Tafuta

Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández - kutoka nchini Argentina ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández - kutoka nchini Argentina ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. 

Askofu mkuu Víctor M. Fernández Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza sana Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Rais wa Tume ya Bibilia Kimataifa na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa kwa kuhitimisha utume wake katika maeneo hayo yaliyotajwa. Papa amemteua Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, wa Jimbo kuu La Plata nchini Argentina na anatarajia kuanza utume huu mpya kati kati ya Mwezi Septemba 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza sana Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Rais wa Tume ya Bibilia Kimataifa na Tume ya Kitaalimungu Kimataifa kwa kuhitimisha utume wake katika maeneo hayo yaliyotajwa. Baba Mtakatifu amemteua Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, wa Jimbo kuu La Plata nchini Argentina kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na anatarajia kuanza utume huu mpya kati kati ya Mwezi Septemba 2023. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, alizaliwa tarehe 18 Julai 1962 huko Alcira Gigena, nchini Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 15 Agosti 1986 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza kwa masomo ya juu na hatimaye akajipatia Shahada ya uzamili katika taalimungu huku akijikita katika Sayansi ya Biblia kutoka Chuo Kikuu cha Gregorian kilichoko mjini Roma na hatimaye, akahitimisha kwa kujipatia Shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Buenos Aires nchini Argentina. Tangu mwaka 1993 hadi mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Paroko, Muasisi wa Taasisi ya Majiundo ya waamini walei na Kituo cha Mafunzo ya Waalimu cha “Jesús Buen Pastor” huko Rio Cuarto, Cordoba. Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, amewahi kuwa Mlezi wa Seminari, na Mkurugenzi wa Majadiliano ya Kiekumene na Katekesi. Mwaka 2007 alishiriki katika Mkutano wa V wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, kama mwakilishi wa Mapadre kutoka Argentina na hatimaye, akateuliwa kuwa ni mjumbe wa kuhariri hati ya mwisho ya Mkutano wa CELAM wa mwaka 2007.

Papa Francisko akiwa na wajumbe wa CELAM
Papa Francisko akiwa na wajumbe wa CELAM

Kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2009 aliteuliwa kuwa ni Dekano wa Kitivo cha Taalimungu Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Cha Argentina na Rais wa Chama cha Wanataalimungu nchini Argentina. Kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2018 aliteuliwa kuwa ni Gambera wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Argentina. Tarehe 13 Mei 2013, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu. Ameshiriki Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2015. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina kunako mwaka 2007 likamchagua kuwa Rais wa Tume ya Imani na Tamaduni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina. Mwezi Juni 2018 akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la La Plata, nchini Argentina. Alikuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Mshauri wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na kwa sasa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu baada ya mageuzi yaliyofanywa na Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Ni mwandishi wa vitabu na makala zaidi 300; vitabu ambavyo vimetafsiriwa katika lugha mbalimbali, kielelezo makini cha msingi wa Kibibla katika maisha na utume wa Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Lengo mahususi la Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ni kulinda mafundisho ambayo yanatokana na imani ili kutoa sababu za tumaini la Kanisa, lakini sio kama adui anayepinga na kulaani, bali katika ukweli na uwazi, kwa kutenda kwa upole na heshima.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa
Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa

Hii ni sehemu ya barua kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliyomwandikia Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, anayemrithi Kadinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J. ambaye Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeka kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kwa kuzingatia kwamba kwa masuala ya kinidhamu - hasa yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo, hivi karibuni, Idara maalum imeundwa na hivyo kujengewa uwezo mkubwa wa kushughulikia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, jukumu lake kuu kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Knaisa ni kulinda imani, kutangaza na kuishuhudia kama sehemu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili mwanga wake uweze kuwa ni kigezo cha kuelewa maana ya uwepo haswa katika maswali yanayoletwa na maendeleo makubwa ya sayansi na jamii. Masuala haya yakikumbatiwa katika muktadha wa utangazaji na ushuhuda wa imani yanakuwa ni vyombo vya uinjilishaji kwa sababu yanaliwezesha Kanisa kuingia katika majadiliano na muktadha wa sasa katika kile ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linahitaji kukua katika tafsiri ya Neno la Mungu lililofuliwa na kueleweka katika ukweli huo, ili kuweza kuunganishwa na Roho Mtakatifu katika heshima na upendo, mambo yanayoliwezesha Kanisa kukua. Ukuaji huu wenye upatanifu utahifadhi fundisho la Kikristo kwa ufanisi zaidi kuliko utaratibu wowote wa udhibiti.

Papa Francisko amemshukuru Kardinali Ladaria
Papa Francisko amemshukuru Kardinali Ladaria

Mama Kanisa anaendelea kuthamini karama ya wanataalimungi na jitihada zao kwa ajili ya tafiti za Kitaalimungu, ili mradi tu, “hawaridhiki na taalimungu inayofanyika mezani na mantiki ya kutaka kutawala kila kitu. Ukweli ni bora kuliko wazo, kumbe, taalimungu inayotilia shaka uweza na ukuu wa Mungu na hasa huruma yake ni hatari sana. Kanisa linahitaji kutangaza na kushuhudia uwezo wa Mungu anayependa, anayesamehe, anayeganga, kuponya na kuwaweka waja wake huru, ili hatimaye, kukuza na kudumisha huduma ya udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anamwomba Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández kuhakikisha kwamba, Hati na Nyaraka mbalimbali za Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa zinakuwa ni msaada wa kutosha kitaalimungu, zinapatana na wingi wa Mafundisho ya kudumu ya Kanisa pamoja na kuzingatia Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” ya hivi karibuni. Mwishoni mwa barua hii, Baba Mtakatifu Francisko anamweka Askofu mkuu Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha na utume huu mpya katika Kanisa.

Mwenyekiti Mpya
02 July 2023, 15:11