Tafuta

Baba Mtakatifu ameandika ujumbe unaounga mkono uzinduzi wa “Family Global Compact” ushirikiano unaopania kuunganisha nguvu za shughuli za kichungaji kuhusu familia. Baba Mtakatifu ameandika ujumbe unaounga mkono uzinduzi wa “Family Global Compact” ushirikiano unaopania kuunganisha nguvu za shughuli za kichungaji kuhusu familia. 

Ujumbe wa Papa Francisko Katika Uzinduzi wa "Family Global Compact 2023"

Papa ameandika ujumbe unaounga mkono uzinduzi wa “Family Global Compact” ushirikiano unaopania kuunganisha nguvu za shughuli za kichungaji kuhusu familia ili kujadiliana na vituo vya masomo na tafiti kuhusu maisha ya ndoa na familia vilivyoko kwenye vyuo vikuu vinavyondeshwa na Kanisa Katoliki, sehemu mbalimbali za dunia. Huu n mkakati unaoendeshwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Taasisi za Sayansi Jamii! Ndoa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” anasema kuhusu matukio na changamoto za familia kwamba ustawi wa familia unaamua jinsi siku za usoni za dunia na za Kanisa zitakavyokuwa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ameandika ujumbe unaounga mkono uzinduzi wa “Family Global Compact” ushirikiano unaopania kuunganisha nguvu za shughuli za kichungaji kuhusu familia ili kujadiliana kwa kina na mapana na vituo vya masomo na tafiti kuhusu maisha ya ndoa na familia vilivyoko kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni mpango mkakati unaoendeshwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kushirikiana na Taasisi za Kipapa za Sayansi Jamii, kwa kujikita katika tamaduni na uelewa wa binadamu kuhusu umuhimu wa familia na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Lengo kuu ni kuwezesha shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Makanisa mahalia kunufaika na tafiti pamoja na masomo yanayotolewa na taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuuu vya Kikatoliki sehemu mbalimbali za dunia, ili kuragibisha utamaduni familia na maisha katika nyakati hizi ambamo matumaini yanaendelea kufifia sana. Msimamo thabiti wa kitamaduni, utaweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu kuthamini ndoa na maisha ya kifamilia, kwa kutambua changamoto na uzuri wa kushiriki katika kazi ya uumbaji na malezi ya uhai wa binadamu. Kinachohitajika kwa sasa ni juhudi ya kuwajibika zaidi, na ukarimu wa kuweka wazi sababu na motisha za kuchagua ndoa na familia, na kwa njia hii kuwasaidia wanaume na wanawake kuitikia vizuri zaidi neema ambayo Mwenyezi Mungu anawawekea wazi. Rej. Amoris laetitia, 35.

Kinachohitajika kwa sasa ni juhudi za kuwajibika na ukarimu
Kinachohitajika kwa sasa ni juhudi za kuwajibika na ukarimu

Taasisi za elimu ya juu na vyuo vikukuu vya Kikatoliki vina dhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, vinaendeleza kwa kina taalimungu, falasafa, sheria, masuala jamii na uchumi mintarafu maisha ya ndoa na familia ili kusoma alama za nyakati kwa kuzingatia mawazo na matendo halisi. Tafiti nyingi zimeonesha mgogoro wa mahusiano na mafungamano ndani ya familia yanayochochewa na matatizo ya kimuundo na ukosefu wa msaada kwa familia kutoka katika jamii, kiasi cha kuzikosesha familia, amani na utulivu wa ndani. Hata hivyo, tafiti nyingi zinabainisha kwamba, familia zinaendelea kuwa ni kitovu cha maisha ya kijamii na mahali pa kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zinazopaswa kushirikishwa na kuragibishwa sehemu mbalimbali za dunia. Familia zinapaswa kuwa ni mashuhuda na viongozi katika mchakato huu. Mkakati wa “Family Global Compact” unasimikwa katika malengo makuu manne. Huu ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki kuhusu masomo na tafiti za masuala ya familia, ili kuweza kufanya shughuli hizi ziwe na ufanisi zaidi kwa kuunda mwingiliano wa mtandao wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya Kikatoliki mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kuandaa maudhui na malengo kati ya Jumuiya za Kikristo na Vyuo vikuu vya Kikatoliki. Kuragibisha utamaduni wa familia na maisha ya kijamii, ili kusaidia kuibua sera, mikakati na maazimio. Kuweka uwiano kati ya mapendekezo kama matokeo ya tafiti hizi, ili huduma kwa familia ya binadamu iweze kuendelezwa na hivyo kuenziwa: kiroho, kichungaji, kitamaduni, kisheria, kiasiasa, kiuchumi na katika masuala ya kijamii.

Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii
Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema ni kwa njia ya familia, ndoto ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Jumuiya ya mwanadamu inaweza kutendeka. Kumbe, kamwe, mwanadamu hawezi kupanga hatima ya familia kwa kujikita katika ubinafsi na ulaji wa kupindukia unaopelekea watu kujifikiria wao wenyewe. Haiwezekani kuipatia mgongo familia kama Jumuiya ya uhai na upendo, kiini cha agano lisilogawanyika kati ya bwana na bibi; mahali ambapo vizazi vinakutana, kiini cha matumaini ya jamii. Familia hauna budi kuangaliwa kwa jicho chanya kwamba, ni mahali pa kuzalisha mafao ya wengi. Familia yenye mahusiano na mafungamano yenye afya ni kiini cha utajiri si tu kwa wanandoa wenyewe pamoja na watoto wao, lakini kwa jumuiya nzima ya Kikanisa na Kiraia. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru na kuwapongeza wale wote waqliojiunga na kushiriki katika mkakati wa “Family Global Compact” bila kuwasahau wale watakaojiunga baadaye. Baba Mtakatifu anawaalika kujisadaka bila ya kujibakiza kwa njia ya kipaji cha ugunduzi na hali ya kujiamini katika utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali zitakazosaidia familia kuwa tena ni kitovu cha shughuli za kichungaji na majitoleo ya kijamii.

Papal Global Compact

 

05 June 2023, 10:55