Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira Kwa Watoto Wadogo 12 Juni 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ulinzi wa utu na heshima ya binadamu ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake. Hizi ni haki ambazo zimebainishwa kwenye “Tamko la Haki ya Mtoto la Mwaka 1959” na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Yesu anaonya kwamba, Ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini!
Kanisa linataka pia kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kukomesha nyanyaso, biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yake; vita na ghasia; mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Umoja wa Mataifa katika Mikakati ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, tarehe 12 Juni 2023 anasema watoto wengi, badala ya kupata elimu bora, wanatumikishwa na kufanyishwa kazi kama watumwa. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujizatiti ili kumaliza janga la utumikishwaji wa watoto, kwani hawa ni tumaini la Taifa na kamwe Jumuiya ya Kimataifa isiruhusu matumaini haya yazuiwe! Baba Mtakatifu Francisko anasema, ameshuhudia mateso na mahangaiko ya watoto hawa sehemu mbalimbali za dunia, changomoto na mwaliko wa kuwajengea tena watoto hawa uwezo wa kuwa na furaha, amani na utulivu wa ndani kwa kuwaboreshea mazingira ya malezi na makuzi. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuunganisha nguvu kwa kujikita katika: haki, ujasiri na furaha ya kuwaangalia watoto machoni pao pasi ya kuona aibu! Ikumbukwe kwamba, utu na heshima ya binadamu vinafumbatwa katika kazi yake halali! Kumbe, kazi isiwe ni mahali pa kunyanyasa na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Kazi ni jina, heshima na utimilifu wa utu wa binadamu! Kila mtu ajisikie kuwa anawajibika kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo!
Utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa katika: Kazi za suluba, ukahaba, biashara ya binadamu na viungo vyake. Kuna masuala ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge. Matendo yote haya ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Tarehe 12 Juni ya kila Mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira za Watoto Wadogo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Haki Jamii Kwa Wote”: Kukomesha Ajira Kwa Watoto Wadogo.” Hadi sasa inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 160 kati ya umri wa miaka 5 hadi 17 waliotumbukizwa kwenye ajira za watoto sehemu mbali mbali za dunia. Kati yao kuna watoto milioni 79 wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, hawana fursa ya kusoma wala kucheza, bali wanalazimika kufanya kazi za suluba. Kumbe, Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa kushirikiana na, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, yanapenda kuwaalika wadau mbali mbali kushirikiana na kushikamana ili kupambana dhidi ya ajira ya watoto wadogo duniani, ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini zaidi. Ikumbukwe kwamba, asilimia kubwa ya ajira za watoto iko kwenye nchi changa zaidi duniani. Hali hii inaathiri ukuaji na ukomavu wa watoto kiafya, kisaikolojia, kiutu na kimaendeleo.