Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 22 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Wanashirika wa “Assumption”. Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 22 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Wanashirika wa “Assumption”.   (Vatican Media)

Mkutano Mkuu wa 96 wa ROACO: Injili ya Matumaini Kwa Watu wa Mungu Walioathirika Kwa Vita

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 22 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na Wanashirika wa “Assumption”. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu ametafakari kuhusu kauli mbiu ya Mkutano mkuu wa 34: “Ufalme wa Mungu umekaribia: kuishi na kutangaza matumaini ya Injili” mintarafu moyo wa Mtakatifu Augustino “Adveniat Regnum tuum." Mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni amani, udugu na maridhiano na wala si vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, (R.O.A.C.O. Riunione Opere Aiuto Chiese Orientali), kuanzia tarehe 19 - 22 Juni 2023 limekuwa likiadhimisha Mkutano wake wa 96. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali za huruma na upendo zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa athari za Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 96 wa ROACO, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 22 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa ROACO. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewashukuru kwa kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuganga na kuponya madonda ya watu wanaoteseka; ili hatimaye, kuwarejeshea tena matumaini wale wanaoteseka kutokana na vita, kinzani na machafuko sehemu mbalimbali za dunia. Mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni: amani, udugu na maridhiano; vijana wa kizazi kipya kwa Makanisa ya Mashariki; kumbukizi ya miaka kumi ya Waraka wa Kitume “Ecclesia in Medio Oriente” yaani “Kanisa Mashariki ya Kati” na kwamba, ROACO inatumwa kupandikiza mbegu ya matumaini kwa kuganga na kuponya madonda ya athari za tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Siria.

Mkutano Mkuu wa 96 wa ROACO 2023
Mkutano Mkuu wa 96 wa ROACO 2023

Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe wa ROACO kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuganga na kuponya madonda ya watu wanaoteseka; ili hatimaye, kuwarejeshea tena matumaini wale wanaoteseka kutokana na vita, kinzani na machafuko sehemu mbalimbali za dunia. Anasema, mpango wa Mungu kwa binadamu katika ulimwengu mamboleo niamani, udugu wa kibinadamu na maridhiano kwa watu wote, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kuunganisha nguvu kupambana na ujinga, maradhi na baa la njaa; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hata baada ya mauaji ya Abeli yaliyofanywa na ndugu yake Kaini, lakini Mwenyezi Mungu alimwonea huruma Kaini, kielelezo cha kwanza cha haki na huruma, mpango wa Mungu unaotaka kuwakumbatia na kuwaokoa watu wote katika Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ROACO kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wanaoogozwa na kauli mbiu “Kanisa Likishirikiana Safari na Vijana wa Kizazi Kipya: Vijana Watendaji Wakuu wa Mafao ya Wengi” ni uamuzi wa hekima na busara, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni wadau wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kuwa wajenzi na walinzi wa amani kwa wote; manabii wanaoota ndoto na kutangaza umoja na mshikamano wa watu wa Mungu.

ROACO inataka kuwekeza katika Injii ya matumaini kwa vijana
ROACO inataka kuwekeza katika Injii ya matumaini kwa vijana

Katika kumbukizi ya miaka kumi tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume “Ecclesia in Medio Oriente” yaani “Kanisa Mashariki ya Kati” huko Cyprus, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikuwa anawahimiza vijana wa kizazi kipya kujenga mahusiano na mafungamano thabiti na Kristo Yesu kwa njia ya sala, chemchemi ya imani, upendo wa dhati sanjari na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Msalaba unamshirikisha Mwenyezi Mungu katika mateso yanayomsibu binadamu na kwa namna ya pekee, vijana wanaotafuta ujasiri wa ushuhuda, nguvu inavyovunjilia mbali ubinafsi, uchoyo na tabia ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine, ili kukua na hatimaye, kukomaa kwa fadhila ya huruma, kiini cha imani ya Kanisa kinachoonesha upendo wa Mungu unaomfanya kujihusisha kwa namna ya pekee na mateso ya mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ROACO inatumwa kupandikiza mbegu ya matumaini kwa kuganga na kuponya madonda ya athari za tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Siria na hivyo kuendelea kuwa ni chombo cha huruma na faraja kwa watu wanaoteseka. Watu wengi wametoa ahadi, lakini bado kuna ugumu wa fedha kuwafikia walengwa. Anawapongeza kwa huduma kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi kutoka nchini Ukraine, mwaliko kwa wajumbe wote kuonesha uwepo na ukaribu wao kwa watu wa Mungu nchini Ukraine kwa sala na matendo ya huruma pamoja na kuendelea kusaidia kugharimia miradi ya Kanisa nchini Iran, Uturuki na Eritrea. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, amana na utajiri mkubwa aliowakirimia watu wa Mungu katika maeneo haya uleta faraja kwa wananchi katika nchi hizi.

Injili ya faraja kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Siria na Uturuki
Injili ya faraja kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Siria na Uturuki

Itakumbukwa kwamba, Mkutano mkuu wa 96 wa ROACO umefunguliwa tarehe 19 Juni 2023 kwa ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki. Nia ya Ibada hii ya Misa imekuwa ni kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati. Wajumbe wa ROACO pamoja na mambo mengine, wamekuwa wakijadili kwa kina na mapana madhara ya vita, kinzani na machafuko ya kidini na kisiasa huko Mashariki. kwa kuwasikiliza viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu. Wajumbe wamepata fursa ya kujadili kuhusu Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta" kwa Mwaka 2023 pamoja na hali ya Makanisa mahalia ambayo yako chini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amewashirikisha wajumbe wa ROACO kuhusu mpango mkakati wa diplomasia ya Vatican kuhusu: Vita kati ya Ukraine na Urusi; Hali tete huko Mashariki ya Kati pamoja na machafuko ya kisiasa nchini Ethiopia. Mabalozi wa Vatican nchini Uturuki na Iran wamewashirikisha wajumbe wa ROACO hali halisi ya huko wanakotoka pamoja na hali ya kisiasa, kijamii na kidini ilivyo nchini Eritrea, taarifa iliyotolewa na Askofu mkuu Menghesteab Tesfamariam, M.C.C.I wa Jimbo kuu la Asmara.

Hali ya kisiasa na kijamii nchini Eritrea
Hali ya kisiasa na kijamii nchini Eritrea

Jumatano tarehe 21 Juni 2023 ni siku ambayo ROACO imetenga kwa ajili ya kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kutoka katika nchi 13 za Makanisa ya Mashariki ambazo ziko chini ya uongozi na usimamizi wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makanisa ya Mashariki. Vijana hawa wamekuwepo mjini Roma kuanzia tarehe 16 na wataendelea kuwepo hadi tarehe 23 Juni 2023 ili kujadili tema inayohusu “Kanisa Likishirikiana Safari na Vijana wa Kizazi Kipya: Vijana Watendaji Wakuu wa Mafao ya Wengi.” Hii imekuwa ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya kufahamiana, kusali kwa pamoja, kutafakari pamoja na kutembelea mji wa Roma ambao umesheheni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa na hatimaye, kushirikishana na wajumbe wa ROACO jinsi ya kusongesha mbele ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, vijana wakiwa ni wadau katika mchakato huu.

Papa Roaco 96
22 June 2023, 15:50