Tafuta

Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Binamu yake Elizabeti, tuombe mapendo kwa jirani. Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Binamu yake Elizabeti, tuombe mapendo kwa jirani.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti: Ushuhuda wa Imani na Fadhila

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 31 Mei ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea binamu yake Elizabeth. Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri kwa sababu alisadiki: kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana! Rej. Lk 1:45. Huu ni ushuhuda wa ujasiri wa kiimani na fadhila. Ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaookoa, kuganga na kuponya! Ushuhuda wa imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rozari takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi wa mwanadamu na ni sehemu ya maisha ya Kristo Yesu. Ni sala inayowawezesha waamini kukimbilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, kwa ajili ya kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Rozari ni sala ya waamini wa kawaida inayowahakikishia uwepo angavu na endelevu wa Bikira Maria katika safari ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Waamini wanakumbushwa umuhimu wa kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea: toba na wongofu wa ndani; utakatifu wa maisha; haki na amani; umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kama Bikira Maria alivyowataka Watoto wa Fatima, yaani: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos. Mwezi Mei umekuwa ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 31 Mei ya Kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kumtembelea binamu yake Elizabeth. Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri kwa sababu alisadiki: kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana! Rej. Lk 1:45. Huu ni ushuhuda wa ujasiri wa kiimani na fadhila. Ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaookoa na kuponya. Huu ni ushuhuda wa Injili ya matumaini, kwa watu wa Agano la Kale na kama ilivyo kwa watu wa ulimwengu mamboleo! Huu mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha, Mkombozi wa Ulimwengu unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji.

Bikira Maria anamtembelea Elizabeti, tuombe mapendo kwa jirani
Bikira Maria anamtembelea Elizabeti, tuombe mapendo kwa jirani

Bikira Maria ni Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeth. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeth ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumsalimia Elizabeth, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano bora wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutisha! Hii ni Sikukuu ya utenzi wa Bikira Maria unaojikita katika fadhila ya kusikiliza kwa makini, kutafakari na kutenda kwa imani, mapendo na matumaini. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio la imani na upendo na ambalo linatangaza utimilifu wa nyakati, kwa kuzaliwa Mkombozi wa ulimwengu anayetanguliwa na Yohane Mbatizaji. Huu ni mwaliko wa kujifunza kujisadaka kwa ajili ya huduma ya mapendo kwa Mungu na kwa ajili ya jirani, jambo ambalo lingeweza kuleta mageuzi makubwa duniani. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni tukio linalobubujika furaha inayoyajaza maisha ya watu kutokana na ujasiri wa mwanamke mwenye uwezo wa kuona, kusikia na kuguswa na mahitaji ya ndugu yake na hivyo kuwa ni chemchemi ya furaha inayowakutanisha ndugu hawa wawili. Haya ndiyo yanayosimulia na Mwinjili Luka; Injili inayobubujika furaha inayoijaza nyoyo za watu!

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila
Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila

Baba Mtakatifu anawataka wakristo kuwa ni watu wenye nyuso za furaha na tabasamu la kukata na shoka, ujumbe unaosheheni Liturujia ya Sherehe ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth kwa ajili ya huduma. Bikira Maria ni kielelezo cha mwanamke msikivu, anayetafakari na kutenda kwa ujasiri na kwa haraka, kielelezo cha ujasiri na huduma; kama inavyojionesha kwa wanawake wengi wajasiri walioko ndani ya Kanisa. Hawa ni wanawake wanaosimama kidete kutoa elimu kwa watoto wao pamoja na kuhudumia wagonjwa ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Kwao huduma inakuwa ni chemchemi ya furaha. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria na Elizabeth wanakutana katika kisima cha furaha, kama kielelezo cha huduma makini kwa jamii, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani, jambo ambalo linaweza kuleta mabadiliko makubwa duniani. Kukutana ni sehemu ya maisha ya Kikristo yanayojikita katika huduma inayowasukuma Wakristo kutoka katika ubinafsi wao, ili kuwahudumia jirani zao kwa upendo. Mwenyezi Mungu yuko kati ya watu wake, ili kuwahudumia na kuwakutanisha katika kisima cha furaha na upendo!

Bikira Maria

 

 

 

31 May 2023, 17:17