Tafuta

. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa pongezi wamisionari wa Consolata wanaoadhimisha Mkutano Mkuu wa XIV . . Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa pongezi wamisionari wa Consolata wanaoadhimisha Mkutano Mkuu wa XIV . 

Papa Francisko Awapongeza Wamisionari wa Consolata kwa Huduma Ndani ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa pongezi wamisionari wa Consolata wanaoadhimisha Mkutano Mkuu wa XIV pamoja na kuwatakia heri na baraka, daima wakijitahidi kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na kuendelea kuthamini maisha ya udugu katika jumuiya zao. Mheshimiwa Padre James Bhola Lengarin, kutoka Kenya amechaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Consolata na hivyo kuandika historia ya kuwa ni Mwafrika wa kwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Shirika ni kipindi maalum cha sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa Shirika na wanashirika wenyewe; maisha na utume wa Shirika kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda katika kipindi cha miaka sita kuanzia sasa! Shirika la Wamisionari wa Consolata, I.M.C., kuanzia tarehe 22 Mei hadi tarehe 25 Juni 2023 linaadhimisha Mkutano Mkuu wa XIV wa Shirika unaonogeshwa na kauli mbiu: Kuwekwa wakfu kwa ajili ya utume. Nanyi mtakuwa ni mashahidi wangu hata mwisho wa nchi”: “Consacrati per la missione. Mi sarete testimoni fino agli estremi confini della terra.” Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia ujumbe wa pongezi wamisionari wa Consolata wanaoadhimisha Mkutano Mkuu wa XIV pamoja na kuwatakia heri na baraka, daima wakijitahidi kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na kuendelea kuthamini maisha ya udugu katika jumuiya zao. Anawahimiza kufanya upembuzi yakinifu utakaowasaidia kubainisha hija za maisha ya kiroho na kichungaji, ili kupyaisha na kuendeleza ari, mwamko wa kimisionari na utume wa Shirika mintarafu karama ya Muasisi wa Shirika la Consolata Mwenyeheri Joseph Allamando na kwa msaada wa neema ya Mungu na sala waweze kutekeleza azma ya kutangaza na kushuhudia mwanga wa Injili sehemu mbalimbali za dunia, lakini hasa pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu.

Mkuu wa Shirika la Waconsolata na Msaidizi wake
Mkuu wa Shirika la Waconsolata na Msaidizi wake

Baba Mtakatifu anawapongeza wamisionari wa Consolata kwa huduma wanayoitoa kwa Kanisa la Kristo. Anawaombea nguvu ya Roho Mtakatifu wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa XIV pamoja na kuwazamisha kwenye ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mfariji. Wamisionari wa Consolata katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa XIV wamemchagua Mheshimiwa Padre James Bhola Lengarin, kuwa mkuu wa Shirika na hivyo kuandika ukurasa wa historia mpya ya Waconsolata kwa kuwa mmisionari wa kwanza kutoka Kenya, Barani Afrika kushika wadhifa wa Mkuu wa Shirika. Padre Michelangelo Piovano, Makamu mkuu wa Shirika. Washauri wakuu wa Shirika ni Padri Owuor Mathews Odhiambo, Padre Juan Pablo De los Ríos Ramírez pamoja na Padre Erasto Colnel Mgalama. Shirika la Wamisionari wa Consolata lenye umri wa miaka 122 wa maisha na utume wake ndani ya Kanisa lina jumla ya wamisionari 905 kutoka katika nchi 30, wanaoishi na kutekeleza utume wao katika Jumuiya 231 ambazo ziko Barani Afrika, Amerika, Asia na Bara la Ulaya.

Maandamano ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa XIV, 2023
Maandamano ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa XIV, 2023

Shirila la Wamisionari wa Waconsolata lilianzishwa na Mwenyeheri Joseph Allamano, kunako mwaka 1901, Jimbo kuu la Torino, nchini Italia. Mwaka 1919 Wamisionari wanne wa Consolata walifika kuanzisha utume huko Tosamaganga na Madibira. Mwaka 1922 Sehemu ya Iringa ilikabidhiwa rasmi na Vatican kwa Shirika la Waconsolata chini ya Monsinyo Francesco Cagliero (1922-35). Makao makuu ya Shirika yakawa ni huko Tosamaganga. Kama usimamizi wa kitume ikiwa na sehemu ya Uhehe yenye utume huko Tosamaganga, Jimbo Katoliki la Iringa; Usangu yenye utume huko Madibira; Ugogo yenye utume huko Bihawana na Pandangani; Ulanga na Masagati yenye vituo vya Mchombe, Merere na Sangi na vile vile Ubena na Ukinga ilikuwa bado bila misioni. Utume huu ulipandishwa kuwa Vikariati mwaka 1948 na Monsinyo Atillio Bertramino (1936 - 1965) aliwekwa wakfu na kuwa Askofu. Mwaka 1963 alihamishia makao makuu ya Jimbo Kihesa, Iringa mjini. Shirika la Wamisionari wa Consolata, limeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya maisha, uwepo na utume wake nchini Tanzania. Kilele cha maadhimisho haya kilikuwa ni tarehe 14 Oktoba 2019, Kanisa nchini Tanzania lilipomwimbia Mwenyezi Mungu, utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Waconsolata wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Faraja kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Mwenyeheri Joseph Allamano katika maisha yake, alibahatika kuwa ni: mwalimu, mtume na kiongozi wa maisha ya kiroho. Katika shughuli za kitume, alikazia kwa namna ya pekee mambo makuu mawili: Kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, yaani: Kuhubiri, ili watu waweze kumfahamu Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, faraja ya watu wa Mungu.

Jubilei ya Miaka 100 ya Faraja nchini Tanzania
Jubilei ya Miaka 100 ya Faraja nchini Tanzania

Pili, ilikuwa ni muhimu sana kusoma alama za nyakati, kwa kuangalia maisha ya watu, ili kujizatiti katika mchakato wa kuwainu: utu na heshima yao kwa kuwapatia huduma yenye kutukuka. Lengo ni kuinua hali ya maisha ya watu wanaowahudumia, ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa maisha. Ni katika muktadha huu, Wamisionari wa Consolata katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, katika maisha na utume wao, wamejielekeza zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Padre Dietrich Canisius Kihaule Pendawazima wa Shirika la Wamisionari wa Consolata katika mahojiano maalum na Radio Vatican alibainisha jinsi ambavyo Shirika la Wamisionari wa Consolata limekuwa faraja kwa familia ya Mungu nchini Tanzania katika: kutangaza na kushuhudia Injili ya faraja kwa njia ya: huduma za Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya faraja ya maisha ya kiroho; huduma ya elimu, afya na malezi kwa mihimi ya uinjilishaji kwa siku za usoni. Wamisionari wa Consolata wanatambua, wanakiri na kuungama kwamba, faraja ya kweli ni Kristo Yesu. Kumbe, mchakato wa uinjilishaji unawasaidia watu wa Mungu kuona sura ya ufunuo wa: faraja, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa hakika, upendo wa Kristo kwa waja wake ndicho kilele cha faraja yenyewe! Mwenyeheri Joseph Allamano alipenda kusema: “Justitia et pax osculatae sunt!”  yaani “Haki na amani zimebusiana.” Padre Dietrich Canisius Kihaule Pendawazima ambaye amewahi kuwa Makamu wa mkuu wa Shirika la Consolata, kwa sasa anatekeleza dhamana na utume wake nchini Argentina anasema, Parokia ya Tosamaganga ni kitovu cha uinjilishaji wa kina kwa Waconsolata nchini Tanzania. Hapa, Waconsolata walianzisha shule, ili kutoa elimu bora na makini ambayo itawawezesha watanzania kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha yao, ili hatimaye, kuyabadili mazingira, ili Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa XIV kwa mwaka 2023
Wajumbe wa mkutano mkuu wa XIV kwa mwaka 2023

Shule hii imekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, tofauti msingi walizo nazo watanzania ni utajiri, amana na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto ya kushikamana kwa dhati ili kukuza umoja, upendo na mshikamano, kama sehemu ya utambulisho wao kama wa watanzania! Wamisionari wa Consolata walianzisha Hospitali ya Tosamaganga ambayo kwa sasa inaendeshwa na Jimbo Katoliki la Iringa nchini ya usimamizi wa Masista wa Jimbo. Ikumbukwe kwamba, Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Jimbo Katoliki la Iringa lilianzishwa na Askofu kutoka Shirika la Waconsolata. Leo hii, watawa hawa wanaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma, upendo na faraja ya Mungu kwa watanzania. Hospitali ya Ikonda inayo milikiwa na kuongozwa na Wamisionari wa Consolata inaendelea kupeta katika huduma kwa kutumia vifaa vya kisasa ili kusaidia kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hospitali ya Ikonda kwa sasa inafahamika ndani na nje ya Tanzania kutokana na huduma zinazojali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Padre Dietrich Canisius Kihaule Pendawazima anaendelea kupembua faraja ya Mungu kwa watu wa Mungu nchini Tanzania kwa njia ya malezi na majiundo ya kipadre. Seminari ndogo ya Mafinga imekuwa ni kitalu cha kukuza na kulelea miito ya Kipadre na Kitawa! Imekuwa ni chimbuko la waamini wengi walei, ambao leo hii ni mifano bora ya kuigwa katika huduma kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Ikumbukwe kwamba, si kila jandokasisi anayeingia Seminarini, atafanikiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre! Katika muktadha huu, Waconsolata wameendelea kutoa malezi na majiundo makini kwa vijana wanaowekwa chini ya ulinzi na tunza yao kama walezi wa miito na kumwachia nafasi Bwana wa mavuno, ili aweze kukamilisha kazi yake! Nyumba ya Malezi, Jimbo Katoliki la Morogoro pamoja na Seminari ya Falsafa iliyoko Jimbo kuu la Nairobi ni matumaini ya Shirika la Consolata ndani na nje ya Bara la Afrika. Kwa hakika ya mbeleni yanapendeza na kwamba, Mwe! Iringa kumenoga!

Waconsolata

 

16 June 2023, 15:44