Papa:Viongozi wa mataifa wasikilize matakwa ya watu wanaoteseka&kutaka amani
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mara baada ya Tafakari na sala ya Malkia wa Mbingu, katika Dominika ya Tano ya Pasa, tarehe 7 Mei 2023, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha maadhimisho mawili yaliyofanyika Jumamosi tarehe 6 Mei kwa kutangazwa wenyeheri Askofu Jacinto Vera huko Montevideo, Uruguay, aliyeishi katika karne ya 19. Padre huyo alikuwa Mchungaji aliyewatunza watu wake, alitoa ushuhuda wa Injili kwa bidii ya kimisionari ya ukarimu, akiendeleza upatanisho wa kijamii katika mazingira magumu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mwenyeheri Maria Garcia
Vile vile huko Papa amesema huko Granada, Hispania, alitangazwa kuwa mwenyeheri Maria de la Concepción Barrecheguren y García, ambaye akiwa amelala kitandani kwa ugonjwa mbaya, alivumilia mateso hayo kwa nguvu nyingi za kiroho, na kuamsha sifa na faraja kwa wote. Alikufa mnamo 1927 akiwa na umri wa miaka 22 tu. Papa ameomba wapigiwe makofu hao wenyeheri wawili... Papa akiendelea amewasalimia waamini wote kuwanzia na Warumi na mahujaji kutoka Italia na kutoka nchi nyingi, hasa waamini kutoka Australia, Hispania, Uingereza na wanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Thomas huko Lisbon.
Chama cha Meter
Salamu zake pia kwa Chama cha Meter ambacho kinajitolea kuzuia na kupiga vita nyanyaso dhidi ya watoto na mwanzilishi wake ni Padre Fortunato Di Noto wanaoendelea na dhamira yao ya kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya watoto wadogo. Kwa hiyo katika muktadha huo Papa Francisko amekumbusha maadhimisho ya siku ya 28 ya Watoto, wahanga wa nyanyaso. Papa amesema “katika miaka 30 ya kutetea utoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili”, kwa hiyo yuko karibu nao kaka na dada na anawasindikiza kwa sala na upendo wake huko akiwaomba wasichoke kuwa upande wa waathirika kwa sababu, kuna Mtoto Kristo anayewasubiri na amewashukuru.
Papa aidha akiendelea na salamu zake amependa kuwasalimu kikundi cha wagonjwa wa Fibromyalgia kutoka eneo la Matibabu la Vicariate ya Roma; Masista wa Mtakatifu Giuseppe Benedetto Cottolengo; Chama cha Walei cha Huruma; Familia ya Walei ya Wakamilliani; waamini wa kutoka Pozzuoli, Caraglio na Valle Grana; Kwaya za Empoli na Ponte Buggianese, Italia.
Salamu kwa kikosi cha Ulinzi cha Uswisi
Papa Francisko ametoa salamu maalumu kwa kikosi cha Ulinzi wa Kipapa cha Kiswisi, kwa familia zao, marafiki na kwa mamlaka ya Uswisi walioshiriki katika sherehe za chombo hiki kinachostahili. Kwa hiyo ameomba wapigiwe makofi kwa wote Walinzi hao. Hiki ni Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswisi, kilichoundwa kunako mwaka 1506 na Papa Giulio II, chenye dhamana na utume wa kumlinda Papa. Jumamosi tarehe 6 Mei 2023 Wanajeshi hao wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi, walifanya kumbukizi ya askari 147 kutoka Uswisi waliotoa maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumlinda na kumtetea Papa Clement VII mnamo mwaka 1527. Katika tukio hilo askari wapya 23 kutoka sehemu mbalimbali za Uswisi wamekula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Sala kwa Maria wa Pompei ni ibada ya kiutamaduni
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea na salamu zake amekumbusha juu ya Sala kwa Mama Maria wa Pompei, ambayo hufanyika kiutamaduni,katia Diminika ya Pili ya Mwezi wa tano na mwezi wa kumi kwa Mama Maria wa Rosari, katika Madhabahu, ambayo Mwenyeheri Bartolo Longo aliijenga kwa kusudi la kusali kwa ajili ya amani. Kwa hiyo Papa Francisko amesema: “Katika mwezi huu wa Mei tunasali Rozari ni kumwomba Bikira Mtakatifu zawadi ya amani, hasa kwa ajili ya Ukraine inayoteswa. Viongozi wa mataifa wasikilize matakwa ya watu wanaoteseka na kutaka amani!” Kwa kuhitimisham amewatakia mlo mwema na kuwatakia baraka ya Dominika na wasisahau kusali kwa ajili yake.
Mara baada ya Tafakari na sala ya Malkia wa Mbingu katika Dominika ya tano ya Pasaka, ndani ya Studio zetu za Vatican News, tulipata mgeni aliyeshiriki Sala hiyo na Papa Francisko katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Dk. Harrison Kalunga Mwilima Mtaalamu wa masuala ya Mahusiano Kimataifa. Katika mahojiano na Dk.Harrison alianza kujitambulisha anavyotekea Tanzania na mahali anapoishi huko Berlin nchini Ujerumani na ni kwa nini alikuwa Roma ambapo ni katika muktadha wa kutoa vipindi katika Chuo Kimojawapo cha Kimataifa hapa Roma, na ikawa pia fursa ya kusimama ili kujimwilisha kiroho kwa kutembelea makanisa makuu na madhabahu kadhaa yaliyoko mjini Roma.
Mahusiano ya kweli yanaanzia katika familia
Kwa kupata fursa hiyo ya kuudhuria Sala ya Malkia wa Mbungu na Baba Mtakatifu Francisko Dk Harrison alieleza ni kitu gani kimemvutai na kuguswa katika tafakari yake. Lakini pia pamoja na shughuli zake za kila siku huko Berlin Ujerumani katika masuala ya Mahusiano kimataifa na vyuo vikuu, alielezea pia kuhusu husiano wa kifamilia kama mzazi na profesa kwa mtazamo wa uzoefu wake wa imani kuanzia na tafakari ya Papa aliyesisitiza uhusiano wa kirafiki na Bwana. Kwa mujibu wake amebainisha kwamba mahusiano yote yanaanzia ndani ya familia. Na ndiyo mzizi wa kila kitu.
Kuunganisha imani na kazi
Katika ulimwengu wa sasa wa kumbiziana hapa na pale katika maisha, Dk. Harrison aliweza pia kutoa machache kuhusu maisha ya kijamii kwa ujumla nchini Ujerumani na hasa katika mji anakoishi Berlin, kwa upande wake alisisitiza juu ya wananchi ambay wanafanya kazi kwa bidii na kwa kasi ukilinganisha na na nchi zetu kama Tanzania na vile vile watu kujali mapumziko wakati wa Dominika. Na hatimaye aliwahamasisha vijana wa shule na vyuo kuwa na bidii lakini zaidi ya hayo waunganishe imani na kazi kwa Mungu ili kuweza kupata mafanikio kwa kila jambo. Alitoa mfano wake mwenyewe, ni kwa jinsi gani alikwenda Ujerumani kama mwanafunzi na sasa ni Profesa, kwa hiyo jambo muhimu ni kuweka kipaumbele Mungu! Kwa kirefu yafuatayo ni mahojiano na Vatican News na Dk. Harrison Kalunga Mwilima: