Tafuta

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.   (ANSA)

Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani na Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Mfano Bora wa Kuigwa

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Kanisa katika huruma na upendo wake ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi duniani, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao, ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa vile Sikukuu hii iligubikwa sana na kilio cha wafanyakazi, machafuko, kinzani na misigano, hasa kwenye Karne ya XIX, Mama Kanisa akataka Mtakatifu Yosefu kuwa ni kielelezo makini cha mapambano ya kudai haki msingi za wafanyakazi, utu na heshima yao pamoja na kutoa hadhi kwa kazi kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kazi ya uumbaji na ukombozi ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliishiriki kiasi hata cha watu kumsema: “Huyu si yule seremala…” Mk. 6:3. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; kwa kutambua na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.

Sehemu kubwa ya vijana nchini Italia hawana fursa za ajira
Sehemu kubwa ya vijana nchini Italia hawana fursa za ajira

Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika usiku na mchana kutafuta fursa za kazi! Kanisa ni Mama na Mwalimu, daima anapenda kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu hazina budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kazi iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu, ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu, anathamini sana kazi ya uumbaji aliyoitekeleza kwa muda wa siku sita na siku ya saba akapumzika. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa wafanyakazi, aendelee kuwakumbuka na kuwaombea watu wote, ili asiyewepo kijana, familia au mtu awaye yote asiyekuwa na fursa ya ajira. Hii iwe ni dhamana inayowawajibisha watu wote. Mei Mosi ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na kuwaua wafanyakazi wanne.

Kumbukumbu ya mauaji ya halaiki mwaka 1886
Kumbukumbu ya mauaji ya halaiki mwaka 1886

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika ujumbe wake kwa Sikukuu ya Wafanyakazi kwa Mwaka 2023 linabainisha kwamba, kuna ukweli unaotia wasiwasi mkubwa kutokana na idadi kubwa ya vijana nchini Italia hawana fursa za ajira na hususan Kusini mwa Italia. Jamii haijawekeza kiasi cha kutosha ili kutoa matumaini kwa vijana wa kizazi kipya. Kama vile Papa Francisko anavyosisitiza katika Wosia wake wa Kitume “Christus vivit” akisema, Ulimwengu wa kazi ni eneo ambalo vijana hupitia hali ya kutengwa; ukosefu wa fursa za ajira, hali ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika umaskini na hivyo kufisha ndoto ya matumaini pamoja na kuwanyima fursa ya kutoa mchango katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii. Na matokeo yake ni vijana kujikatia tamaa ya maisha. Mgogoro wa idadi ya watu inazidisha hali hii na hivyo vijana wengi kutengwa hali kadhalika wanawake pia. Kinachotia wasiwasi pia ni idadi kubwa ya vijana kuhama kutoka Kusini na kukimbilia miji mikuu ya Kaskazini mwa Italia au hata kwenda nchi nyingine kutafuta fursa za ajira. Hali ya ukosefu wa usalama wa ajira ambayo vijana wengi huipata inastahili kuangaliwa hasa: pale ambapo mahitaji ya kazi ni haba, vijana wanalipwa ujira mdogo, wanaona ujuzi na umahiri wao unavyokatishwa tamaa. Kuna uwiano mdogo kati ya mahitaji na usambazaji wa kazi; kuna idadi kubwa ya vijana wasiosoma wala kufanya kazi; kiasi kwamba, vijana wengi wanajikuta wakiishia kwenye mitandao ya uhalifu, kamari, kazi haramu na za kunyonywa; matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia.

Uchumi unaolinda tamaduni na maisha ya watu husika
Uchumi unaolinda tamaduni na maisha ya watu husika

Baba Mtakatifu Francisko, kuhusiana na mada ya vijana, mara kwa mara amezungumzia kuhusu: Zawadi ya neema, dhihirisho la utu wa ndani wa mtu, chanzo na chombo cha bure. Bila kazi, kwa kweli, sio tu chanzo cha mapato kinakosekana, watu wanakosa utu wa ndani, kwa sababu kazi ni kielelezo cha utu wa mtu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya za Kikristo kuwa na mwalekeo wa Kisinodi: kwa kukutana na kusikilizana; kwa kushiriki uzuri na bidii ya Kazi; furaha ya kusaidiana na kutunzana, ili kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini mapya; kukuza na kudumisha sera ya kukuza ajira kwa vijana; sanjari na kuweka uhusiano wa kazi na shule, ili kuwa na usalama utakao saidia kudhibiti uhamiaji wa nguvu kwa kukosa fursa za ajira. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linakazia kuhusu: uchumi wa amani na sio wa vita; uchumi unaotunza kazi ya Uumbaji, kwa huduma ya mtu binafsi, familia na maisha; uchumi unaojua kutunza kila mtu na haumwachi mtu nyuma. Maaskofu wanatamani uchumi unaolinda tamaduni na mila za watu, za viumbe hai vyote na maliasili za dunia, uchumi unaopiga vita umaskini wa aina zote, unaopunguza ukosefu wa usawa na unaoweza kusema, pamoja na Yesu na pamoja na Papa Francisko; "heri walio maskini.

Uchumi shirikishi, utu heshima na haki msingi za binadamu
Uchumi shirikishi, utu heshima na haki msingi za binadamu

Huu ni mwaliko wa kuchangia katika ushiriki wa uchumi wa Kiinjili ili usiwe ni ndoto inayoelea kwenye ombwe! Huu ni mtazamo mpya wa uchumi unaozingatia kilio cha Dunia Mama na Maskini! Lengo ni kukuza nafasi za ajira kwa vijana wa kizazi kipya katika mantiki ya ikolojia ya mazingira bora nyumba ya wote. Kunahitajika muungano bora kati ya uchumi, fedha, siasa na utamaduni ili kujenga mitandao ya mshikamano itakayokuwa na uwezo wa kuwasaidia vijana wa kizazi kipya. Machipukizi haya yatakuwa ni ishara za uhakika za majira ya machipuko mapya yanayojumuisha mahusiano mazuri kati ya watu, familia zenye uwezo wa kujifungulia maisha kwa matumaini ya ujasiri, jamii ya mshikamano na kujaliana. Maaskofu Katoliki Italia wana uhakika kwamba, utendaji wa Roho Mtakatifu utazaa chipukizi jipya ulimwenguni shukrani pia kwa vizazi vijavyo. Unabii wa Yoeli tayari unatimizwa mbele ya macho yetu: “Wana wenu na binti zenu watakuwa manabii” (Yoe 3:1).

Wafanyakazi Duniani 2023
01 May 2023, 13:25