Tafuta

Rais Sergio mattarella wa Italia, Ametunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023. Rais Sergio mattarella wa Italia, Ametunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023.  

Rais Mattarella Atunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023: Ushuhuda wa Imani

Baba Mtakatifu Francisko, katika hotuba yake ya kumtunukia Rais Sergio mattarella wa Italia, Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023. Mtakatifu Paulo VI alitoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wanashirikishwa kwa namna ya pekee katika huduma ya kikuhani, ya kinabii na ya kifalme ya Kristo Yesu na hivyo wanatekeleza kadiri ya uwezo wao, utume wa Taifa lote la Kikristo katika Kanisa na katika ulimwengu. Huduma

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI (26 Septemba 1897 hadi 6 Agosti 1978) alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 21 Juni 1963. Tarehe 19 Oktoba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Na tarehe 14 Oktoba 2018 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Mtakatifu. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, Taasisi ya Paulo VI imeamua kumtunukia Rais Sergio Mattarella wa Italia, Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023 Jumatatu tarehe 29 Mei 2023. Rais Sergio Mattarella katika maisha na uongozi wake amejipambanua kuwa ni shuhuda wa huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia, kiongozi mwenye hekima na mwalimu wa maisha ambaye anawajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia, huku akisimamia: ukweli na uwazi pamoja na kuendelea kujikita katika utawala wa sheria, ili kujenga jamii inayosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa muhtasari hayo ndiyo yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Francisko, katika hotuba yake ya kumtunukia Rais Sergio mattarella wa Italia, Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023. Mtakatifu Paulo VI alitoa kipaumbele cha kwanza kwa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wanashirikishwa kwa namna ya pekee katika huduma ya kikuhani, ya kinabii na ya kifalme ya Kristo Yesu na hivyo wanatekeleza kadiri ya uwezo wao, utume wa Taifa lote la Kikristo katika Kanisa na katika ulimwengu.

Rais Sergio Mattarella wa Italia ametunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI
Rais Sergio Mattarella wa Italia ametunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI

Ni juu ya waamini walei kutokana na wito wao, kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadiri ya Mungu na kwamba, wanaitwa kusaidia kuutakatifuza ulimwengu, wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo thabiti. Rej. LG, 31. Uongozi bora unakwenda sanjari na uwajibikaji kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Kristo Yesu anasema, “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” Mk 10:42-44. Kristo Yesu anaufananisha ukuu na huduma, kwani kuishi ni kuhudumia. Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023 ambayo ametunukiwa Rais Sergio Mattarella wa Italia ni fursa ya kusherehekea tunu na heshima ya huduma inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa watu anaowahudumia. Rais Sergio Mattarella amekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa kujitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya kijamii, kidini pamoja na kujenga mshikamano wa watu wa Mungu nchini Italia, kiasi hata cha kuwa ni mfano wa hekima ya kimaadili na mwalimu wa maisha. Kimsingi, huduma ni chanzo cha furaha na maisha bora.

Papa Francisko akimkabidhi Rais Mattarella Tuzo ya Kimataifa
Papa Francisko akimkabidhi Rais Mattarella Tuzo ya Kimataifa

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huduma hii inakwenda sanjari na uwajibikaji, ili kutoa majibu muafaka kwa wakati wake na kwa hili Rais Mattarella amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa matendo yake. Ili kusimamia haki, kuna haja ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kujenga mafungamano ya kijamii na kiutu. Kuna watu ambao wamesadaka maisha yao kwa ajili ya kulinda na kutetea haki, kama kaka yake Rais Sergio aliyejulikana kama Piersanti Mattarella (Alizaliwa Castellammare del Golfo, tarehe 24 Mei 1935 na kuuwawa kikatili huko Palermo, 6 Januari 1980). Kwa hakika Rais Mattarella katika utekelezaji wa utawala wa haki na sheria amewajibika barabara. Mtakatifu Paulo VI katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikazia sana uwajibikaji, haki na amani hasa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Leo hii changamoto kubwa ni athari za mazingira nyumba ya wote na waamini wanapaswa kuwajibika barabara. Mtakatifu Paulo VI aliacha msingi mkubwa wa ujenzi wa jumuiya inayoshikamana na kushirikishana pia maisha. Kuna watu wa Mungu wanaomwona Rais Sergio Mattarella kuwa ni mfano bora wa huduma ya uongozi na uwajibikaji. Walimwengu wanawasikiliza zaidi mashuhuda kuliko waalimu.

Rais Mattarella shuhuda wa imani katika matendo
Rais Mattarella shuhuda wa imani katika matendo

Kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia katika hotuba yake ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko amemwelezea Mtakatifu Paulo VI kuwa ni kiongozi aliyekuwa na mwono safi wa imani, utu, heshima ya binadamu; uhuru na amani duniani. Amesema, ameshangazwa sana kuteuliwa kupokea Tuzo ya Kimataifa ya Paulo VI Kwa Mwaka 2023. Fedha inayoambatana na Tuzo hii ya Kimataifa ameitoa kwa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII, ili kusaidia huduma kwa watu waliokumbwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo huko Emilia Romagna. Rais Mattarella anaukumbuka mchango wa Mtakatifu Paulo wa VI katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake.

Rais Sergio Mattarella

 

05 June 2023, 10:24