Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Petro Mwamba wa Kanisa: Nguvu na Udhaifu Wake

Papa Francisko: Utume wa Mtakatifu Petro katika Kanisa; Petro katika maisha na utume wake, anatambua pia udogo na udhaifu wake, kiasi hata cha kutaka kuyakimbia mateso yaliyokuwa mbele yake, lakini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa wakasamehewa mapungufu yao ya kibinadamu na kuimarishwa kwa neema ya Mungu. Mitume hawa wawe ni mifano bora ya kuigwa katika nguvu, ukarimu na unyenyekevu ili kumtangaza Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ulioongozwa na Askofu mkuu Job Getcha wa Jimbo kuu la Pissidia, Askofu Athenagoras, Katibu mkuu wa Sinodi Takatifu ya Jimbo kuu la Marekani pamoja na Mheshimiwa sana Shemasi Kallinikos Chasapis. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amedadavua kuhusu dhamana na utume wa Mtakatifu Petro katika Kanisa ili kuwasaidia ndugu zake katika ujenzi wa Kanisa; Petro katika maisha na utume wake, anatambua pia udogo na udhaifu wake, kiasi hata cha kutaka kuyakimbia mateso yaliyokuwa mbele yake, lakini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa wakasamehewa mapungufu yao ya kibinadamu na kuimarishwa kwa neema ya Mungu. Mitume hawa wawe ni mifano bora ya kuigwa katika nguvu, ukarimu na unyenyekevu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha ya kila siku! Kristo Yesu akasema: “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mt 16:18.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba ya imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba ya imani.

Baba Mtakatifu anasema, Jina Petro linaweza kuwa na maana kadhaa yaani linaweza kumaanisha “Jiwe au Mwamba.” Katika maisha ya Mtakatifu Petro Mtume, mambo yote haya yanajidhihirisha wazi. Mtume Petro kama mwamba, anaonesha nguvu, anamtambua Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai; akajitosa baharini kwenda kukutana na Kristo Yesu aliyekuwa anatembea juu ya bahari; akamkiri Kristo Yesu na hatimaye akayamimina maisha yake mjini Roma. Petro ni jiwe ambalo lilitoa msaada katika ujenzi wa Makanisa kama walivyojibu na kuitikia wito kutoka kwa Kristo Yesu, Andrea nduguye, Yakobo wa Zebedayo na Yohane nduguye, akajibidiisha kuwahudumia wale waliokuwa wanateseka, akahimiza utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, akawa ni kiongozi wa Mitume na Jumuiya ya kwanza ya waamini. Mtakatifu Petro Mtume, kama jiwe alionesha udhaifu wake wa kibinadamu, wakati mwingine, alishindwa kutambua kile ambacho Kristo Yesu alikuwa akitenda. Kristo Yesu alipokamatwa, akateswa na kuhukumiwa afe, Petro Mtume, akashikwa na woga akamkana mara tatu, akashindwa hata kusimama chini ya Msalaba kutokana na woga wa hata yeye kukamata na kusulubishwa. Akiwa Antiokia, aliona aibu kushikamana na wapagani, lakini Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakazia ukweli wa Injili na neema ya imani akisema, “Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu. Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa. Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao. Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi? Gal 2:11-14.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba na mashuhuda wa imani
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba na mashuhuda wa imani

Kadiri ya “Quo Vadis” inaelezwa kwamba, Mtume Petro alipoona madhulumu yanamwijia akataka kuyakimbia, lakini akiwa njiani akutana mubashara na Kristo Yesu, akapata ujasiri wa kurejea nyuma na kuyakabili madhulumu kwa kutundikwa kichwa chini na miguu juu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maisha na utume wa Mtakatifu Petro yote yanajidhihirisha wazi kwani hakuna mtu ambaye ni mkamilifu, lakini alithubutu kukubali wito na mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa na hata kwa watakatifu wengine wote, waliwezeshwa kwa neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akawakirimia upendo na kuwasamehe mapungufu yao ya kibinadamu, kwa huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Hivyo ndivyo Roho Mtakatifu anavyojenga na kulisimamisha Kanisa la Kristo katika ubinadamu halisi wenye nguvu na udhaifu wake. Hata leo hii, Kanisa linahitaji kuwa na watu halisi. Huu ni mwaliko kwa waamini kujitathmini nyoyoni mwao ili kutambua ukweli wa maisha yao, kama kweli wao ni miamba wakiwa na ari na nguvu ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu? Je, wanasaidia katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kristo Yesu? Je, wanaendelea kujizatiti katika kutafuta na kudumisha umoja wa Kanisa? Je, wanatambua udogo na udhaifu wao wa kibinadamu, kiasi hata cha kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu katika ukweli na unyenyekevu wa moyo? Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Mitume ili aweze kuwasaidia kuiga nguvu, ukarimu na unyenyekevu wa watakatifu Petro na Paulo katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia. 

Petro Mtakatifu
29 June 2023, 15:04

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >