Wanasiasa: Injili Iwe Ni Mwongozo na Mafundisho Jamii ya Kanisa: Dira ya Maisha na Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Afya ya Baba Mtakatifu Francisko tangu alipofanyiwa upasuaji mkubwa, Jumatano tarehe 7 Juni 2023 inaendelea kuimarika zaidi na hivyo kumwezesha kufanya shughuli ndogo ndogo akiwa bado amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Baba Mtakatifu kunako mwaka 2014 alipata nafasi ya kutembelea Bunge la Ulaya na kubahatika kukutana na kuzungumza na Kundi la “The European People’s Party, EPP.”
Kundi la “The European People’s Party, EPP,” ndilo kundi kubwa na kongwe zaidi katika Bunge la Ulaya lililoundwa kunako mwaka 1999. Hili ni kundi la mrengo wa kulia, ambalo limejizatiti kuunda Ulaya yenye nguvu na inayojiamini zaidi, iliyojengwa kuwahudumia raia wake. Lengo kuu ni kuunda Ulaya yenye ushindani na yenye demokrasia zaidi, ambapo watu wanaweza kujenga maisha wanayotaka. Kwa sasa Mwenyekiti wake ni Dr. Manfred Weber. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wabunge hawa amekazia kuhusu: Uwakilishi wa wananchi waliowachagua; Wingi wao kama Kundi; Amana na Utajiri wa Mafundisho Jamii ya Kanisa; Umoja katika utofauti wao; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu pamoja na utume kwa vijana ambao wanaishi Barani Ulaya! Baba Mtakatifu anawakumbusha wabunge hawa kwamba, chaguzi nyingi za kwanza kwanza zilikuwa na mvuto na mashiko kwa wananchi wa Ulaya, waliokuwa na kiu ya ujenzi wa umoja, lakini kadiri muda unavyoyoyoma, watu wameanza kuchoka na zoezi la kupiga kura kwa ajili ya chaguzi, kumbe, kuna umuhimu wa kufanya maboresho ya mahusiano na mafungamano kati ya wabunge na wananchi wanaowapatia ridhaa ya kuingia Bungeni na kwa kutumia njia za mawasiliano ya jamii, kuweza kupungumza umbali uliopo kati ya wabunge na wananchi wanaowachagua kushika nyadhifa mbalimbali. Kutokana na wingi na ukubwa wa chama hiki, kuna haja ya kujizatiti katika ujenzi wa umoja na mshikamano unaopaswa kusimikwa katika majiundo endelevu ya wabunge, ili kuwapatia fursa ya kukaa na kutafakari masuala ya maadili na utu wema ambao kwa sasa ni muhimu sana. Hii ni changamoto pevu kwani inagusa dhamiri ya mtu na hivyo kutoa mwanga kwa wanasiasa. Mwanasiasa mkatoliki anapaswa kujipambanua kwa kutafuta suluhu ya kudumu inayosimikwa katika utu, heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko amegusia kuhusu amana na utajiri wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaosimikwa katika mshikamano na kanuni ya auni; mwaliko wa kushirikishana amana na utajiri huu na wabunge wengine wanapojadili masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Umoja na Utofauti ni changamoto pevu inayowahimiza wabunge kushirikiana na kushikamana ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo mintarafu mawazo ya waanzilishi wa Jumuiya ya Ulaya, EU, ili watu wote waweze kuishi kama binadamu, huku wakijenga udugu na kuimarisha haki. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni ndoto ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameitoa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Hii pia inapaswa kuwa ni ndoto yao ili kujenga na kukuza siasa bora zaidi katika medani mbalimbali za maisha. Udugu huu unaweza kujengwa kwa kushirikiana na wakimbizi na wahamiaji sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Yote haya yapate chimbuko lake katika udugu wa kibinadamu. Mchakato wa ujenzi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ni matokeo ya athari za Vita Kuu ya Dunia katika Karne ya Ishirini. Wazo kuu likawa ni kujenga na kudumisha uhuru, haki na amani, kwa kukazia umoja katika utofauti wao. Leo hii, mradi huu mkubwa unakabiliana na changamoto pevu kutokana na utandawazi. Lakini, Bara la Ulaya linaweza bado kufanya rejea kwa mawazo ya wasisi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, si tu kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Bara la Ulaya peke yake, bali kwa ajili ya familia kubwa ya binadamu. Raia wa Bara la Ulaya wengi wao ni vijana wanaotafuta maisha bora zaidi kwa kujikita katika masomo na hatimaye fursa za ajira. Vijana wengi wanapenda kuanza masomo yao nchini mwao na hatimaye kujiendeleza zaidi, mahali pengine. Kumbe, kuna haja ya kujenga Ulaya kadiri ya ndoto ya vijana na kazi hii itendeke kwa ujasiri, matumaini pamoja na kutegemea msaada wa Mungu. Injili iwe ni nyota ya kuwaongoza na Mafundisho Jamii ya Kanisa yawe ni dira ya maisha na utume wao kama wanasiasa!