Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Ufuasi; Utangazaji na Ushuhuda wa Injili

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 29 Juni 2023, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, amebariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Kutoka Barani Afrika Maaskofu wakuu hao ni: Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes wa Jimbo kuu Maputo Msumbiji pamoja na Askofu mkuu Jean de Dieu Raoelison wa Jimbo kuu la Antananarivo, Madagascar. Itakumbukwa kwamba, Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa kwa manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wapya wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni siku pia ya kuonesha umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani.

Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli ulioongozwa na Askofu mkuu Job Getcha wa Jimbo kuu la Pissidia, Askofu Athenagoras, Katibu mkuu wa Sinodi Takatifu ya Jimbo kuu la Marekani pamoja na Mheshimiwa sana Shemasi Kallinikos Chasapis. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uwepo na ushiriki wao na hivyo kwa pamoja wanapaswa kujizatiti katika kumfuasa Kristo Yesu sanjari na kuwatangazia watu wa Mataifa, Habari Njema ya wokovu, huku wakiendelea kukua na kukomaa katika udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi kuhusu ufuasi wa Kristo Yesu na kwamba Kanisa ni mahali pa kukutana na Kristo Yesu na waamini kati yao; Paulo Mtume katika maisha yake, alijikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuinjilisha na kuinjilishwa na kwamba, furaha ya Kanisa ni kuinjilisha. Mama Kanisa anawasherehekea miamba wawili wa imani walionesha mapendo thabiti kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kiasi cha kutoa majibu muafaka kwamba, Kristo Yesu alikuwa nani kwao, kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu na jibu muafaka kutoka katika undani wa maisha ya Mtakatifu Simoni Petro aliyejibu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Mt 16:16. Hili ni jibu la haraka na muafaka na ni kama muhtasari wa Katekesi. Mwinjili Mathayo anasimulia yale yaliyojiri tangu siku ile ya kwanza ambapo Kristo Yesu alivyomwita Petro na Andrea nduguye, mara wakaziacha nyavu zao wakamfuata na tangu siku hiyo, katika kumfuasa Kristo Yesu kila siku alijitahidi kufuata nyayo zake hadi siku ile ya mwisho, Yesu akamwambia “nifuate.” Yn 21:22.

Sherehe imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza
Sherehe imehudhuriwa na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza

Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kufafanua kwamba, ili kumfahamu Kristo Yesu kwa undani zaidi, kuna haja ya kusoma, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kirafiki. Huu ni mwaliko wa kutoa jibu la “Ndiyo” na kuanza kumfuasa Kristo Yesu bila kumwekea vikwazo au vizingiti vya maisha, bali jambo la msingi ni kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuachana na kisingizio kwamba, mimi siwezi, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye muweza wa yote na wala si kwa nguvu za kibinadamu. Kumbe, kuna haja ya kujimanua kutoka katika uhakika wa usalama wa maisha na kuanza kumfuasa Kristo Yesu siku kwa siku. Kanisa linalopaswa kuwa ni mfuasi wa Kristo Yesu linasimikwa katika fadhla ya unyenyekevu na huduma kwa Habari Njema ya Wokovu. Ni kwa jinsi hii, Kanisa litaweza kuanzisha na kuendeleza mchakato wa majadiliano na watu wote na hivyo kuwa ni mahali pa kuwakutanisha watu, tayari kuwasindikiza sanjari na kuwatangazia ukaribu pamoja na Injili ya matumaini kwa watu wa nyakati hizi, ili hatimaye, watu wenye mapenzi mema watambue kwamba, Kanisa ni mahali pa kukutana na Mwana wa Mungu aliye hai na ni mahali pa watu wa Mungu kukutana pia wao kwa wao. Mtakatifu Petro, Mtume alijikita katika dhana ya ufuasi wa Kristo Yesu katika maisha na Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa alizama zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Baadhi ya Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa mwaka 2022-2023
Baadhi ya Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa mwaka 2022-2023

Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anazungumzia haki ya ukweli na hamu ya kuwa na Kristo Yesu aliyekutana naye mubashara akiwa njiani kuelekea Dameski akiwa na kibali cha kuwapeleka mbele ya mahakama wale wote waliokuwa wanafuata njia mpya. “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani…” Fil 3:7-9. Hivi ndivyo alivyofanya Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa akafanya safari nyingi za kimisionari, akateseka sana na kudhulumiwa, lakini akapiga moyo konde na kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kiasi kwamba, Neno la Mungu lilimwezesha kuzama zaidi katika Fumbo la Mungu, kiasi kwamba, ijapokuwa anaihubiri Injili, hana la kujisifia, kwani amewekewa masharti; tena “Ole wake asipoihubiri Injili” na kwamba, kwake Mtume Paulo kuishi ni Kristo na kufa ni faida. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anaendelea kujibu swali la msingi, Je, Kristo Yesu ni nani kwako?

Papa amebariki pia Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu
Papa amebariki pia Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu

Paulo Mtume anafundisha kwamba, waamini wanakua kiimani na katika utambuzi wa Fumbo la maisha ya Kristo Yesu, ikiwa kama waamini hao ni watangazaji na mashuhuda wa Injili na kwamba, waamini wanaitwa kuinjilisha pamoja na wao wenyewe kuinjilishwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, daima likitambua kwamba, linaishi kwa sababu ya Kristo Yesu ili kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu na furaha ya Injili ya Kristo. Sherehe ya watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani ni jibu muafaka la jinsi watakatifu hawa walivyoishi na kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Hili ni Kanisa ambao ni kielelezo cha ufuasi wa Kristo Yesu ambalo pia katika unyenyekevu linamtafuta Kristo Yesu kwa ud ina uvumba. Hili ni Kanisa ambalo linapata utimilifu wa furaha yake kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika medani mbalimbali za maisha ya waamini na hasa pale ambapo umaskini umekithiri na watu wanatupwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023 amewataka wawe kama Mitume Petro na Paulo, tayari kumfuasa Kristo Yesu na hivyo kutangaza na kushuhudia uzuri wa Injili mahali popote pale walipo, huku wakishikamana na watu watakatifu wa Mungu.

Watakatifu Petro na Paulo

 

29 June 2023, 15:32