Tafuta

Papa amewashukuru na kuwapongeza wenyeji wa Roma, ambao walikuwa wanaadhimisha kwa namna ya pekee Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani ambao ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma. Papa amewashukuru na kuwapongeza wenyeji wa Roma, ambao walikuwa wanaadhimisha kwa namna ya pekee Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani ambao ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma.   (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Walinzi na Waombezi wa Mji wa Roma

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wenyeji wa mji wa Roma, ambao walikuwa wanaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo ambao ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma. Amewashukuru pia “Pro Loco wa Roma” walioandaa onesho la maua ambalo linatafakarisha kuhusu amani, changamoto na mwaliko wa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini kwa namna ya pekee amani nchini Ukraine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Itakumbukwa kwamba, Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa kwa manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Pia ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii imekuwa siku pia ya kuonesha umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Watakatifu Petro na Paulo walinzi na waombezi wa Mji wa Roma
Watakatifu Petro na Paulo walinzi na waombezi wa Mji wa Roma

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ulioongozwa na Askofu mkuu Job Getcha wa Jimbo kuu la Pissidia, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, Askofu Nazianzus Athenagoras Katibu mkuu wa Sinodi Takatifu ya Jimbo kuu la Marekani pamoja na Mheshimiwa sana Shemasi Kallinikos Chasapis. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uwepo na ushiriki wao na hivyo kwa pamoja wanapaswa kujizatiti katika kumfuasa Kristo Yesu sanjari na kuwatangazia watu wa Mataifa, Habari Njema ya wokovu, huku wakiendelea kukua na kukomaa katika udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amewakumbuka wakati wa mahubiri yake na hatimaye, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.

Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amedadavua kuhusu dhamana na utume wa Mtakatifu Petro katika Kanisa ili kuwasaidia ndugu zake katika ujenzi wa Kanisa; Petro katika maisha na utume wake, anatambua pia udogo na udhaifu wake, kiasi hata cha kutaka kuyakimbia mateso yaliyokuwa mbele yake, lakini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa wakasamehewa mapungufu yao ya kibinadamu na kuimarishwa kwa neema ya Mungu. Mitume hawa wawe ni mifano bora ya kuigwa katika nguvu, ukarimu na unyenyekevu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha ya kila siku! Kristo Yesu akasema: “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mt 16:18. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wenyeji wa mji wa Roma, ambao walikuwa wanaadhimisha kwa namna ya pekee Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani ambao ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma. Amewashukuru pia “Pro Loco wa Roma” walioandaa onesho la maua, ambalo kwa mwaka 2023 limefikia awamu yake yak umi. Ni onesho la maua ambalo linatafakarisha kuhusu amani, changamoto na mwaliko wa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini kwa namna ya pekee, amani kwa watu wa Mungu nchini Ukraine, wanaoteseka sana.  

Petro na Paulo
30 June 2023, 15:49