Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kutembelea nchini Mongolia kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 4 Septemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kutembelea nchini Mongolia kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 4 Septemba 2023.  

Papa Francisko Kutembelea Mongolia Kuanzia 31 Agosti Hadi 4 Septemba 2023!

Papa ametia nia ya kutembelea nchini Mongolia kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 4 Septemba 2023. Baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Mongolia. Kardinali Giorgio Marengo, Msimamizi wa Kitume wa Ulaanbaatar, Mongolia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mongolia ni ushuhuda wa uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa familia ya Mungu Mongolia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea kutoka nchini Hungaria, baada ya kuhitimisha hija yake ya 41 ya Kitume, alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kujibu maswali matano yaliyohusu: Mtazamo wake kuhusu Hungaria; Ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023 na hatimaye, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni mintarafu hija yake ya kitume nchini Mongolia. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kutembelea nchini Mongolia kuanzia tarehe 31 Agosti hadi tarehe 4 Septemba 2023. Na hii itakuwa ni hija yake ya 43 ya Kitume, baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Mongolia. Kardinali Giorgio Marengo, Msimamizi wa Kitume wa Ulaanbaatar, nchini Mongolia katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mongolia ni ushuhuda wa uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa familia ya Mungu nchini Mongolia, itakayoleta ari na msukumo wa pekee kwa waamini na wamisionari wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jumuiya ya wamisionari nchini Mongolia inaundwa na wamisionari 75 kutoka katika nchi 27. Kuna Mapadre 29 na kati yao kuna Mapadre 2 wa Jimbo, watawa ni 36, watawa wa kiume ni 6 na 3 ni waamini walei. Kuna nyumba 9 za ibada zilizosajiriwa kwa ajili ya huduma kwa waamini 1,500.

Papa Francisko ametia nia ya kutembelea Mongolia
Papa Francisko ametia nia ya kutembelea Mongolia

Kazi kubwa ya Kanisa nchini Mongolia ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; sanjari na kukuza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Mongolia katika ujumla wake. Kanisa nchini Mongolia ni maskini na bado ni changa sana linalosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Hiki ni kikundi cha waamini wachache, ambao wangeweza kukusanyika na kupigwa picha ya pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Jumuiya inayojitahidi kukuza, kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwaka 2022, Kanisa nchini Mongolia limeadhimisha kumbukizi ya Miaka 30 ya Uinjilishaji nchini Mongolia, kazi na utume ambao umetekelezwa kwa umakini mkubwa na Wamisionari wa Moyo Safi wa Bikira Maria waliofika nchini humo kunako mwaka 1992.

Kanisa nchini Mongolia: Uinjilishaji wa kina: mahitaji msingi.
Kanisa nchini Mongolia: Uinjilishaji wa kina: mahitaji msingi.

Kunako mwaka 2003 Wamisionari wa Consolata waliwasili nchini Mongolia ili kuongeza ari, kasi na nguvu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Itakumbukwa kwamba, Mongolia inapakana na Urusi pamoja na China, lakini ni nchi inayokabiliana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini pia bado kuna watu wa Mungu ambao hawajaguswa na maendeleo haya na kwamba, bado wanasiginwa na umaskini, upweke na utupu wa maisha ya ndani. Kumbe, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Mongolia kama hujaji wa mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, mchakato unaopania kuwasaidia waamini kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake ndani na nje ya Mongolia. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Papa Mongolia

 

05 June 2023, 15:12