Tafuta

Umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; uhaba wa maji safi na salama; huduma bora za elimu, afya pamoja na makazi bora ni kati ya mambo yanayosugina utu na heshima ya binadamu. Umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; uhaba wa maji safi na salama; huduma bora za elimu, afya pamoja na makazi bora ni kati ya mambo yanayosugina utu na heshima ya binadamu.  (ANSA)

Baa la Njaa Duniani Linasigina Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu

Baa la njaa linazidi kuongezeka kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau majanga asilia. Na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; uhaba wa maji safi na salama; huduma bora za elimu, afya pamoja na makazi bora ni kati ya mambo yanayosigina utu na heshima ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kikao cha 43 cha Mkutano wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO kimefunguliwa rasmi tarehe 1 Julai na kinatarajiwa kukamilika tarehe 7 Julai 2023. Katika mkutano huu mkuu, wajumbe wa FAO wamemchagua tena Dr. QU Dongyu kuiongoza FAO kuanzia tarehe 1 Agosti 2023 hadi tarehe 31 Julai 2027, hii ikiwa ni awamu yake ya pili  katika uongozi wa FAO. Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza Dr. QU Dongyu alichaguliwa kuiongoza FAO Juni, 2019. Tangu wakati huo amefanya mageuzi makubwa kwa FAO, ikiwa ni pamoja na Mtandao wa Chakula Duniani, “World Food Forum” unaoongozwa na vijana wa kizazi kipya, ili kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo. Huu ni mkutano wa ngazi ya Mawaziri, ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili.  Hili ni Baraza kuu la uongozi wa FAO na huidhinisha: Mpango kazi na Bajeti ya Shirika kwa miaka miwili ijayo. Pia unatoa mapendekezo kuhusu masuala ya chakula na kilimo duniani na kukagua masuala ya sera ya utawala wa Kimataifa. Maji ni sehemu ya msingi ya mifumo ya chakula na kilimo lakini inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kila kukicha. Uhaba wa maji na ukame, mafuriko, na uchafuzi wa vyanzo vya maji vyote hivi vinadhoofisha juhudi za Kimataifa za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaani: Uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora na maisha bora, bila kumwacha mtu yoyote nyuma. Kuna zaidi ya watu bilioni tatu wanaoishi katika maeneo ya kilimo yenye viwango vya juu kabisa vya uhaba wa maji. Wakati ambapo takribani watu bilioni 1.2 wanaishi katika maeneno yenye ukame mkubwa.

Dr. Qu Dongyou Mkurugenzi mkuu wa FAO
Dr. Qu Dongyou Mkurugenzi mkuu wa FAO

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa FAO, anampongeza kwa kuchaguliwa tena kuiongoza FAO na kumtia shime aendeleze mapambano dhidi ya baa la njaa duniani linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baa la njaa linazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau majanga asilia. Na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; uhaba wa maji safi na salama; huduma bora za elimu, afya pamoja na makazi bora ni kati ya mambo yanayosigina utu na heshima ya binadamu. Lengo la Jumuiya ya Kimataifa la kutaka kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 pengine lisifikiwe kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwa sasa duniani. Kumekuwepo na matumizi makubwa ya rasilimali za dunia kupita kiasi; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa usawa kati ya watu. Mbinu mkakati wa uhakika wa usalama wa chakula duniani ulishafikiwa takribani miaka thelathini iliyopita, lakini athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto mpya zinazotishia uhakika na usalama wa chakula duniani.

Baa la njaa linasigina utu na heshima ya watu wengi duniani
Baa la njaa linasigina utu na heshima ya watu wengi duniani

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuangalia mahitaji msingi ya watu mahalia; kwa kuheshimu na kuzingatia tofauti zao msingi kitamaduni ili kuondokana na dhana ya ukoloni wa kiitikadi. Kumbe, sera na mikakati ya kutokomeza baa la njaa duniani lazima izingatie mahitaji ya watu na jumuiya zao na wala watu mahalia wasitwishwe sera na mikakati kutoka juu, ambayo mara nyingi ni kwa ajili ya faida ya watunga sera hizi. Changamoto kubwa ya kutokomeza baa la njaa duniani, itaweza kufanikiwa ikiwa kama Jumuiya yote ya Kimataifa itashiriki kikamilifu, sanjari na kuondokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kumbe, FAO pamoja na Mashirika yake yote ya Kimataifa yanaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kipaumbele cha kwanza, kikiwa ni maskini. Wadau mbalimbali hawana budi kuunganisha nguvu na rasilimali zao ili kupambana na baa la njaa duniani bila kumwacha mtu awaye yote nyumba. Vatican kwa upande wake, itaendelea kujizatiti kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku ikichota amana, utajiri, uzoefu na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika Kanisa Katoliki, ili duniani asiwe mtu anayekufa kwa baa la njaa; kwa kuendelea kulinda na kuhifadhi mazingira nyumba ya wote, ili dunia irejee tena kuwa ni bustani iliyotengenezwa kwa mikono ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya binadamu wote.

Papa Fao Kikao 43
04 July 2023, 16:03