Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Tume ya Kimataifa ya Majadiliano Kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Yesu: Roho Mtakatifu

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu; katika hotuba yake amejikita zaidi katika kufafanua kuhusu: Kumbukumbu, Roho Mtakatifu kama kiongozi na chemchemi ya utulivu anayeongoza na kuratibu majadiliano ya kiekumene katika sala inayomwilishwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili kielelezo cha imani tendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu: “The International Commission for Dialogue between the Catholic Church and the Disciples of Christ” iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1977. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amejikita zaidi katika kufafanua kuhusu: Kumbukumbu, Roho Mtakatifu kama kiongozi na chemchemi ya utulivu anayeongoza na kuratibu majadiliano ya kiekumene katika sala inayomwilishwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu amewakaribisha wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu, waliokusanyika kwa pamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalowataka kujibidiisha katika ujenzi wa ushirika na kwa wakati huu, wakiwa katika awamu ya sita, wanaendelea kujikita katika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu “Utume wa Roho Mtakatifu.” Nyaraka za awali zilitangaza “Roho Mtakatifu sio tu analipa Kanisa kumbukumbu ile inayoliwezesha kubaki katika Mapokeo ya Kitume, bali pia yumo ndani ya Kanisa, akiwaongoza Wakristo na jumuiya nzima ya wabatizwa kwa undani zaidi katika fumbo hilo la Kristo” (The Church as Communion in Christ, 39). Kwa hivyo Roho Mtakatifu ni kumbukumbu na kiongozi; ndiye atakayewafundisha yote, na kuwakumbusha yote  walioambiwa na Kristo Yesu. Rej. Yn 14:26.

Tume ya Kimataifa ya majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Yesu
Tume ya Kimataifa ya majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Yesu

Waamini wanapomkaribia kwa sala na moyo ulio wazi kwa Maandiko Matakatifu, wanamwachia nafasi Roho Mtakatifu atende kazi ndani mwao na kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mungu Rej. Lk 1:37. Roho Mtakatifu anawataka waamini kila siku wazaliwe upya kutoka juu. Rej. Yn 1: 1-21 ili kukoleza upendo kwa ndugu zao. Roho Mtakatifu ni kumbukumbu na kiongozi kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, Roho Mtakatifu hulitakatifuza Kanisa. Kwa nguvu ya Injili hulitia tena Kanisa ujana wake, hulitengeneza upya daima na kuliongoza lipate kuunganika kikamilifu na Bwana harusi wake. LG, 4. Roho Mtakatifu huliongoza Kanisa kwenye kweli yote, hulifanya kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya kihierakia na vya kikarama ambavyo kwavyo huliongoza na kulipamba kwa matunda yake. Kwa maneno machache kabisa, Roho Mtakatifu hulifanya Kanisa kuwa kijana na kwamba, mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji ni Roho Mtakatifu anayewawezesha wakristo kufurahi na kumtangaza Kristo Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wao na hivyo kuendelea kudumu katika kumtangaza na kumshuhudia pamoja na kuwalinda ili wasitumbukie katika kishawishi cha kukata tamaa na kuanza kujitafuta wenyewe.

Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa majadiliano ya kiekumene
Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa majadiliano ya kiekumene

Hizi ni dalili anasema Baba Mtakatifu Francisko zinazowatumbukiza kwenye malimwengu kwa kuuukataa unabii na kuendelea kuonesha makosa ya wengine, kwa kujikita katika upeo mfinyu, kwa hiyo hawajifunzi wala hawako tayari kumpokea msamaha. Njia pekee ya kuyaponya malimwengu haya yanayodumaza ni kuvutia ndani hewa safi ya Roho Mtakatifu anayewafungua kutoka kwenye kifungo cha ubinafsi uliofunikwa kwa utawa wa nje usiokuwa na Mungu na kamwe Wakristo wasijiruhusu kupokwa Injili. Rej. Evangelii gaudium, 97. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa njia ya jicho la imani, waamini wanaweza kutambua uwepo angavu wa Roho Mtakatifu na waamini wakiwa wanyenyekevu atawakirimi amani na utulivu wa ndani. Wakati wa Pentekoste ile ya kwanza kulikuwapo na migawanyiko mingi, lakini wakati wa Pentekoste yenyewe, mambo yote yakawa shwari, mwaliko kwa waamini ni kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu na hivyo kujikita katika ujenzi wa ushirika na utume wa Kanisa. Inapendeza ikiwa kama waamini watajihusisha kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni.

Roho Mtakatifu ni kiongozi na chemchemi ya utulivu.
Roho Mtakatifu ni kiongozi na chemchemi ya utulivu.

Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Wafuasi wa Kristo Yesu kujikita na hatimaye kuzama katika mchakato wa ujenzi wa ushirika wa Kanisa, kwa kuendeleza majadiliano ya kiekumene, kwani umoja wa Kanisa unapatikana kwa wakristo kutembea kwa pamoja. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua dhamana na nafasi ya wanataalimungu: kusoma, kuzungumza na kujadili, lakini waamini wanahamasishwa kusali pamoja na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ndiyo njia iendayo kwenye uzima wa milele. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kukubali maongozi ya Roho Mtakatifu na kwamba, bila shaka wataendelea kujizatiti kwa ujasiri mkubwa katika safari hii ambayo wamekwisha kuianzisha.

Tume ya Kimataifa
28 June 2023, 16:41