anapaswa kuwa ni mtu wa sala

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 2 Julai 2023 amejikita katika Unabii na kwamba, Kristo Yesu anasema, “Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.” Mt 10:41. Kwa bahati mbaya sana baadhi ya waamini wanauelewa potofu kuhusu “Nabii”. Kuna baadhi ya watu wanamwona kuwa kama mganga wa kienyeji na mpiga ramli dhana ìnayowatumbukiza wengi katika usomaji wa nyota na ushirikina. Wegine wanamwona Nabii kama mjumbe wa Agano la Kale aliyetabiri ujio wa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Lakini hata Kristo Yesu katika Injili ya Dominika ya 13 ya Mwaka A wa Kanisa anazungumzia kuhusu Nabii. Mababa wa Kanisa wanasema, wabatizwa wamekuwa mawe hai kwa ajili ya kujenga nyumba ya kiroho, kuwa ukuhani mtakatifu. Kwa njia ya Ubatizo wabatizwa hushiriki ukuhani wa Kristo, utume wake wa kinabii na wa kifalme. Ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzingatangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. Rej. KKK, 1268. Nabii kwa nguvu ya Sakramenti ya Ubatizo anawasaidia wengine kusoma yaliyopo kwa mwanga wa Roho Mtakatifu; anawasaidia jirani zake kutambua mpango wa Mungu na kuuishi. Nabii ni yule anayewaonesha wengine uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja nao kwa njia ya ushuhuda unaomsaidia kuishi vyema leo yake na kujenga kesho kadiri ya mpango wa Mungu. Kumbe, wabatizwa wote ni manabii na mashuhuda wa Kristo Yesu ili nguvu ya Injili ing’ae katika maisha ya kila siku, ya kifamilia na ya kijamii. Rej. LG. 35.

Wabatizwa wote wanahisiri kazi ya ukuahani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu
Wabatizwa wote wanahisiri kazi ya ukuahani, ufalme na unabii wa Kristo Yesu

Nabii ni alama wazi inayomwonesha na kumtambulisha Mungu pamoja na kumuakisi Kristo Yesu katika njia ya waamini. Kumbe, huu ni wajibu wa waamini kujiuliza ikiwa kama kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wamechaguliwa kuwa Manabii, wanazungumza kinabii na kumshuhudia Kristo Yesu, huku wakionesha mwanga wa maisha kati ya watu wanaokutana nao? Ni wakati wa kujiuliza kuhusu ushuhuda na unabii wao. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kuwapokea Manabii, kwani ni wajumbe wa Neno la Mungu kila mtu kadiri ya wito na dhamana yake katika medani mbalimbali za maisha. Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu amegawa karama na mapaji yake ya kinabii kwa watu watakatifu wa Mungu, kumbe kuna umuhimu wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kusali kwa ajili ya kumwomba Roho Mtakatifu; kusikilizana, kujadiliana kwa kuaminiana, kwani hata mdogo kuliko wote anaweza kuwa na jambo la kushirikisha. Ni katika muktadha huu, kunajengeka mazingira ya kumsikiliza Mwenyezi Mungu sanjari na kusikilizana wao kwa wao, wanakubalika na kupokelewa kama zawadi ya jinsi walivyo. Kimsingi utamaduni wa kusikilizana ungekuwa ni tiba muafaka kwa kinzani na migogoro inayoibuka kila kukicha. Huu ni mwaliko kwa waamini kupokeana kama kielelezo cha unabii, kwa kuheshimiana na kusikilizana, tayari kujiweka katika mazingira ya kujifunza kutoka kwa wengine.

Papa Nabii
02 July 2023, 14:38

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >