Papa Francisko: Ujio wa Roho Mtakatifu Mfariji, Msaidizi, Wakili na Jirani Mwema!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema pale tu ilipotimia saa atakapotukuzwa Yesu anaahidi ujio wa Roho Mtakatifu, kwani kifo na ufufuko vitakuwa ni utimilifu wa ahadi waliyopewa Mababa: Roho wa kweli, Msaidizi mwingine atatolewa na Baba kwa ombi la Kristo Yesu; atatumwa na Baba kwa jina la Yesu; Yesu atampeleka atakapokuwa kwa Baba kwa sababu ametoka kwa Baba. Roho Mtakatifu atakuja, na waamini watamjua, atakuwa pamoja nao daima, atawafundisha kila kitu, na kuwakumbusha yote aliyosema Kristo Yesu, naye atatoa ushuhuda. Atawaongoza waamini kwenye kweli yote na atamtukuza Kristo Yesu; atauhakikishia ulimwengu juu ya dhambi, haki na hukumu. Rej. KKK. 729. Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka inamzungumzia Roho Mtakatifu, ambaye Kristo Yesu anamwita “Msaidizi,” kadiri ya maana ya neno “Yule ambaye anaitwa awe jirani,” Wakili (Advocatus) na Mfariji, Kristo Yesu akiwa ndiye Mfariji wa kwanza. Bwana Mwenyewe anamwita Roho Mtakatifu kuwa ni Roho wa kweli. Rej. KKK. 692. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 14 Mei 2023 amemtafakari Roho Mtakatifu: Msaidizi anayeitwa awe jirani na msaada kwa wale watakao watuhumu na kuwashitaki.
Roho Mtakatifu ni jirani mwema, maana anakaa kwao naye yu ndani yao. Roho Mtakatifu si mgeni wa kupita, bali ni mwandani wa safari anayetamani kukaa katika nyoyo za waamini. Roho Mtakatifu ni mvumilivu hata pale waamini wanapoteleza na kuanguka, bado anaendelea kubaki kwa sababu anawapenda kweli kweli na kamwe hawezi kuwaacha katika mateso na mahangaiko ya ndani. Roho Mtakatifu ni Mfariji wakati wa majaribu, mahangaiko na mateso, ndiye anayewaletea waamini msamaha na nguvu ya Mungu; anayewasahihisha kwa upole, huruma na upendo. Roho Mtakatifu Mfariji ni rafiki wa kweli na ni mwaminifu anayewafunza waamini yale mambo ya kubadili, ili hatimaye, waweze kukua. Ni Roho ambaye ni mnyenyekevu hata pale anapowasahihisha waja wake, anafanya hivyo kwa upole, bila kuondoa imani kwao, bali anawapatia uhakika kuhusu uwepo na ukaribu wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu Mfariji kama Wakili na mtetezi mbele ya watu wanaowashutumu, kiasi cha kuonekana kuwa “si mali kitu” mbele ya walimwengu na mshitaki wa ndugu zao, yeye awashitakiye mbele ya Mungu wao mchana na usiku amefanya yote ili wajisikie watu wasiokuwa na furaha wala uwezo. Lakini mbele ya shutuma na mashitaka yote haya, Roho Mtakatifu Mfariji, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote waliyoambiwa na Kristo Yesu.
Kumbe, wataweza kumjibu Shetani, Ibilisi kwa maneno ya Kristo Yesu aliyekuwa anazungumza na Baba yake wa mbinguni, aliyewawezesha watoto wake kulifahamu pendo lake. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwaliko kwa waamini kumwomba, kumpokea na kukumbuka ukweli muhimu wa maisha kwamba, ni Yeye anayewalinda waamini dhidi ya shutuma na mashitaka kwa sababu wao ni watoto wapendwa wa Mungu. Jambo la kujiuliza ni kiwa kama waamini wamejenga mazoea na utamaduni wa kumwomba daima Roho Mtakatifu, kiasi cha kumsahau kwamba, ni jirani na kwamba yuko ndani mwao! Je, waamini wamekuwa makini kusikiliza sauti yake na tayari kujirekebisha pale anapowarekebisha? Je, wanaposhutumiwa katika maisha, wanajbu kwa kutumia maneno la Kristo Yesu! Je, wanakumbuka kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu? Bikira Maria awasaidie kuwa wanyenyekevu kwa sauti ya Roho Mtakatifu sanjari na kutambua uwepo wake wa daima.