Tafuta

Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, Ijumaa tarehe 30 Juni 2023 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, Ijumaa tarehe 30 Juni 2023 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Ujumbe wa Kanisa la Kiorthodox: Ukulu na Sinodi

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi kuhusu: Kikao cha kumi na tano cha Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox; Mchakato wa Kisinodi ni kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Ushirika ni kazi ya Roho Mtakatifu, Madhara ya Vita kati ya Ukraine na Urusi na kwamba, amani inahatarishwa na tabia ya uchoyo, ubinafsi na mafao ya watu wachache ndani ya jamii. Ukulu na Sinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ulioongozwa na Askofu mkuu Job Getcha wa Jimbo kuu la Pissidia, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, Askofu Nazianzus Athenagoras Katibu mkuu wa Sinodi Takatifu ya Jimbo kuu la Marekani pamoja na Mheshimiwa sana Shemasi Kallinikos Chasapis. Ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, Ijumaa tarehe 30 Juni 2023 umekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia zaidi kuhusu: Kikao cha kumi na tano cha Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, kilichofanyika hivi karibuni huko Alexandria nchini Misri kwa mwaliko kutoka kwa Papa Theodoros II wa Kanisa la Kiothodox la Ugiriki, Patriaki wa Aleksandria na Afrika yote. Mchakato wa Kisinodi ni kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Ushirika ni kazi ya Roho Mtakatifu, Madhara ya Vita kati ya Ukraine na Urusi na kwamba, amani inahatarishwa na tabia ya uchoyo, ubinafsi na mafao ya watu wachache ndani ya jamii.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni ishara ya umoja wa Kanisa
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ni ishara ya umoja wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kikao cha kumi na tano cha Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox, kilichofanyika hivi karibuni huko Alexandria nchini Misri kwa mwaliko kutoka kwa Papa Theodoros II wa Kanisa la Kiothodox la Ugiriki, Patriaki wa Aleksandria na Afrika yote kimejadili pamoja na mambo mengine kuhusu mchakato wa Sinodi na ukuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na jinsi ya kutekeleza dhamana na utume huu katika muktadha wa mchakato wa Sinodi ambacho ni chombo cha huduma cha Kanisa kwa ajili ya kujenga na kuimarisha ushirika wa Kanisa na kwamba, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, siku moja wataweza kuunganishwa katika imani na mapendo. Huduma itakayokuwa inatolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro itabidi itenganishwe kati ya ukulu wa Mtakatifu Petro na Sinodi. Waamini wakumbuke kwamba, umoja wa Kanisa ni matunda na zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu; ni kielelezo cha udugu wa kibinadamu miongoni mwa wafuasi wa Kristo Yesu, wanaopendwa na Mungu Baba, huku wakiwa wamesheheni Roho wa Kristo Yesu wataweza kutatua changamoto za umoja katika tofauti zao msingi, kazi ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa Makanisa haya mawili kuendelea kumwita Roho Mtakatifu, ili kwa pamoja waweze kuendelea kuwa ni mashuhuda wa furana na majonzi, magumu na matumaini ya maisha.

Ukulu wa Mtakatifu Petro na Sinodi
Ukulu wa Mtakatifu Petro na Sinodi

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua madhara ya vita inayoendelea nchini Ukraine kwa kuwatumbukiza watu wa Mungu katika majanga na uharibifu mkubwa, lakini kama wakristo wasichoke kamwe kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano na kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu na kwamba, waamini wanahimizwa kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika ujenzi wa amani duniani. Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwamini na kwamba, vita na mipasuko ya kijamii ni matokeo ya uchoyo na ubinafsi, kumbe kuna haja ya toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika fadhila ya upendo unaowaangazia watu wote bila ya ubaguzi kwa kujitahidi hata kuwapenda adui zao: “ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” Mt 5:45. Huu ni upendo unaovuka mipaka, tayari kutangazwa na kushuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia kwa kujikita katika huduma na sadaka binafsi na kwa njia hii, waamini wataweza kujenga na kudumisha ushirika, ili kuganga na kuponya mipasuko na kinzani duniani.

Ujumbe wa Patriaki
30 June 2023, 16:14